Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya juma la elimu ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akihutubia wakati wa maadhimisho hayo,ambayo kiwilaya yamefanyika katika viwanja vya shule ya sekondari Kibaya.
Kaimu Mkurugenzi ambaye pia ni Afisa Elimu Msingi (W) Mwl. Emmanuel Mwagala akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya juma la elimu wilayani kiteto.
Walimu ,wanafunzi pamoja na wadau mbalimbali wa elimu wakiwa katika maandamano ya kilele cha maadhimisho ya juma la elimu wilayani Kiteto.
Mgeni rasmi na ujumbe wake alioambatana nao wakiwa katika vyumba vya maonyesho kuhusu mada mbalimbali za masomo,huku wanafunzi wakionyesha umahiri mkubwa katka kutoa maelezo kuhusiana na mada hizo.
Wanafunzi wakiimba wimbo katika kilele cha maadhimisho ya juma la elimu wilayani Kiteto.Maadhimisho hayo yamefanyika katika viwanja vya shule ya sekondari Kibaya mwishoni mwa juma.
Walimu , wanafunzi,wazazi pamoja na wadau mbalimbali wa elimu wakiwa wamekusanyika katika kilele cha maadhimisho ya juma la elimu wilayani Kiteto.Maadhimisho hayo yamefanyika katika shule ya sekondari Kibaya mwishoni mwa juma.
.....HABARI KAMILI......
Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya juma la elimu , ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Kiteto Mheshimiwa Tumaini Magessa amewataka wanafunzi kuwa na utayari wa kusoma kwa bidii ili waweze kuwa na maendeleo mazuri kielimu na kupata matokeo mazuri katika mitihani . Mhe. Magessa ameyasema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya juma la elimu, ambayo kiwilaya yamefanyika katika shule ya sekondari Kibaya mwishoni mwa juma.
Akizungumza wakati wa hotuba yake, Mhe Magessa ameweka mkazo katika uwajibikaji wa pamoja,kwa walimu na wanafunzi ,kwamba wote wanawajibu wa kutimiza ili kupata matokeo mazuri katika elimu. Hapa Mhe. Magessa anasema “ Sisi viongozi tunatarajia mambo makubwa kutoka kwenu ,msituangushe. Wanafunzi wekeni bidii katika kusoma kwa hiyari yenu, hiyari ndio inayoweza kubadilisha matokeo ya wilaya yetu.Kwa sababu hata kama walimu wakifundisha kwa bidii, kama wanafunzi hamjahiyari kufanya vizuri,haiwezi kuleta matokeo mazuri”.
Kadhalika Mhe Magessa amewapongeza walimu kwa juhudi wanazozifanya katika kuboresha elimu ,ambapo amesema kwamba serikali itawalipa kwa juhudi hizo.Huku akiwataka wanafunzi kutojihusisha katika mambo ambayo yatawasababisha kutokuzingatia masomo yao.Akisisitiza kuhusu hilo Mhe. Magessa anasema “Nimesikia kwamba kuna wanafunzi wanaokesha disko siku za mwisho wa wiki.Tutawakamata na tutawashughulikia.Mwanafunzi uliyeko hapa tunakutegemea utoe matokeo mazuri kwenye elimu.Achana na mambo mengine, shughulika na elimu. Kazi ya wanafunzi iwe moja tu kusoma,na walimu wafundishe tupate matokeo”.
Aidha Mhe. Magessa ameeleza mikakati yake ya kuhakikisha kwamba Kiteto inafanya vizuri kwenye elimu, ambapo mikakati hiyo ni kutembelea shule zote kukagua namna ya ufundishaji kwa kuingia darasani kuuliza maswali yanayohusiana na masomo yanayofundishwa ili kuhakikisha kama wanafunzi wanaelewa wanachofundishwa , kuzungumza na wazazi kuhusu namna ya kuweka utaratibu ili wanafunzi waweze kupata kifungua kinywa na chakula cha mchana shuleni, ambapo katika kufanikisha hili amewata wakuu wa shule zote kuandaa siku ya wazazi kuja shule yaani ‘parents day’ na yeye aalikwe ili kwa pamoja waweze kuzungumzia suala hilo ,pamoja na masuala mbalimbali yatakayosaidia kuinua kiwango cha taaluma .
Mkakati mwingine ni kufanya jitihada za kupata walimu wa masomo ya sayansi pamoja na masomo mengine ambayo hayana walimu kwa kuwatumia walimu wa masomo hayo wanaofundisha katika shule za jirani ndani ya wilaya .
Katika hatua nyingine zawadi mbalimbali zimetolewa na kukabidhiwa kwa wahusika na Mgeni rasmi Mhe Magessa ambapo shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya taifa mwaka 2017 zimezawadiwa , Shule ya Sekondari Ecco na shule ya msingi Laalakiri kila moja ikipewa shilingi 1,000,000, shule ya sekondari Lesoiti na shule ya msingi Sunya kila moja ikipewa shilingi 700,000 , shule ya sekondari Engusero na shule ya msingi Kibaya kila moja ikipewa shilingi 500,000.
Vilevile shule 12, 4 zikiwa za sekondari na 8 za msingi zilizoshiriki katika kuandaa maonyesho mbalimbali kwa ajili ya maadhimisho ya juma la elimu zimezawadiwa kiasi cha shilingi 20,000 kila moja .Pia wanamichezo waliowakilisha wilaya katika UMISETA ngazi ya taifa na kufanya vizuri katika michezo mbalimbali nao wametunukiwa vyeti vya pongezi, .
Juma la elimu huadhimishwa kila mwaka, ambapo kwa mwaka 2018 Kauli mbiu inasema “Uwajibikaji wa Pamoja Katika Kutoa Elimu Bora”.
..........MWISHO.........
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa