Katibu tawala wa wilaya ya Kiteto ndugu Stephano Ndaki akiwatambulisha wajumbe wa kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya
Wajumbe wa kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya wakifuatilia kwa makini taarifa mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa katika kikao hicho
Mweka hazina wa wilaya ya Kiteto ndugu Nassoro Mkwanda akiwasilisha taarifa ya mapato ya ndani ya halmashauri ya wilaya ya Kiteto ya kuanzia mwezi Julai - Septemba 2017
Kaimu afisa mipango wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto ndugu Edga Kavenuke akiwasilisha taarifa ya bajeti ya hamashauri ya wilaya ya Kiteto kwa mwaka 2017/2018 na taarifa ya utekelezaji wa miradi kwa mwaka 2016/2017
Meneja wa TRA wilaya ya Kiteto ndugu Willjones Kisamba akiwasilisha taarifa ya mapato ya serikali kuu kwaka 2016/2017.
Wajumbe wa kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya wakishauri juu ya taarifa mbalimbali zilizowasilishwa katika kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya
Habari kamili.....
Kiteto yafanya kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya
Wilaya ya kiteto imefanya kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya baada ya miaka mitano.Mara ya mwisho kikao hicho kilifanyika mwaka 2013.Akimkaribisha mwenyekiti kwa ajili ya kufungua kikao hicho, katibu tawala wa wilaya ya Kiteto ndugu Stephano Ndaki amesema kwamba vikao hivyo vimekuwa havifanyiki kwa muda mrefu kutokana na gharama za kuviendesha kuwa kubwa kwa sababu ilikuwa ni lazima wajumbe walipwe posho, jambo ambalo lilikuwa linasababisha vikao hivi kutokukaa, lakini kwa utaratibu wa sasa vikao hivyo vitakaa kwa gharama nafuu, ambayo ni gharama ya chakula na nauli kwa wajumbe wanaotoka mbali sana, kwani umuhimu wa vikao hivyo ni mkubwa sana kuliko kuangalia zaidi kupata posho halafu wakashindwa kukaa.
Akifungua kikao hicho mkuu wa wilaya ya Kiteto mheshimiwa Tumaini magesa ambaye kwa mujibu wa sheria ndiye mwenyekiti, amesema kwamba migogoro ya wakulima na wafugaji imeendelea kutatuliwa , na wao kama viongozi kazi yao ni kuhakikisha kuwa migogoro hiyo inakwisha , japokuwa kawaida ya Kiteto inaeleweka kwamba kila wanapotatua mgogoro mmoja ,yule ambaye katika utatuzi wa mgogoro anaona haki haikuwa kwa upande wake , anadhani mwenzake ametoa rushwa. Lakini anaamini kwamba watakuwa wanakwenda vizuri kadiri watatakavyokuwa wanakutana katika vikao kama hivyo kwani mambo yote ili yaweze kwenda vizuri ni muhimu kuwa wanakutana kwenye vikao, watakapokuwa wanakutana migogoro itakuwa inakwenda ikipungua kwa sababu kila mmoja atakuwa anajua kinachoendelea.
Kwa upande wa ulinzi na usalama, mwenyekikiti amesema kwamba hali ya ulinzi na usalama katika wilaya ya Kiteto imeimarika ,kuna matukio machache ya uhalifu, lakini vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi yake, na kuwataka wajumbe tuviruhusu vyombo hivyo vifanye kazi . Aidha mwenyekiti amewahakikishia wajumbe wa kikao hicho kwamba yeye kwa kushirikiana na kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya wanaendelea kupambana kuhakikisha kwamba wanafika mahali ambapo wilaya ya Kiteto itakuwa imetulia ,na kwamba ikitulia kila mmoja atafanya shughuli za maendeleo katika utaratibu ambao unakubalika na serikali na atakula matunda ya uhuru.
Katika kikao hicho taarifa mbalimbali ziliwasilishwa, wajumbe walizijadili na kutoa ushauri ambapo katika taarifa ya bajeti ya mwaka 2017/18 wajumbe walishauri kwamba ni vyema halmashauri ikajikita zaidi katika ukusanyaji wa mapato kwa kuwa fedha zinazoletwa na serikali kuu hazilingani na kazi na miradi ambayo halmashauri inapaswa kuitekeleza, hali ambayo inasababisha kukwama kwa miradi ya maendeleo. Wajumbe walishauri kwamba minada iliyokuwepo miaka ya 1980 ya Kijungu na Ndedo ifunguliwe na maeneo mengine mazuri yatafutwe ili kuwezesha biashara ya mifugo kuiletea halmashauri ya wilaya ya Kiteto mapato na siyo wilaya jirani kama ilivyo sasa. Wajumbe walishauri kwamba halmashauri iweke utaratibu wa kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji wakubwa ili kuanza kuchangia maendeleo kwa mwaka.
Vilevile wajumbe walishauri mamlaka ya mji mdogo wa Kibaya iendelee kutafuta vyanzo vya mapato ili kuiwezesha kujiendesha vizuri.Aidha wajumbe walishauri elimu iendelee kutolewa kwa kata za Njoro na Partimbo ili waridhie kuwa sehemu ya mamlaka ya mji mdogo wa Kibaya.Wajumbe walishauri kwamba ili kupata mapato ni vyema mabaraza ya kata ambayo yalivunjwa kwa mujibu wa sheria yaundwe kabla ya mwezi Desemba 2017, kwani mabaraza hayo ni moja wapo ya vyanzo vya mapato vya halmashauri. Kwa upande wa ukusanyaji mapato wa TRA wajumbe walishauri kwamba elimu zaidi itolewe kwa wafanyabiashara juu ya matumizi ya mashine za kutolea risiti za kielekroniki yaani EFD.Na watumiaji wa huduma mbalimbali waelimishwe juu ya umuhimu wa kudai risiti.
Katika kujadili suala la migogoro ya ardhi,wajumbe walishauri kuwa wataalamu pamoja na viongozi wasimamie matumizi bora ya ardhi ili kuondoa migogoro.Aidha walishauri kuwa miundo mbinu katika maeneo ya kilimo na ufugaji iboreshwe ili kuwezesha wahusika kufanya shughuli zao bila migogoro na kwa usalama zaidi,katika kipengele cha usalama wa watu na mali zao, wajumbe walisisitiza zaidi juu ya alama za barabarani kwa ajili ya kuonyesha maeneo ya kuvukia binadamu na mifugo,hususani katika barabara kuu.
Katika suala la afya,wajumbe walishauri elimu na hamasa itolewe zaidi kwa jamii ili jamii iweze kuona umuhimu wa kujiunga na bima ya afya iliyoboresha ,ili kupunguza gharama za matibabu ,na kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wote ili waweze kufanya shughuli za kiuchumi na kujiletea maendeleo.Aidha baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya hali ya vyoo katika wilaya, wajumbe walishauri halmashauri kuweka mkakati maalum wa kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa vyoo na matumizi ya vyoo ,halmashauri iweke faini kwa kaya ambazo zitakuwa hazikujenga vyoo katika muda fulani ambao utakuwa umepangwa ili kudhibiti hali ya uchafu katika mazingira ya wilaya na kuzuia milipuko ya magonjwa.Wakati huohuo wajumbe walipokea taarifa ya maandalizi ya kilimo kwa mwaka 2017/2018 na walishauri kuwa elimu ya hali ya hewa iwafikie wananchi wote ili kujiandaa kwa kilimo kulingana na hali ya hewa .Pia wajumbe walishauri juu ya suala la ruzuku ya pembejeo kufuatiliwa mapema na idara husika ili kujua kama zinapatikana.
Katika hatua nyingine wajumbe waliweka maazimio ishirini (20),ambapo maazimio hayo yaliafikiwa baada ya mijadala ya kina iliyotokana na taarifa zilizowasilishwa na wataalamu mbalimbali wa halmashjauri na mamlaka ya mapato wilaya ya Kiteto. Maazimio hayo ni kuboresha mapato ya halmashauri ya wilaya kwa kuongeza vyanzo vya mapato na kuwa na vitega uchumi.Wadau kuendelea kushirikiana na TRA ili kuhakikisha kwamba mapato ya serikali yanakusanywa ili kuweza kupata fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.Taarifa ya kutowasilishwa kwa fedha za miradi ya maendeleo iwasilishwe kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) ili kamati hiyo iweze kusaidia kusukuma jambo hilo, ili fedha hizo ziweze kuwasilishwa kwa wakati. Viongozi wa wilaya wafuatilie moja kwa moja katika wizara husika fedha za miradi ya maendeleo. Minada iboreshwe kwa kujenga miundo mbinu kama vile vyoo,barabara , sehemu za kuingilia na kutokea mifugo, kuweka uzio ili kuzuia watu kutorosha mifugo kabla ya kuilipia ushuru. Halmashauri ianzishe minada katika maeneo ya Ndedo na Kijungu. Mabaraza ya kata yawezeshwe kwa kupatiwa mafunzo na vitendea kazi.Elimu itolewe kwa wafugaji, wapeleke mifugo minadani na badala ya kuuzia majumbani. Alama za barabarani ziwekwe ili kutambua vivuko vya binadamu na mifugo.Wadau waendelee kuhamasishwa kuingia katika uchumi wa viwanda. Vijiji vitoe maeneo ili kuvutia wawekezaji,aidha halmashauri ya wilaya pamoja na vijiji viendelee kutenga maeneo hayo.Vijiji vizingatie matumizi bora ya ardhi. Mabwana afya wasimamie usafi ipasavyo badala ya kukaa ofisini. Katika zile siku maalumu zilizoamriwa za kufanya usafi, wananchi wote washiriki katika usafi wa mazingira,biashara zote zifungwe. Kuwepo na tathmini ya elimu katika ngazi ya vijiji hadi katika ngazi ya halmashauri ya wilaya . Vijiji ambavyo havina shule ,ifikapo 2018 viwe na shule mfano Ngapapa.Kuboresha miundo mbinu ya shule mfano madarasa, vyoo na nyumba za walimu .Wananchi waelimishwe namna ya uchangiaji wa mfuko wa bima ya afya iliyoboreshwa. Serikali ishauriwe juu ya fedha za TASAF, fedha za TASAF III zielekezwe zaidi kwenye miradi ya maendeleo ambapo itanufaisha watu wengi zaidi kuliko inavyofanyika sasa ambapo kaya maskini hupewa fedha hizo lakini wengi wao wanaopewa fedha hizo huzitumia vibaya mfano kuongeza wake, kulewa , matumizi ambayo husababisha fedha hizo kutokuwanufaisha hata wao wenyewe.Wakulima na wafugaji wahamasishwe kulima na kufuga kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo na ufugaji bora ili mifugo na kilimo hicho viweze kuwaletea maendeleo na pia kutoharibu mazingira .
Akifunga kikao hicho mwenyekiti aliwashukuru wajumbe wote kwa kushiriki katika kikao hicho na kusisitiza kuwa maazimio yaliyofikiwa yafanyiwe kazi kwa wakati .Aidha kikao kingine cha kamati hiyo kitafanyika mnamo mwezi wa tatu mwaka 2018.
Kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya ni kikao cha juu katika wilaya. Kikao hiki hukaa mara mbili kwa mwaka, mwezi wa tatu na mwezi wa kumi. kikao hiki hukutana kupokea na kupitia mpango wa maendeleo wa halmashauri na kisha kushauri ili utekelezaji uweze kufanyika ipasavyo, kupitia taarifa mbalimbali za miradi mbalimbali ya kitaifa na kuweza kushauri, kusimamia na kushauri uendeshwaji wa taasisi zisizokuwa za kiserikali kwenye wilaya na kusimamia na kuhakikisha kwamba halmashauri inatekeleza mpango wake wa bajeti kama ilivyokusudiwa . Kamati ya ushauri ya wilaya iliundwa kwa mujibu wa sheria ya serikali za mitaa ya mwaka 2006 kipengele cha 15a – 15 b ambapo mwenyekiti wa kikao cha kamati hiyo ni mkuu wa wilaya.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa