Mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Manyara Ndg. Anold Msuya akizungumza katika baraza maalumu la kujadili hoja za ukaguzi kwa mwaka 2016/2017.Baraza hilo limefanyika ndani ya ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto.
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akimkaribisha mwakilishi wa mkuu wa mkoa kuzungumza katika baraza maalumu la kujadili hoja za ukaguzi kwa mwaka 2016/2017.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto Mhe. Lairumbe Mollel akizungumza katika baraza maalumu la kujadili hoja za ukaguzi kwa mwaka 2016/2017.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto Ndg. Tamim Kambona akizungumza katika baraza maalumu la kujadili hoja za ukaguzi kwa mwaka 2016/2017.
Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papian akizungumza katika baraza maalumu la kujadili hoja za ukaguzi kwa mwaka 2016/2017.
Wahe. Madiwani pamoja na wakuu wa idara na vitengo vya halmashauri wakiwa katika baraza maalumu la kujadili hoja za ukaguzi kwa mwaka 2016/2017.
.....HABARI KAMILI......
Mkuu wa mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti ametoa pongezi kwa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto kwa kupata hati safi katika ukaguzi mwaka 2016/2017.Pongezi hizo zimetolewa na mwakilishi wake ambaye pia ni afisa elimu wa mkoa wa Manyara ndugu Anold Msuya wakati wa kikao cha baraza maalum la madiwani la kujadili hoja za ukaguzi kwa mwaka 2016/2017 lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri mapema jana.
Katika hotuba yake iliyosomwa na mwakilishi wake Mhe. Mnyeti amesema kwamba pamoja na kupata hati safi, baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Kiteto lisimamie kwa ukamilifu kuhakikisha kwamba maeneo yaliyotajwa kuwa na udhaifu na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali kwa mwaka 2016/2017 yanafanyiwa kazi kikamilifu,ikiwemo kujibu hoja za miaka ya nyuma , pamoja na maagizo ya kamati ya kudumu ya bunge ya hesabu za serikali.
Aidha Mhe. Mnyeti amesema kwamba Kila mkuu wa idara na kitengo atalazima kuwajibika na kushiriki kikamilifu wakati wa ukaguzi,tofauti na utaratibu ambao umekuwepo miaka ya nyuma ambapo jukumu la kujibu hoja za ukaguzi liliachwa kwa mweka hazina pamoja na watendaji wake wa idara ya fedha na mkaguzi wa ndani.
Mhe Mnyeti amesisitiza kuwa katika utaratibu wa sasa, atakaepaswa kujibu hoja za ukaguzi ni mkuu wa idara au kitengo kilichohusika kuzalisha hoja . Na kwamba wakuu wa idara na vitengo watawajibika kuhangaika ili kuzuia hoja zisitokee, na pale zitakapokuwa zimetokea, watawajibika kutafuta majibu ya hoja hizo.Na kwamba wakuu wa idara na vitengo wanapaswa kuwajibika kikamilifu kuhakikisha kwamba idara na vitengo vyao havizalishi hoja, na endapo zitazaliwa hoja, wakuu wa idara na vitengo vilivyozalisha hoja hizo watawajibishwa.
Kadhalika Mhe Mnyeti amelipongeza baraza la madiwani kwa usimamizi mzuri, na kuwataka Wahe. madiwani kuhakikisha kwamba wanaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha , ili Halmashauri yao iendelee kupata hati safi.
Katika hatua nyingine mwakilishi huyo wa mkuu wa mkoa ametoa pongezi kwa waheshimiwa madiwani pamoja na watendaji wote wa Halmashauri wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji ndugu Tamim Kambona kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo.Akitoa pongezi hizo ndugu Msuya amesema,“ Jana nilifanikiwa kutembelea miradi yenu, nimejionea jinsi ambavyo miradi yenu mnayoitekeleza ilivyo katika viwango vya juu kabisa. Miradi inatekelezwa kwa kasi na kwa ubora unaotakiwa.Kama kuna jambo Kiteto la kujivunia, ni kuwa na baraza makini kama hili, na kuwa na Mkurugenzi anayesimamia watendaji wakafanya kazi kwa ubora na kwa uadilifu mkubwa namna hii”.
Naye Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa ametoa rai kwa watendaji wote ambapo amesema kwamba kwa sababu Halmashauri imepata hati safi, wanatakiwa kuwa makini katika utendaji ili kuzuia kuwepo kwa hoja nyingine . Akisisitiza kuhusu umakini katika utendaji Mhe. Magessa anasema “ Tusipokuwa makini maana yake ni kwamba tutaendelea kuacumulate hoja, wakati tayari zimeanza kufutwa, kwa hiyo tutegemee kabisa kwamba hatuwezi kuacumulate tena hoja zingine.Wakaguzi wako hapa. Mara nyingi hoja hizi zinakuja kwa sababu ya kutokuwa na utii, yaani unafanya mambo nje ya kanuni,kwa hiyo kufanya mambo kwa kutokufuata kanuni ndiko kunasababisha hizi hoja tunazoziona”.
Mhe Magessa amewataka watendaji wote kuhakikisha kwamba wanafuata kanuni katika utendaji wao ili wasiendelee kuzalisha hoja nyingine. Akisisitiza kuhusu kauli yake hiyo Mhe Magessa amesema “Kama Halmashauri ni vizuri tukaelezana kwamba kila mmoja katika nafasi yake afuate kanuni.Kanuni ya serikali inasema nini fanya hicho, inaposhindikana kabisa basi tufuate utaratibu mwingine ambao tunaweza kuomba kufanya jambo fulani pasipo kuiingiza Halmashauri kwenye hoja’’.
Baraza maalumu la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Kiteto limekaa ijumaa kwa lengo la kujadili hoja za mkaguzi wa hesabu za serikali kwa mwaka 2016/2017. Jumla ya hoja Hoja 151, ziliibuliwa katika ukaguzi huo. Kati ya hoja hizo 151, hoja 101 ni za miaka ya nyuma, ambapo hoja 92 zimefungwa .Hoja za mwaka unaoishia Juni 2017 ni hoja 50 , kati ya hoja hizo 50, hoja 32 zimefungwa.
........MWISHO.........
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa