Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti Akisikiliza Kero Mbalimbali Zilizokuwa Zikiwasilishwa Wakati wa Kikao Chake na Watumishi wa Serikali,Wenyeviti wa Vijiji Pamoja na Wahe. Madiwani kilichofanyika ndani ya ukumbi wa Kituo cha Jamii (Community Center) Kibaya - Kiteto
Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa Akiwasilisha Taarifa ya Wilaya kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti Katika Kikao cha Mhe. Mkuu wa Mkoa na Watumishi wa Serikali,Wenyeviti wa Vijiji Pamoja na Wahe. Madiwani .
Watumishi wa Serikali,Wenyeviti wa Vijiji ,Wahe. Madiwani pamoja na Kamati ya siasa ya wilaya ya Kiteto wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti ndani ya Ukumbi wa Kituo cha Jamii ( Community Center) Kibaya - Kiteto.
RC MNYETI KUWASHUGHULIKIA WACHOCHEZI WA MIGOGORO KITETO
Mkuu wa mkoa wa Manyara mheshimiwa Alexander Mnyeti ameahidi kuwachukulia hatua watu wote wanaochochea migogoro wilayani Kiteto. Mheshimiwa Mnyeti ameyasema hayo katika kikao chake na watumishi wa serikali,wenyeviti wa vijiji pamoja na waheshimiwa madiwani kilichofanyika ndani ya ukumbi wa kituo cha jamii (Community Center) kilichopo katika mji mdogo wa Kibaya .
Akizungumza katika kikao hicho mheshimiwa Mnyeti amesema kwamba iko migogoro ya ardhi inayoendelea wilayani Kiteto, kazi kubwa imefanywa na watangulizi waliotangulia katika kushughulikia migogoro hiyo, mkuu wa wilaya aliyeko sasa amefanya kazi kubwa kupunguza migogoro hiyo, na kwamba imefika wakati sasa migogoro hiyo ifike mwisho. Kadhalika mheshimiwa Mnyeti amesema kuwa migogoro ya Kiteto ina sura nyingi, kwani ipo migogoro ambayo ni ya muda mrefu sana,ipo migogoro yenye mantiki ,lakini pia ipo migogoro isiyo na mantiki ambayo inasababishwa na wanasiasa na watu wengine ambao wanaichochea migogoro hiyo kwa faida zao binafsi,
Aidha mheshimiwa Mnyeti amekemea vikali tabia ya baadhi ya watu kufufua na kuendeleza migogoro ambayo ilishatatuliwa, ambapo amewataka kuacha mara moja tabia hiyo, na hapa mheshimiwa Mnyeti anasema‘‘Migogoro ya Kiteto imewachosha watu, hatuwezi kuwa tunaendekezana, tunavumiliana kumbe yuko mtu ambaye kwa migogoro hii yeye ananufaika . Anachochea migogoro halafu anakaa pembeni anasubiri bomu lilipuke DC ukimbizane. Jana nimesikia sentensi moja mtu anasema bora sasa Rais alete DC mwingine tuwe na maDC wawili, mmoja awe kazi yake ni kushugulikia migogoro, na mwingine wa kutafuta maendeleo ya Kiteto. Serikali haiwezi kufanya biashara ya namna hiyo, nitawachulia hatua’’. Pia amewataka wakazi wa Kiteto kufahamu kwamba maelekezo yote ya serikali wilayani yanatolewa na mkuu wa wilaya .Mkuu wa wilaya ndiye mtu wa mwisho,maelekezo yake ndio sahihi na ndio ya mwisho,hivyo mtu mwingine yeyote haruhusiwi kutoa maagizo juu ya maagizo ya mkuu wa wilaya.
Mheshimiwa Mnyeti pia amewataka watumishi wa serikali kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kwani kumekuwepo na vitendo vya utovu wa nidhamu kwa baadhi ya watumishi, hususani tabia ya ulevi uliokithiri na watumishi kutofika katika vituo vyao vya kazi. Vitendo ambavyo vinasababisha wananchi kulalamika kwa kukosa huduma.
Katika hatua nyingine mheshimiwa Mnyeti amezungumzia suala la elimu, ambapo amesema kwamba mkoa wa Manyara ni wa mwisho katika matokeo ya mitihani ya darasa la saba.Kutokana na hali hiyo, Mheshimiwa mnyeti ametengua uteuzi wa waratibu elimu kata pamoja na walimu wakuu wa shule zote ambazo hazikufikia ufaulu wa asilimia hamsini(50%) katika matokeo ya mitihani ya darasa la saba kwa mwaka 2017. Vilevile amemuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto ndugu Tamim Kambona kuhakikisha kwamba shule zote zinakuwa na uwiano sawa wa walimu, na kwamba uhamisho uanze mara moja kuhamisha walimu kutoka katika shule zenye walimu wengi, hususani shule zilizoko maeneo ya mijini na kuwapeleka katika shule zenye walimu wachache ambazo ziko vijijini. Sambamba na hilo mheshimiwa Mnyeti amempongeza mkuu wa wilaya ya Kiteto mheshimiwa Tumaini Magessa kwa hatua anazochukua katika kupambana na tatizo la mimba mashuleni na amemtaka kuongeza jitihada zaidi ili kuondoa tatizo hilo.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa