Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti Akiwasalimia Wanafunzi wa Shule ya Msingi Partimbo katika Ziara Yake Shule ya Msingi Partimbo.
Wanafunzi wa Bweni Katika Shule ya Msingi Partimbo Wakipiga Makofi kama Ishara ya Kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti Alipotembelea Shule Hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti Akitoa Maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa Katika Ziara Yake Shule ya Msingi Partimbo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Ndg. Tamim Kambona Akifafanua Jambo Mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti Katika Ziara Shule ya Msingi Partimbo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Partimbo Mwl. Donald Mazengo Akiwasilisha Taarifa ya Shule Yake Mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti ,Wakati wa Ziara ya Mhe. Mnyeti Katika Shule Hiyo.
Majengo ya shule ya sekondari Partimbo ,Shule ambayo Ujenzi Wake Ulianzishwa kwa Fedha Zilizochangwa na Wananchi wa Kata ya Partimbo.
.............HABARI KAMILI...........
''Vyakula vya Shule Visinunuliwe kwa Zabuni’’ - RC Mnyeti
Mkuu wa mkoa wa Manyara mheshimiwa Alexander Mnyeti amewataka wakuu wa shule kuacha kununua vyakula vya shule kwa zabuni, badala yake wanunue kwa bei ya soko ili kupunguza gharama.Mheshimiwa Mnyeti ameyasema hayo akiwa katika ziara yake katika shule ya msingi partimbo, iliyopo kata ya Partimbo wilayani Kiteto ,baada ya mkuu wa shule hiyo mwalimu Donald Mazengo kueleza changamoto zinazoikabili shule hiyo ikiwemo upungufu wa fedha za chakula ambapo shule hiyo inapata shilingi 8,331,529 kwa mwezi , idadi ya wanafunzi wa bweni ikiwa ni 265.Na hivyo kuwa na upungufu wa takribani shilingi milioni tano .
Kabla ya kujibu kuhusu changamoto hiyo Mhe. Mnyeti akataka maelezo kutoka kwa kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara ndugu Anold Msuya . Hapa Msuya anasema ‘‘Ni kweli shule hii inapata kiasi hicho cha fedha, lakini tulishatoa maelekezo ambayo yalitolewa na TAMISEMI, na tulileta hapa halmashauri kwamba kamati za shule zitanunua chakula.Kwa hiyo wajitahidi kununua chakula kwa bei ya soko na sio kwa zabuni.Wakifuata utaratibu huo,wakinunua chakula wakati wa mavuno ,watanunua kwa bei ndogo,kwa hiyo chakula kile kitachukua muda mrefu kuliko ambavyo kingenunuliwa na wazabuni’’. Baada ya majibu ya katibu Tawala wa Mkoa Mhe. Mnyeti akauliza kuhusu utaratibu unaotumika kununua chakula shuleni hapo ambapo mwalimu Mazengo alijibu kwamba chakula kinanunuliwa kwa zabuni, ndipo Mhe. Mnyeti akatoa tamko kwamba vyakula visinunuliwe kwa zabuni,badala yake wakuu wa shule wanunue vyakula wenyewe.Akisisitiza kuhusu tamko hilo Mhe. Mnyeti anasema “kununua vyakula kwa zabuni ni gharama kubwa sana, hivyo fedha inayotolewa na serikali kwa ajili ya chakula kwa mwezi haiwezi kutosha.Lakini mwalimu mkuu ukinunua vyakula mwenyewe kwa bei ya soko fedha hizo zinatosha sana.Kwa watoto 265 ,shilingi 8,331,529 kwa mwezi zinatosha kabisa, kama utanunua vyakula mwenyewe.Hakikisha watoto wanakula wanashiba ,nunua mwenyewe vyakula’’.
Aidha Mhe. Mnyeti akataka ufafanuzi kutoka kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto ndugu Tamimu Kambona kwa nini vyakula vya shule vinanunuliwa kwa zabuni , hali ya kuwa maelekezo kuhusu manunuzi ya vyakula hivyo yalishatolewa. Hapa Mkurugenzi Kambona anatoa ufafanuzi anasema ‘‘ tulishawaambia kwa mwaka huu kwamba utaratibu ni huo ,lakini tuliwaambia tukiwa tumechelewa.Na mimi mwenyewe ndiye niliye gundua tatizo ,ambapo kule Ndedo tulikuta chakula cha zabuni kinauzwa gunia moja la unga shilingi 200,000 ,nikaja kufuatilia mchakato wote kujua nini kilitokea,baadae tukawaagiza wazabuni wote wakae bei hizo zishuke.Tulipambana sana , bei ya gunia la unga ikatoka kwenye shilingi 200,000 ikashuka hadi 120,000 , na vitu vingine pia vikaendelea kupunguzwa bei. Lakini na mimi niliagiza niliwaambia kwamba kuanzia sasa zoezi hili la kutumia wazabuni life.Nataka wakuu wa shule wanunue vyakula wenyewe”.
Changamoto nyingine zinazoikabili shule ya msingi Partimbo ni uchakavu wa majengo, ukosefu wa umeme na kutokuwa na uzio . Kuhusu changamoto ya shule hiyo kutokuwa na uzio, mwalimu Mazengo amemueleza Mhe. Mnyeti kwamba kutokana na shule hiyo kutokuwa na uzio walimu wanapata shida sana kuwadhibiti wanafunzi kwa sababu wanafunzi hao huchukuliwa kutoka sehemu mbalimbali ambapo sehemu hizo wazazi hawapendi watoto wao waende shule,hivyo kutokana na kutokuwa na uzio kuna wazazi wanakuja kuwatorosha wanafunzi, na wanafunzi wengine hutoroka wenyewe,lakini kama kungekuwa na uzio wangeweza kuwadhibiti .Akijibu kuhusu changamoto hiyo Mhe. Mnyeti anasema “ Mkurugenzi anza na hili la uzio.Hii shule ipe kipaumbele kwa sababu watoto wanaweza wakazidi zaidi ya hapo.Wale wote wanaohangaika huko vijijini wakiletwa hapa hii shule itakuwa kubwa sana,sasa sio lazima ufanye kwa mara moja ,anza ujenzi kwa awamu kulingana na uwezo wa halmashauri.Kama ulivyofanya pale hospitali,umefanya kazi kubwa sana .Uwezo wako tunauona ,na tunaujua ,sasa hebu fanya na hapa walimu wanapata shida ,unaweza kuwasaidia kwa kuwajengea ukuta”.
Kuhusu changamoto ya uchakavu wa majengo , Mhe.Mnyeti alimtaka Mkurugenzi kutoa majibu ,na hapa mkurugenzi anasema “ Suala la ukarabati tumeanza ,hizi shule za bweni ziko saba,tulianza na shule ya Kibaya na kule Ndedo .Hii shule iko kwenye bajeti kwa mwaka huu wa fedha tunaoendelea nao.Tunategemea wakati wowote fedha za ruzuku ya maendeleo (LGDG) zikiingia tutakuja kufanya ukarabati wa majengo katika shue hii”.
Kwa upande wa changamoto ya kutokuwepo kwa umeme katika shule hiyo. Mhe. Mnyeti amemtaka katibu tawala wa mkoa kumuandikia barua meneja wa TANESCO wilaya ya Kiteto atume wataalamu wake katika shule hiyo, wafanye tathimini, waseme nini kinahitajika ili umeme uweze kufika shuleni hapo wanafunzi wa bweni wanaosoma katika shule hiyo wasiendelee kukaa gizani.
Wakati huohuo Mhe. Mnyeti amefanya ziara katika shule ya sekondari Partimbo ambapo amewapongeza wananchi wa kata ya Partimbo kwa kuweza kuanzisha ujenzi wa shule ya sekondari katika kata yao na kumtaka ndugu Msuya ambaye ndiye afisa elimu Mkoa kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapangwa kwenda kusoma katika shule hiyo na vilevile walimu wapangiwe kufundisha katika shule hiyo, ili ianze kufanya kazi mara moja,wananchi wasiendelee kuona kwamba nguvu zao zimepotea bure. Akisisitiza kuhusu kuanza kazi kwa shule hiyo Mhe. Mnyeti anasema “ wananchi wanapoanzisha miradi ya maendeleo ni vema miradi hiyo ikasimamiwa na kuanza kufanya kazi zilizokusudiwa ili wasione kwamba wamepoteza nguvu zao. Watieni moyo wananchi kwa kuleta walimu na wanafunzi katika shule hii, ufundishaji uanze mara moja”.
Shule ya sekondari Partimbo ilianza kujengwa mwaka 2010 kwa nguvu za wananchi, ambapo wananchi hao walichangia shilingi 11,000,000 na kufanikiwa kukamilisha ujenzi wa madarasa matatu.Halmashauri ya wilaya ya Kiteto kupitia fedha za ndani za halmashauri shilingi 10,000,000 ,fedha za elimu ( Perfomance for Result) shilingi 11,000,000 , fedha za mfuko wa jimbo shilingi 13,000,000 na fedha za ruzuku ya maendeleo shilingi 20,000,000 ( LGDG) imejenga madarasa mawili, maabara mbili , moja ya somo la kemia na nyingine ya somo la baiolojia, maktaba pamoja na vyoo; choo cha wanafunzi chenye jumla ya matundu nane na choo cha walimu, matundu mawili .Hadi sasa madarasa matano na maabara moja ya somo la baiolojia ujenzi wake umekamilika, maabara moja ya somo la kemia, maktaba pamoja na vyoo viko katika hatua ya umaliziaji ( finishing).
...............MWISHO...............
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa