Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Cuthbert Sendiga, Februari 19, 2025 amezindua Huduma ya Kliniki ya Madaktari Bingwa na Bobezi awamu ya pili katika Mkoa wa Manyara.
Kliniki hiyo ambayo imeanza Februari 17, 2025 katika hospitali ya Wilaya ya Kiteto iliyopo kata ya Kibaya, inahusisha huduma za kibingwa za Magonjwa ya Ndani, Upasuaji, Watoto, Wanawake na Afya ya Uzazi pamoja na huduma za kibingwa za Masikio Pua na Koo.
Katika uzinduzi huo, Mhe. Sendiga, ametoa wito kwa wananchi wa Kiteto na wilaya za jirani kufika hospitalini hapo ili kupata huduma hizo za madaktari bingwa na bobezi kabla ya kufungwa kwa zoezi hilo Februari 21,2025.
Mbali na kufanya uzinduzi huo, akiwa katika eneo hilo la hospitali ya Wilaya, Mhe. Sendinga pia amezindua pia Mradi wa Ujenzi wa miundo mbinu ya uvunaji wa maji ya mvua, usimikaji wa vifaa vya kuzalisha umeme wa jua (Solar System) na ujenzi wa shimo la kutupia kondo la nyuma la mama, mradi ambao unafadhiliwa na shirika la “Pathfinder International”.
Kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya uvunaji wa maji ya mvua, utawanufaisha wananchi wa Wilaya ya Kiteto zaidi ya laki tatu, kupata huduma bora za afya katika hospitali ya Wilaya – Kibaya kwani mradi huo utaondoa changamoto ya kuharibika kwa vifaa tiba wakati wa utakasaji kwakua maji yanayopatikana Kiteto ni ya chumvi, huku kukamilika kwa usimikaji wa vifaa vya umeme wa jua, utasaidia upatikanaji umeme mbadala mara umeme wa gridi ya taifa unapokatika.
Mbali na hayo, Mhe. Mkuu wa Mkoa huyo, alikabidhi pikipiki mbili zilizotolewa na Wizara ya Afya kwaajili ya shughuli za chanjo na pia alikabidhi jenereta lililotolewa na Bohari ya Dawa (MSD).
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa