Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti Kuzungumza na wakazi wa Kata ya Njoro Katika Mkutano wa Hadhara Uliofanyika Katika Kata hiyo Wilayani Kiteto.
Mbunge wa Jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papiani akijitambulisha Katika Mkutano wa Hadhara Uliofanyika Katika Kata ya Njoro Wilayani Kiteto.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Awataka Watumishi Wilayani Kiteto Kuishi katika Maeneo Yao ya Kazi
Mkuuu wa mkoa wa Manyara mheshimiwa Alexander Mnyeti amewataka watumishi wilayani Kiteto kuishi katika maeneo wanayofanyia kazi ili iwe rahisi kupatikana wakati wote wananchi wanapowahitaji.Mheshimiwa Mnyeti ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Njoro, kata ya Njoro wilayani Kiteto kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu watendaji wa vijiji pamoja na mtendaji wa kata kuishi nje ya kata hiyo.
Akizungumza katika mkutano huo Mhe. Mnyeti amesema kwamba watumishi wanatakiwa kuishi katika maeneo wanayofanyia kazi,na kama mtu hawezi kufanya hivyo aache kazi. Katika kutaka kuthibitisha madai ya wananchi kuhusu watendaji hao , Mhe. Mnyeti aliwataka watumishi wote wa serikali waliokuwepo katika mkutano huo kupita mbele na kila mmoja kueleza mahali anakoishi, na na hapo ikabainika kwamba watendaji wote wa vijiji pamoja na mtendaji kata wanaishi Kibaya. Ndipo Mheshimiwa Mnyeti akatoa agizo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto ndugu Tamim Kambona kuwahamisha watumishi wote ambao hawaishi katika kata hiyo. Mhe. Mnyeti anasema ‘‘Mkurugenzi hamisha watendaji wote hawa ambao hawaishi Njoro peleka katika vijiji na kata zilizoko mwisho wa mipaka kabisa ya wilaya hii”. Sambamba na agizo hilo, Mhe. Mnyeti ametoa kiasi cha shilingi za Kitanzania 1,000,000 kwa walimu , daktari na wauguzi wa zahanati ya Njoro ambao wanaishi katika maeneo yao ya kazi.
Vilevile Mhe. Mnyeti ametoa agizo kwamba mlima Simu uhifadhiwe kwa ukamilifu. Agizo hilo hilo la mheshimiwa Mnyeti limetokana na baadhi ya wakazi wa kata hiyo kuwasilisha kero zao kwake, ambapo kero kubwa ni wakazi wa kijiji cha Njoro kunyang’anywa mashamba yao na kufanywa kuwa sehemu ya hifadhi, jambo ambalo linasababisha wao kukosa mashamba ya kulima hali ya yakuwa wao wanategemea kilimo kuendesha maisha yao . RC Myeti kwa kutaka kujua ukweli wa jambo hilo akawaagiza watu wote wenye mashamba katka mlima huo kupeleka vithibitisho vyao ambavyo vinaonyesha kwamba wao ni wamiliki halali wa mashamba hayo ili wapatiwe mashamba mengine.Na hapa mheshimiwa Mnyeti anasema “ Watu wote wenye mashamba katka mlima wa simu pelekeni kwa mkuu wa wilaya vithibitisho vyenu vyote vinaonyesha kwamba ninyi ni wamiliki halali wa mashamba katika mlima huo. Ikithibitika pasipo shaka kwamba ninyi ni wamiliki halali, jiorodhesheni majina yenu mpeleke kwa mkuu wa Wilaya,mimi nitajua nitakako wapeleka kuwapatia mashamba.Nataka mlima huu uhifadhiwe kikamilifu kwa manufaa ya vizazi vijavyo,lakini pia sitaki kumuonea mtu’’.
Kero nyingine zilizowasilishwa na wananchi katika mkutano huo ni pamoja na uchakavu wa majengo ya madarasa katika shule ya Msingi Njoro,migogoro ya mipaka,mgogoro kati ya kata ya Njoro na Kata ya Partimbo unaohusu umiliki wa eneo la mlima ambalo lina minara ya makampuni ya simu ,mwenyekiti wa kijiji cha Njoro kutoonyesha ushirikiano pindi anapopewa taarifa za matatizo mbalimbali ya wakazi wa kijiji hicho na matibabu ya wazee ambapo mzee mmoja alimueleza mheshimiwa Mnyeti kwamba hawajapewa kadi za matibabu zinazotolewa kwa wazee jambo ambalo linawapa wakati mgumu pale wanapohitaji kutibiwa.
Mheshimiwa Mnyeti akatoa majibu ya kero hizo ambapo katika kero ya uchakavu wa madarasa Mhe. Mnyeti amewataka wananchi kuchangia ujenzi wa majengo hayo ,na wakishaonyesha nguvu zao serikali itamalizia. Pia amechangia shilingi 1,000,000 kwa ajili ya ukarabati wa madarasa katika shule hiyo. Kadhalika amemtaka afisa mipango wa Wilaya ya Kiteto (DPLO) ndugu Beatrice Lumbeli kuwaelimisha wananchi kuhusu kuibua miradi itakayopelekwa katika vikao husika ili itakapopitishwa na kutekelezwa katika kata zao itokane na vipaumbele vyao kuondoa malalamiko na kuwafanya wananchi hao kuithamini miradi hiyo. Katika hili Mheshimiwa myeti anasema “ waelimisheni hawa watu jinsi ya kuibua miradi.Afisa mipango tembelea vijiji vyote waelimishe wananchi’’.
Kuhusu Migogoro ya mipaka, Mhe. Mnyeti ametoa rai kwa wananchi kuacha kuchochea migogoro hiyo, kwani mipaka hiyo imewekwa kwa sababu za kiutawala na haina athari kwa mwananchi yeyote hivyo isiwe sababu ya wananchi kugombana. Pia amewaonya wanasiasa kutochochea migogoro ya mipaka kwa sababu zao za kisiasa .Mhe.Mnyeti anasema “ Acheni kufanya siasa kwenye maisha ya watu,nitawashughulikia”.
Katika kutatua mgogoro wa umiliki wa eneo lenye minara Mhe. Mnyeti amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa kuipitia mikataba yote ili kujua minara hiyo iko upande gani kati ya Njoro au Partimbo.Kuhusu mwenyekiti wa kijiji cha Njoro Mhe. Mnyeti anasema “ mwenyekiti umelalamikiwa sana . Busara ni wewe mwenywe kujitathmini kama unatosha au la.Kama ukiona unatosha endelea,kama utaona hutoshi pisha’’. Kwa upande wa matibabu ya wazee Mhe. Mnyeti alimtaka mganga mkuu wa Wilaya ya Kiteto Daktari Malkiadi Mbota kujibu kero hiyo ambapo Dkt. Mbota amesema kwamba wazee kuanzia miaka 60 wanatibiwa bure,na katika utaratibu wa kuwatambua , mchakato ulishaanza ,na tayari jumla ya wazee 100 wa kata hiyo wameshapewa vitambulisho vya matibabu. Vilevile Mhe. Mnyeti amechangia kiasi cha shilingi milioni moja kwa ajiri ya marekebisho ya zahanati ya Kijiji cha Njoro.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa