Jumla ya madawati 358 yamegawiwa katika shule za msingi 16 wilayani Kiteto katika mpango mkakati wa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati katika shule za msingi.
Hafla hiyo ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali na Chama, baadhi ya madiwani, Kaimu Mkurugenzi, Watumishi, wananchi pamoja na wanafunzi, imefanyika Machi 21, 2024 katika viwanja vya Shule ya Msingi Kaloleni ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mh. Remidius Mwema.
Akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa madawati katika shule za msingi, Mkuu wa Idara ya Elimu ya Awali na Msingi Mwl. Papakinyi Kaai amesema kwamba, Halmashauri inahitaji jumla ya madawati 21,883 ya kukaliwa na wanafunzi watatu watatu, ila kwa sasa Halmashauri ina madawati 14,281 hivyo kuna upungufu wa madawati 14,281.
Aidha Mwl. Papakinyi amesema kwamba upungufu huo wa madawati unasababisha wanafunzi wengi kubanana kwenye dawati moja na katika baadhi ya shule wanafunzi wengine wanakaa chini darasani kwa kukosa madawati.
“Hali hii inasababisha kwa kiwango kikubwa kazi ya ufundishaji na ujifunzaji kuwa ngumu na matokeo yake wanafunzi wengi wa wilaya ya Kiteto hawafanyi vizuri katika maendeleo ya kitaaluma,” ameongeza Mwl. Papakinyi.
Ili kukabiliana na upungufu wa madawati, Wilaya ilikuja na mpango mkakati wa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati katika shule za msingi ambapo toka mpango huo uanze Novemba 2022, mpaka Machi 2024, jumla ya madawati 3,353 yamekwisha tengenezwa na kati ya hayo madawati 358 yamekadhiwa kwa shule 16 kwenye hafla hiyo.
Akiongea kabla ya kukabidhi madawati hayo, Mh. Mwema amewapongeza wadau wote na jamii kwa ujumla kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa ajili ya kupatikana kwa madawati hayo.
Vilevile Mh. Mwema ameishukuru serikali ya Mh. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa fedha ambazo wilaya inazipokea kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ambayo madawati pia yanatengenezwa kupitia miradi hiyo.
Aidha Mh. Mwema ameahidi kuendeleza kampeni ya upatikanaji wa madawati na aliwasihi wadau na wananchi kwa ujumla kuendelea kuhamasishana ili kuwezesha Halmashauri kumaliza kabisa changamoto ya upungufu wa madawati.
“Nitoe pongezi za dhati kwa jitihada za Idara ya Elimu ya Awali na Msingi katika kukabiliana na changamoto hii ya upungufu wa madawati ila niwaombe jitihada hizi ziende sambamba na kuongezeka kwa ufaulu” aliongeza Mh. Mwema.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Mh. Abdalla Bundala, amewapongeza wote waliochangia kupatikana kwa madawati hayo.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa