Katika maandalizi ya kuelekea katika mashindano ya UMISSETA Mkoa, timu ya mpira wa Miguu ya UMISSETA Kiteto imewapa kichapo cha bao 3 kwa 1 timu ya mpira wa miguu ya Kibaya watu wazima yenye mchanganyiko wa wachezaji mahiri.
Mechi hiyo ya kirafiki ambayo imechezwa Juni 9,2025 katika Uwanja wa Michezo wa Wilayani hapa , ilikuwa na lengo la kuiweka ‘fiti’ timu hiyo ya UMISSETA ambayo inatarajia kusafiri Juni 11, 2025 kuelekea Babati kwaajili ya Mashindano ya UMISSETA Mkoa wa Manyara.
Mbali na mechi hiyo, timu ya Mpira wa Wavu (Volleyball) nayo ilionekana ikifanya mazoezi katika uwanja huo.
Mbali na mpira wa miguu na mpira wa wavu, michezo mingine ambayo Wilaya ya Kiteto itashiriki katika mashindano hayo ni pamoja na mpira wa pete (netball) kwa wasichana, riadha pamoja na mpira wa meza (table tennis) kwa wavulana na wasichana.
Mratibu wa Michezo ya UMISSETA Kiteto, Mwl. Ibrahim Mmwaja, amesema kwamba wanashauku kubwa ya kutetea makombe yao yote ya mwaka jana kwani wamejiandaa vizuri pia mwaka huu.
“Mwaka jana tulichukua kombe la mpira wa miguu, volleyball, table tennis, usafi na nidhamu,” ameongeza Mmwaja.
Katika ngazi ya Taifa Mashindano ya UMISSETA kwa mwaka 2025, yatafanyika Mkoani Iringa na yameshafunguliwa Juni 9,2025 na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa. Kauli Mbinu katika mashindano hayo kwa mwaka 2025 ni “ Viongozi Bora ni Msingi wa Maendeleo ya Taaluma, Sanaa na Michezo, Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu”
UMISSETA ni Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari Tanzania ambao hukutanisha wachezaji waliochujwa kutoka shule mbalimbali za sekondari. Lengo la UMISSETA ni pamoja na kukuza vipaji vya michezo miongoni mwa wanafunzi wa shule za sekondari na kuhamasisha ushiriki wa vijana katika michezo kama njia ya kujenga afya bora na nidhamu.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa