Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, SSI. Mbaraka Alhaji Batenga, ameagiza kila shule ya sekondari na msingi wilayani hapo kulima angalau heka kumi ili kuwapunguzia wazazi gharama ya kuchangia chakula shuleni.
Hayo ameyaongea katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) wilayani hapo kilichofanyika Novemba 27,2023.
Katika kukabiliana na tatizo la lishe nchini, serikali iliamua wanafunzi wote lazma wale angalau mlo mmoja shuleni. Kutokana na agizo hilo kila mzazi anawajibika kuchangia chakula shuleni.
Mkuu wa Wilaya amesema endapo kila shule watalima angalau heka kumi, mazao yatakayopatikana yatatumika kama sehemu ya chakula hivyo itawapunguzia wazazi mzigo wa kuchangia chakula.
“Na ili kilimo kiwe chenye tija, ni lazma kuacha kilimo cha mazoea, ni lazma sasa wafuate kanuni bora za kilimo ikiwemo kulima kwa wakati, kupanda kwa wakati, matumizi ya mbegu bora; matumizi sahihi ya mbolea na kupalilia kwa wakati” amesema Mh. Batenga.
Mkuu huyo wa Wilaya aliongeza kwa kusema matumizi ya mbolea si lazma iwe mbolea ya dukani bali hata samadi inaweza kuongeza uzalishaji wa mazao.
Katika hatua nyingine, Kaimu Mkuu wa Idara ya Kilimo na Mifugo, Ndugu Said Sembade, aliiambia Kamati hiyo kua Kampuni ya Minjingu imeahidi kutoa mbolea tani 2 kwa shule 10 za msingi na shule 10 za sekondari.
“Mashamba katika shule hizo zitakazopokea mbolea, yatatumika kama mashamba madarasa. Lengo la utoaji wa mbolea kwenye shule hizo ni kuongeza uzalishaji na tija ili shule ziweze kukeleza agizo la lishe kwa wanafunzi”, aliongeza Sembade.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa