Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amewaasa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto kuifahamu na kuiheshimu mipaka ya majukumu yao ya kisheria, akisisitiza kuwa mipaka hiyo ndiyo dira ya uongozi wao na ngao muhimu ya kuepuka migongano ya madaraka, migogoro ya kimaslahi pamoja na kuvuruga utawala wa sheria.
Rai hiyo imetolewa leo Februari 10, 2026, wilayani Kiteto wakati akifungua na kufunga Mafunzo Maalumu ya siku mbili kwa Madiwani wa Halmashauri hiyo.

Aidha, Mhe. Sendiga aliwataka madiwani hao kuyachukulia mafunzo hayo kama mwongozo wa kudumu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kiuongozi, akisisitiza kuwa uongozi bora haupimwi kwa kauli, bali kwa matendo yenye tija kwa jamii.
Katika muktadha wa maendeleo, aliwahamasisha madiwani kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa kuisaidia Serikali, hususan katika usimamizi wa miradi ya maendeleo na ukusanyaji wa mapato ya halmashauri, akibainisha kuwa uwajibikaji wao una mchango wa moja kwa moja katika kuboresha huduma za jamii.
Kuhusu amani na mshikamano wa kijamii, Mhe. Sendiga aliwaonya madiwani kutojihusisha na migogoro ya ardhi, akieleza kuwa kata yenye migogoro ya ardhi ni ishara ya kutotekelezwa ipasavyo kwa majukumu ya uongozi katika eneo husika. Vilevile, aliwataka kusimamia wananchi kufuata sheria, taratibu na miongozo ya nchi ili kulinda amani, haki na utulivu wa jamii.
Katika sekta ya elimu, aliweka mkazo maalumu kwenye suala la chakula shuleni, akiwataka madiwani kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mpango huo ili kuhakikisha kila mzazi anatimiza wajibu wake wa kuchangia chakula cha mtoto wake, akisisitiza kuwa mtoto mwenye lishe bora ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri kitaaluma na kimaadili.
Mafunzo hayo ya siku mbili, yaliyofanyika kuanzia Februari 09 hadi 10, 2026, na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, yamelenga kujenga uelewa wa kisheria, kimaadili na kiuongozi kwa madiwani, ili kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na maendeleo endelevu ya Wilaya ya Kiteto.

Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa