Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papian akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika makao makuu ya kata ya makame wilayani Kiteto,wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za maendeleo katika jimbo lake.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kiteto Ndg. Mohamed Kiondo akizungumza katika mkutano huo.
Katibu wa mbunge wa jimbo la Kiteto ambaye pia ni diwani wa kata ya Kaloleni Mhe. Christopher Permet akizungumza katika mkutano huo.
Wananchi wa kata ya makame wakiwasilisha kero zao kwa mbunge katika mkutano huo.
Wananchi wa kata ya makame wakiwa wamekusanyika katika mkutano wa hadhara kumsikiliza mbunge wao Mhe . Emmanuel Papian.
........HABARI KAMILI......
Mbunge wa Kiteto Mhe. Emmanuel Papian ameahidi kushughulikia tatizo la maji katika kata ya makame.Mhe Papian ametoa ahadi hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya makame,wakati wa ziara yake katika kata hiyo.
Akizungumza katika mkutano huo Mhe. Papian amesema kwamba anafahamu kuwa Makame kuna shida ya maji, na kwamba yeye pamoja na viongozi wengine kwa muda sasa wamekuwa katika kufikiri ni kwa namna gani watatatua kero hiyo ya maji. Amewahakikishia wananchi hao kwamba tatizo hilo linashughulikiwa ,na kwamba katika mwaka wa fedha 2018/2019 atahakikisha kuwa maji yanapatikana katika kata hiyo kama ambavyo yamepatikana katika kata ya Ndedo.
Mhe Papian ameeleza namna ambavyo tatizo hilo la maji linaweza kutatuliwa, Mhe. Papian amesema “Kuna kisima hapa,hakijafungwa pamp, tunataka tupambane ,tuhangaikie tupate mkandarasi aje hapa kisima kifungwe pampu, kifungwe sola,na hata ikiwezekana kisima kingine kichimbwe maji yapatikane hapa makame”.
Aidha Mhe. Mbunge amesema kwamba kazi yake kubwa ni kusukuma maendeleo, hivyo amewataka wakazi wa kata ya makame kuendelea kushirikiana nae ili kwa pamoja waweze kuleta maendeleo katika kata hiyo .
Kadhalika Mhe. Papian ameeleza mikakati yake ya kuboresha sekta ya elimu , Mhe. Papian amesema “Tunataka kuinua kiwango cha elimu hapa makame, mkakati wetu ni kwamba katika ajira za serikali za mwaka 2018/2019 tutaongeza walimu hapa.Tunajenga madarasa, tunajenga bweni, wanafunzi wakae bwenini wasome vizuri”.
Katika mkutano huo pia wananchi wa makame wamewasilisha kero kwa mbunge wao, huku kero kubwa ikiwa ni tatizo la maji na ugonjwa wa maralia, ambapo ugonjwa huo umesababisha vifo vya wanafunzi 5 wa shule ya msingi makame.Akijibu kuhusu tatizo la ugonjwa wa malaria Mhe Papian amewataka wazazi na walezi wote kuhakikisha kwamba wananunua vyandarua,watoto wao na wao wenyewe walale katika vyandarua ili kujikinga na mbu, kwa upande wa tiba Mhe . Papian ameahidi kuzungumza na wahusika kwa lengo la kuweka utaratibu wa kupeleka dawa nyingi za malaria ,wananchi wanapougua waweze kupata dawa mapema ,ili vifo vinavyotokana na malaria visiendelee kutokea katika kata hiyo.
............MWISHO................
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa