Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya KIteto, CPA. Hawa Abdul Hassan, amewagiza wasimamizi wa miradi ya ujenzi wilayani Kiteto kuhakikisha kuwa inatekelezwa kwa ubora unaotakiwa ili thamani ya pesa ionekane.
Hayo ameyazungumza katika ziara yake ya kukagua miradi Mei 4, 2024 akiwa ameongozana na Mkuu wa Idara ya Elimu ya Awali na Msingi, Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari, Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi, Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu pamoja na wahandisi wa Ujenzi wa Halmashauri.
Katika kila mradi ambapo alipita kukagua, Mkurugenzi amesisitiza mambo matatu ambayo ni kuongezwa kwa kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati, ubora wa miradi hiyo pamoja na matumizi bora ya fedha (Value for Money).
Aidha amesema maelekezo hayo siyo kwa ajili ya miradi hiyo tu bali ni kwa miradi yote inayoendelea kutekelezwa wilayani Kiteto.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi, Ndugu Godfrey Mwangairo, amesisitiza kufuata utaratibu wa serikali wa manunuzi ya umma katika mfumo wa kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NEST).
Ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo ilianzia katika Hospitali ya Wilaya kwa kukagua ukamilishaji wa mradi wa majengo matatu kisha kuelekea katika shule ya Msingi Chemchem na kukagua mradi wa vyoo matundu 11 na kutoa maelekezo ya kuanza kwa ujenzi wa chumba kimoja cha darasa katika shule hiyo. Maagizo hayo pia yametolewa katika shule ya Msingi Msente.
Aidha Mkurugenzi pamoja na timu yake alikagua ujenzi wa nyumba nne za wakuu wa idara pamoja na nyumba ya mkurugenzi zinazojengwa katika eneo la Bwagamoyo. Mkurugenzi huyo aliendelea na ziara yake katika Shule ya Sekondari Kiteto na kukagua ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa pamoja na ujenzi wa vyoo matundu manane shuleni hapo. Ujenzi wa chumba kimoja cha darasa pamoja na ukamilishaji wa boma la chumba cha darasa katika Shule ya Sekondari Bwakalo pia ulikaguliwa katika ziara hiyo.
Vilevile Mkurugenzi huyo alipita kukagua ujenzi wa bweni la watoto wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Partimbo na pia kukagua ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa pamoja na vyoo matundu manane katika Shule ya Sekondari Partimbo. Mradi kama huu pia unatekelezwa katika shule ya Sekondari Njoro ambapo timu hiyo pia ilifika kukagua.
Jumla ya miradi tisa ilikaguliwa katika ziara hiyo ya siku moja. Miradi yote hiyo ina jumla ya thamani ya TZS 1.9 bilioni ambapo ni fedha kutoka serikali kuu na pia kutoka Mapato ya Ndani ya Halmashauri katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa