Wajumbe wa kamati ya lishe wakiendeklea na kikao
Mwenyekiti( Christopher Simwimba aliyeko kushoto) na katibu wa kikao ( Dkt. Paschal Malkiad Mbota aliyekaa kulia) wakifuatilia kwa makini majadiliano kuhusu taarifa zilizowasilishwa kwenye kikao cha kamati ya lishe.
Wajumbe wa kamati wakifuatilia kwa makini uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji wa shughuuli za lishe.
.........HABARI KAMILI..............
Kamati ya lishe wilaya ya Kiteto imeitaka idara ya afya na usafi wa mazingira kufuatilia kwa karibu biashara zote zinazohusisha bidhaa za vyakula, ili kuipeusha jamii na madhara yatokanayo na ulaji wa vyakula vilivyoisha muda wake, na vilivyotayarishwa na kuhifadhiwa katika hali isiyo salama.Azimio hilo limeafikiwa katika kikao cha kamati ya lishe kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto asubuhi ya leo tarehe 15.01.2019.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wajumbe wa kamati ya lishe wamesema kwamba ziko bidhaa ambazo hata muda wake wa matumizi hauonekani,vilevile wamezungumzia kuhusu uhifadhi wa vyakula na huduma ya chakula kwa ujumla katika migahawa ambapo wameitaka idara ya afya na usafi wa mazingira kutoa elimu kwa wamiliki wa migahawa, kuhusu madhara ya kuhifadhi vyakula vya moto katika mifuko ya plastiki, pia kuhakikisha kwamba vyakula wanavyowauzia wateja wao ni vyamoto, sambamba na kuwahudumia wateja katika hali ya usafi ,na kuweka mazingira ya migahawa yao katika hali ya usafi.
Naye Afisa lishe wa wilaya ya Kiteto bibi Beatrice Rutanjuka ametoa angalizo kuhusiana na bidhaa ambazo muda wake wa matumizi umekwisha, hapa Rutanjuka anasema “Mwaka umekwisha sasa, tumeingia mwaka mwingine, kuna bidhaa ambazo muda wake wa matumizi utakuwa umekwisha, lakini bado zinaendelea kuuzwa. Na kutokana na watanzania wengi kutokuwa na utamaduni wa kuangalia muda wa matumizi kabla ya kununua bidhaa, wataendelea kuzinunua na kuzitumia.Matumizi ya bidhaa hizo yanaweza kuwasababishia walaji kupata saratani. Ni vema idara ya afya na usafi wa mazingira ifanye ukaguzi wa kina ili bidhaa zilizoisha muda wake ziondolewe sokoni”.
Kadhalika Rutanjuka amezungumzia kuhusu matumizi ya chumvi , ambapo amewataka watu kutumie chumvi zenye madini joto.Amesisitiza kuwa hakuna mahali ambapo mtu anaweza kupata madini joto, zaidi ya kwenye chumvi,hivyo ni muhimu kwa idara ya afya na wajumbe wote wa kamati ya lishe kuweka msisitizo katika kuelimisha jamii kutumia chumvi yenye madini joto.
Rutanjuka pia amezungumzia kuhusu chumvi zinazouzwa magulioni ambazo hazina madini joto, ambapo amesema kwamba ni vema idara ya afya ikafanya utafiti kufahamu upatikanaji wa chumvi hiyo ni wa kiasi gani,wasambazaji wake ni wakina nani ili taarifa sahihi kuhusu upatikanaji wa bidhaa hiyo zipatikane, zitumwe mkoani, Afisa lishe mkoa afanye utaratibu wa kuagiza madini joto, chumvi hiyo iwekewe madini hayo kabla haijasambazwa kwa wafanyabiashara warejareja na kuwafikia walaji.Kwani ni vizuri kutafuta suluhisho la tatizo, kwa kuiwekea madini joto chumvi hiyo kuliko kuzuia isiuzwe, hali ya kuwa chumvi hiyo imekuwa ikichimbwa ,na watu wameendelea kufanya biashara hiyo kwa miaka mingi.
Aidha baadhi ya wajumbe wamehoji kuhusu ubora wa mafuta ya alizeti ambayo yanakamuliwa na viwanda vidogo vidogo vilivyoko wilayani hapa, usalama wa mafuta yanayouzwa na wanyabiashara wadogo, ambayo hupatikana baada ya kuchemsha mabaki ya alizeti iliyokwisha kukamuliwa viwandani maarufu kama tope na ladha ya uchungu ambayo wakati mwingine husikika katika mafuta hayo.
Akijibu hoja za wajumbe kuhusu mafuta ya alizeti mwakilishi wa umoja wa viwanda vidogo vidogo vya kukamua alizeti ndugu Mohamed Ismail amesema kwamba mafuta yanayotokana na kuchemshwa kwa mabaki ya alizeti iliyokwisha kamuliwa sio salama kwa walaji. Kuhusu ladha ya uchungu kwenye mafuta Ismail amesema kwamba baadhi ya wakulima wa alizeti huvuna alizeti ikiwa haijakomaa vizuri, vilevile alizeti isipopepetwa vizuri, na ikakamuliwa ikiwa na pumba,pumba hizo husababisha mafuta kuwa na ladha ya uchungu.
Katika hatua nyingine kaimu afisa afya na usafi wa mazingira wilaya ya Kiteto ndugu Ezekieli Kimolo amesema kwamba baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakifanya biashara ya kukamua alizeti kiholea bila kujisajili hivyo wanapowatembelea kwa ajili ya ukaguzi hufunga na kukimbia.Vilevile amezungumizia kuhusu uhifadhi wa alizeti kabla ya kukamuliwa, ambapo amesema kwamba wafanyabiashara wengi huhifadhi mahali ambapo hakuna sehemu za kuingiza hewa, na wakati mwingine huhifadhi chini kwenye sakafu, jambo ambalo linasababisha alizeti kuharibika, hivyo kusababisha mafuta yanayokamuliwa kutokuwa na ubora na ladha inayotakiwa.
Hata hivyo Kimolo amesisitiza kwamba wamekuwa wakifuatilia na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara sio kwenye viwanda vya kukamua alizeti tu, bali kwa wafanyabiashara wote wa bidhaa za vyakula, na kwamba ufuatiliaji wa karibu zaidi utaendelea ili kuendelea kulinda afya za walaji.
Kikao hicho cha robo ya pili ya mwaka,kilikuwa na ajenda 8, moja wapo ya ajenda hizo ikiwa ni uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji wa shughuli za lishe ambapo idara na vitengo mbalimbali vya Halmashauri vinavyohusika na masuala ya lishe kama idara ya mifugo, idara ya kilimo,idara ya maji, idara ya mipango, idara ya elimu msingi, idara ya elimu sekondari,idara ya maendeleo ya jamii, idara ya afya na usafi wa mazingira,kitengo cha lishe, kitengo cha dawa na vifaa tiba, kitengo cha afya ya uzazi na mtoto, pamoja na taasisi mbalimbali kama Umoja wa Viwanda Vidogo Vidogo Kiteto, Baraza la Waislamu (BAKWATA)-wilaya ya Kiteto,‘Mwanasatu Development Organization’ (MWADO) ziliwasilisha taarifa zake.Ajenda nyingine ilikuwa ni majadiliano kuhusu taarifa zilizowasilishwa pamoja na kuweka maazimio .
.........MWISHO..........
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa