Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mh Remedius Mwema Emmanuel, amesema kwamba yupo tayari kumchukulia hatua mtu yoyote atakayekwamisha zoezi la chanjo ya Surua Rubella inayoendelea nchi nzima.
Mh Mwema ameyasema hayo Februari 16, 2024 kwenye Ukumbi wa Maktaba katika kikao cha PHC (Primary Health Care) kuhusu Kampeni ya Chanjo ya Surua Rubella Wilaya ya Kiteto.
Mheshimiwa Mwema amesema kwamba suala la chanjo ni ajenda ya Kitaifa na anahitaji wilaya yake iwe ya kwanza katika Mkoa, hivyo hatopenda kuona mtu yoyote akikwamisha zoezi hilo na hivyo kwa yoyote ambaye atakwamisha zoezi la chanjo wilayani hapo atamchukulia hatua. “Wilaya kua ya kwanza inawezekana maana kua wa kwanza kunahitaji kuratibu na kushirikiana” aliongeza Mh. Mwema.
Lengo la kikao hicho ilikua ni kutoa elimu juu ya Kampeni ya Chanjo ya Surua Rubella inayoendela nchini kwa watoto wenye umri wa miezi 9 hadi miezi 59.
Mh Mwema amesema kwamba kupeana elimu kunasaidia kupata uelewa na viongozi wakielewa wataenda kuelimisha jamii na hivyo kuondoa dhana potofu.
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Huduma za Afya, Bi Elizabeth Joseoh Urio, amesema kwamba wananchi wanapaswa waelezwe umuhimu wa chanjo hiyo.” Wapo watu ambao wanaacha kuwapeleka watoto chanjo haswa wakiona kuna watu wengi hivyo wanaona wanapoteza muda wao ila wakifahamu umuhimu wa chanjo watahakikisha watoto wao wanapata chanjo” aliongeza Bi. Elizabeth.
Nae Mganga Mkuu wa Wilaya, Dr. Vicent Gyunda, amesema kwamba wamejipanga kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa kwa kuhakikisha wanafikia lengo na pia wanavuka lengo la uchanjaji.
Halmashauri ya Wilaya Kiteto inalenga kuchanja watoto 57,435. Mpaka kufikia siku ya pili ya Kampeni hiyo Februari 16,2024, Halmashauri imeweza kuchanja jumla ya watoto 34,418 ambapo ni sawa na 59.93% ya lengo la uchanjaji.
Chanjo ya Surua Rubella inatolewa bure kwa watoto walio na umri kuanzia miezi 9 hadi miezi 59 katika Hospitali ya Wilaya, Vituo vya Afya vyote, Zahanati zote na katika vituo maalumu vilivyoteluliwa kwa muda kutoa huduma hiyo. Kampeni hii ina lengo la kuongeza kinga kwa walengwa.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa