Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akitoa maelekezo ya serikali ,katika siku ya pili ya kikao cha baraza la madiwani Oktoba 31,2018, ndani ya ukumbi wa halmashauri .Waliokaa pembeni yake , upande wake wa kulia ni Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papian, na upande wake wa kushoto ni Makamu mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Hassan Benzi.
.........HABARI KAMILI.......
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mheshimiwa Tumaini Magessa amewataka Madiwani kulima kwa kufuata kanuni bora za kilimo , ili wananchi wanaowaongoza waweze kuiga mfano kutoka kwao. Mhe. Magessa ameyasema hayo wakati akitoa maelekezo ya serikali katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto Oktoba 31, 2018.
Akizungumza wakati akitoa maelekezo hayo Mhe. Magessa amesema kwamba kila diwani awe na mtaalamu wake mmoja ambaye atamuelekeza namna ya kulima kisasa , pamoja na kufanya ufuatiliaji wa karibu katika shamba lake ,na kwamba agizo hilo ni lazima lianze kutekelezwa katika msimu ujao wa kilimo.Akisisitiza kuhusu agizo hilo Mheshimiwa Magessa amesema “ kila diwani alime kwa kufuata kanuni za kilimo bora, na mimi nitakuwa nikitembelea shamba la diwani mmoja baada ya mwingine. Naomba niwahakikishie kwamba nitafuatilia sana suala hili, tunataka tuone mabadiliko, ambayo yameanzishwa na sisi wenyewe,lazima tulime kilimo ambacho kitakuwa cha mfano kwa watu tunaowaongoza, na zaidi sana kilimo ambacho kitakuwa na tija kwetu”.
Kadhalika Mhe Magessa amewataka wakuu wa idara na wakuu wa vitengo wote, viongozi wa chama pamoja na taasisi nyingine zote za serikali kufanya vivyo hivyo .Katika kuhakikisha kwamba ufuatiliaji wa utekelezaji wa agizo hilo unafanyika kikamilifu , Mheshimiwa Magessa amesema ‘‘najua kila mtu hapa ana shamba,wewe uliyejificha pori kwa pori kule ndani, mimi nitatembea tu,nitafika kote huko. Na ndugu zangu madaktari mjue, kama una shamba lima vizuri, fuata kanuni,waziri amesema ‘professionals’ wasikamatwe,sisi tutakukamata kwenye hoja ya shamba, sio ya udaktari.Kama umelima chini ya kiwango sisi hatutakuacha kwa sababu wewe ni daktari, tutakukamata tu kwa sababu ya kutotekeleza agizo hili la kwetu huku”.
Aidha Mheshimwa Magessa amesema kwamba hata yeye mwenyewe katika msimu ujao wa kilimo ana mpango wa kulima , na atalima kwa kufuata kanuni zote za kilimo bora. Mheshimiwa Magessa ameendelea kusema kwamba wao kama viongozi , wote wakifanya hivyo, na wakawaelekeza wanachi , na wananchi wakaelewa, na kuiga mfano kutoka kwao, wakalima kisasa, wilaya ya Kiteto itafika mbali sana kiuchumi,kwa sababu watavuna mavuno mengi ,watakuwa na chakula cha kutosha, na watakuwa na chakula kingi zaidi cha kuuza, watapata fedha nyingi, na hivyo uchumi wa mwananchi mmoja mmoja utakuwa, uchumi wa wilaya pia utakuwa .
Wilaya ya Kiteto ni miongoni mwa wilaya ambazo kilimo ni moja wapo ya shughuli kuu ya kiuchumi inayofanywa na wananchi wengi,lakini wengi wao, wamekuwa wakilima kilimo cha mazoea, hawalimi kwa kufuata kanuni za kilimo bora, jambo ambalo linasababisha kilimo hicho kutokuwa na tija kwao, hali ya kuwa wanalima maeneo makubwa,wanatumia nguvu nyingi, muda mwingi na fedha nyingi kulima,lakini mavuno yanayopatikana hayalingani na uwekezaji uliofanyika .
.................MWISHO......................
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa