Daktari wa Mifugo Wilaya ya Kiteto Dkt. Lunonu Sigala akielezea kuhusu ugonjwa wa mifugo unaosababisha mifugo mingi kufa wilayani Kiteto.
Pichani ni mabaki ya nyama ambayo imetokana na mifugo iliyochinjwa baada ya kufa. Ulaji wa nyama hizi ,na mazingira haya ya upatikanaji wake ,ndio chanzo cha mlipuko wa ugojwa wa kuharisha na kutapika katika baadhi ya vijiji wilayani Kiteto.
Hali ilivyo sasa katika baadhi ya maeneo ya wafugaji wilayani Kiteto ambapo mifugo imekuwa ikianguka na kufa na wafugaji kuacha mizoga ikizagaa, kitu ambacho ni hatari sana kwa afya za binadamu na viumbe hai wengine.
( Picha zote ni kwa hisani ya idara ya afya mazingira na idara ya mifugo wilaya ya Kiteto)
............... HABARI KAMILI..............
Wakazi wa Kiteto Watakiwa Kuchukua Tahadhari Kuhusu Ulaji wa Nyama
Wakazi wa wilaya ya kiteto mkoani Manyara wametakiwa kuchukua tahadhari kuhusu ulaji wa nyama ambayo haijakaguliwa na wataalamu wa mifugo, pia kuhakikisha kwamba nyama inahifadhiwa na kuandaliwa vizuri na kwa umakini kabla ya haijaliwa. Tahadhari hiyo imetolewa na Afisa afya mazingira wilaya ya Kiteto ndugu Israel Nyalubeli kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa kuharisha na kutapika ambao umevikumba vijiji vya Krash, Ndirgishi visimani na Taigo vilivyopo katika kata ya Ndirgishi na kijiji cha Emarti kilichopo katika kata ya Magungu. Nyalubeli amesema kwamba ugonjwa huo unatokana na kula nyama ya mifugo ambayo imeugua ugonjwa unaosababishwa na kupe jina la kitaalam Ndigana baridi ( Anaplasmosis) .
Akitoa taarifa ya mlipuko wa ugonjwa huo Nyalubeli amesema kwamba dalili za wagonjwa wote waliougua kutokana na kula nyama hizo ni kuharisha na kutapika ,dalili ambazo zinafanana na dalili za kipindupindu. Ambapo amesema kwamba hadi sasa jumla ya watu 43 wameugua ugonjwa huo , na watu 5 wamefariki. Nyalubeli ameanisha mambo matatu ambayo yanaweza kuwa chanzo cha ugonjwa huo , ambapo amesema kuwa jambo la kwanza ni nyama kutohifadhiwa vizuri ,ambapo inakuwa ni mazalia mazuri sana ya wadudu , wadudu hao hutengeneza sumu, sumu ikishakuwepo kwenye nyama , hata ipikwe vipi haiwezi kwisha, hivyo yeyote atayekula nyama hiyo atapata madhara. Jambo la pili ni nyama kutoandaliwa vizuri, Nyama isipoandaliwa vizuri wadudu hai wanaokuepo kwenye nyama hiyo husababisha madhara kwa mlaji. Jambo la tatu ni mabaki ya dawa kwenye nyama. Dawa hizo zinakuwa sumu , hivyo binadamu anapokula nyama hiyo hupata madhara. Hapa Nyalubeli anafafanua zaidi kuhusu madhara ya kula nyama ambayo imetokana na mfugo uliogua na kutibiwa kwa dawa nyingi anasema ‘‘Kinachotokea ni kwamba mifugo inapougua inahudumiwa kwa dawa, na inapokufa dawa hizo zinabaki kwenye nyama. Kwa hiyo zikifa ndugu zetu wafugaji wao wanachojali ni ngozi, wanachuna ngozi kimnyakimnya, na wanajua kabisa kwamba wakila zile nyama zinaweza kuwadhuru kwa hiyo wanachofanya wanauza hiyo mifugo kwa bei nafuu, watu wananunua nyama wanakula na ndio hapo sasa wanaharisha na kutapika. Serikali ina utaratibu wa kuyaripoti haya magonjwa,kwa hiyo ambacho tunajua hadi sasa sampuli za mifugo zimepimwa, kwa matokeo ya hapa wilayani imeonekana ni aina fulani ya wadudu ambao wanatokana na kupe.Lakini kwa sampuli zilizopelekwa wizarani ,mpaka jana tunaongea na dakatari wa mifugo majibu yake yalikuwa hayajarudi.Lakini angalau tunataarifa za mwanzo kwamba chanzo ni hao wadudu.Kwa hiyo tunachokifanya ni kuchukua tu tahadhari kuelimisha watu kwa msisitizo kwamba mizoga isiliwe,mizoga izikwe.Yaani iondoke kabisa kwenye uso wa dunia kwa sababu ikishaingia kwenye mzunguko wa maji ikaingia kwenye mzunguko wa chakula hakuna atakae kuwa salama na ndio maana sasa tunaenda mpaka kwenye eneo la machinjio , kusimamia ule utaratibu wa kawaida kwamba ng’ombe anakaguliwa siku moja kabla ya kuchinjwa na nyama inakaguliwa baada ya kuchinjwa . Ndio tunawekeza nguvu huko kwa sababu unaweza kushtukia hapa mtu ametoa ng’ombe wake huko anamuona anataka kufa akampigia mchinjaji njoo ununue kumbe ni kundi lilelile . Kwa hiyo kila mtu yuko kwenye hatari hiyo.Kwa sababu hiyo basi, tumesema kwamba maeneo yote ambayo nyama inaliwa ,wahakikishe kweli ni nyama ambayo imechinjwa ,imekaguliwa na kufuata taratibu zote zinazotakiwa’’.
Kadhalika Nyalubeli ameainisha hatua ambazo zimechukuliwa na wataalamu wa afya katika kudhibiti ugonjwa huo .Hatua hizo ni kuchuua historia kamili ya wagojwa hao kutoka kwa uongozi wa vijiji na familia zilizotoa wagonjwa, kutembelea wagonjwa na kuwapa dawa za kinga tiba , kusimamia na kuhakikisha kwamba wagonjwa wanapelekwa kituo cha huduma ya afya (Engusero HC) kwa matibabu zaidi, kuhudhuria mazishi ya mmojawapo kati ya waliofariki kwa ugonjwa huo na kutoa elimu ya afya kwenye mazishi; ya kuwa pindi anapopatikana mgonjwa yeyote wa kuhara na kutapika akimbizwe haraka kwenye kituo cha kutolea huduma ya afya. Kwenda kwenye maboma ya wafugaji ambako kulibainika mifugo iliyokufa na taarifa ya kuaminika imedhihirisha kwamba ndio chanzo cha watu kuharisha na kutapika , kutoa maelekezo kwa uongozi kwamba ni marufuku watu kula nyama za mifugo ambayo haijakaguliwa na wataalamu wa mifugo na wataalamu wa afya , pia kusimamia na kuhakikisha mizoga yote inazikwa ili kuzuia kuendelea kuchafua mazingira na kuhatarisha afya za watu .
Katika hatua nyingine Nyalubeli amesema kwamba wafugaji wanatakiwa kuzika mifugo yao inapokufa kwani wanapoiacha bila kuizika ni hatari sana, hususani wakati huu wa mvua ambapo mizoga ya mifugo hiyo inasombwa na maji na kupelekwa katika vyanzo vya maji, ikizingatiwa hasa kwamba vyanzo vingi vya maji viko katika miteremko, mizoga hiyo isipozikwa ugonjwa huo unaweza kuwapata watu wengi zaidi ambao ni watumiaji wa maji katika vyanzo ambavyo mizoga hiyo itakuwa imeingia .Akizungumzia mikakati waliyonayo katika kuhakikisha kwamba mifugo hiyo inazikwa Nyalubeli anasema ‘‘tumekubaliana na mkurugenzi kwamba watendaji wa vijiji wasimamie katika maeneo yao mifugo inayokufa izikwe ,isiliwe, na barua inayoelekeza hivyo imeshasambazwa kwa watendaji wote wa vijiji , pia nimezungumza na afisa mifugo wa wilaya ambaye kwa wakati huu yuko kwenye upigaji chapa ngombe, tumekubaliana kwamba maafisa mifugo wote waambiwe ,ili wanapokwenda kupiga chapa, au kufanya kazi yoyote ile kulingana na majukumu yao huko kwenye maboma ,wakikutana na mifugo iliyokufa,wasimamie mifugo hiyo izikwe , na jana tumepeleka matangazo mnadani, kwa sababu pale kuna watu wengi,tumepeleka matangazo ili taarifa iwafikie watu wengi.
Kwa upande wake Daktari wa Mifugo Wilaya ya Kiteto Daktari Lunonu Sigala amesema kuwa ni kweli kwamba kuna ugonjwa wa mifugo , ugonjwa huo unasababishwa na kupe, kitaalamu unaitwa Ndigana baridi au Anaplasmosis na umeshaua mifugo mingi sana ,na sababu kubwa ni kwamba wafugaji hawaogeshi mifugo. Akitoa uthibitisho wa kitaalamu kuhusu kuwepo kwa ugonjwa huo wa mifugo wilayani Kiteto Dkt. Sigala anasema ‘‘ kama Wilaya tumefanya vipimo vyetu ,tumechukua damu kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara na tumethibitisha kwamba ugonjwa ni huo , na dalili zote asilimia mia moja zinaonyesha hivyo.Kwa hiyo mimi niwatoe hofu wafugaji ,maana wapo watu wanafikiri kwamba ni Kimeta, sio Kimeta, ni ugonjwa wa kupe unaojulikana kama Ndigana baridi kwa Kiswahili. Kwa hiyo ushauri tunaoutoa kwa wananchi ni kwamba kama mfugo umekufa wananchi wasile ule mzoga ,wafukie.Na ndio unasikia kuna matukio ya binadamu kuugua na wengine wamefariki kwa sababu ya kula nyama za mifugo ambayo imeugua ugonjwa huo, kwa sababu mfugo unapo kuwa unaugua anakuwa kwenye tiba, na wafugaji wetu,anachukua dawa hii,akiona hajapona anachukua dawa hii, akiona hajapona anarudi tena kwenye ile dawa ya kwanza anaongeza dozi, kwa kudhani kwamba ile dozi ya mwanzo ilikuwa ndogo, ndio sasa mfugo ukija kufa unakuta ile nyama yote inamabaki ya dawa,kwa hiyo ile ndio inayokuja kusababisha shida sana kwa binadamu. Na hasa ukifuatilia sana waliokufa wote ni wale waliokula maini ya mifugo iliyokufa. Kama tunavyojua kwamba maini ndio kiwanda cha sumu, sumu yote ikishaingia mwilini moja kwa moja inaenda kwenye maini .Kwa hiyo wale walikula kiwango kikubwa sana cha sumu ,na ndio waliugua na hatimaye wengine kupoteza maisha’’
Dkt. Sigala amesema kwamba wafugaji hawaogeshi mifugo pamoja na kwamba wanapewa elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kuogesha mifugo.Akifafanua kuhusu sababu ya wafugaji kutoogesha mifugo yao Dkt. Sigala anasema ‘‘ Tunatoa sana elimu juu ya umuhimu wa kuogesha mifugo, na kila kijiji tumeunda kamati ya majosho,lakini sijui hasa ni nini kinatokea , labda wakati mvua kuna uhaba wa maji kwa baadhi ya vijiji, lakini hata vijiji vyenye mabwawa na pampu walikuwa hawaogeshi mifugo yao. Sasa sijui kama ni sababu za kiuchumi au ni sababu za kijamii kwamba wanahofu na menejimenti ambazo zipo za hayo majosho, lakini hata kwa ngazi ya boma, wanashindwa kuwa na pampu za kuogeshea? Kwa sababu baadhi yao wana pampu za mkono ambazo wanatumia kuogeshea.Kwa hiyo mimi naona bado uzembe ni wa wafugaji. kwa sababu elimu wanayo,na ukirudi kwenye kumbukumbu za miaka miwili nyuma asilimia 75 ya mifugo ya hapa wilayani ilikuwa inaogeshwa, na asilimia tisini ya majosho yalikuwa yanafanya kazi. Lakini sasa hivi kwa kumbukumbu zangu ni kwamba hakuna hata josho moja linalofanya kazi .Sasa hatuwezi kuwa na tatizo linalofanana kwa vijiji vyote’’.
Akizungumza kuhusu usimamizi wa majosho na ufuatiliaji uogeshaji mifugo Dkt. Sigala anasema ‘‘ pamoja na kuwa na kamati za majosho katika vijiji , tuna afisa majosho wa wilaya ambaye kazi yake kubwa ni kusimamia hayo majosho, na kuna mwaka kupitia shirika la SNV tulifanya utafiti kwamba ni kwa nini tabia ya uogeshaji ng’ombe inaenda ikishuka , kijiji kimoja wapo kati ya vijiji tulivyovifanyia utafiti sababu kubwa ilikuwa ni kwamba kamati nzima ya usimamizi wa josho ilitokea ikawa ni familia moja.Kwa hiyo wafugaji wakawa wanaona kwamba kuna jinsi ambayo fedha zao zinaliwa na hivyo kuacha kuogesha mifugo yao. Kwa hiyo inawezekana suala la usimamizi wa pesa ni sababu, kwani kila mahali hali imekuwa hivyo. Nadhani hawana uhakika kwamba fedha wanazolipia kuogesha zinakuwa salama, au zinaliwa, ama zinatumika kweli kufanya shughuli ya kununua dawa tena na kuogeshea . Labda sasa tuone kama serikali tunaweza kuingilia kati hii hali, kwamba sasa turudi kama ilivyokuwa miaka ya sabini kurudi nyuma ambapo majosho yote yalikuwa chini ya serikali.Lakini hata hivyo uendeshaji wake utakuwa mgumu sana kwa kuwa dawa zote sasa hivi ziko kwenye sekta binafsi’’ .
Aidha Dkt. Sigara amesema kwamba tiba ya kwanza kwa mnyama anapougua ni chakula, akipata chakula cha kutosha ndipo tiba nyingine pia zinaweza kumsaidia kwa haraka. Lakini kutokana na ukame wa miezi michache iliyopita mifugo imekosa chakula na hivyo imekuwa na udhaifu ,ambapo inapotokea inakumbwa na ugonjwa ,inaongezewa na mzigo wa dawa kali, hali hiyo husababisha mifugo hiyo kufa ,kwa sababu ugonjwa unakuta tayari miili ya mifugo hiyo imedhoofika sana. Katika hili Dkt Sigala amewashauri wafugaji kuwa na maeneo ya malisho, ambayo watakuwa wanapanda nyasi, na hatimaye kuweza kuyatumia maeneo hayo kulisha mifugo yao wakati wa ukame. Dkt. Sigala amesema kwamba wanaendelea kutoa elimu hiyo ya upandaji nyasi za kulishia mifugo ,na tayari wameshaleta mbegu,na baadhi ya wafugaji wameshaanza kuja kuchukua mbegu hizo na kwenda kupanda.Vilevile amesema kwamba wale wafugaji wenye mifugo mingi ni vema wakajenga majosho yao wenyewe na wakajiwekea utaratibu mzuri wakuogesha mifugo yao, kwani wapo wafugaji ambao kwa idadi ya mifugo waliyonayo wana uwezo wa kujenga majosho yao .Sambamba na hayo Dkt. Sigala amewataka wafugaji kuacha imani potofu kwamba wakati wa kiangazi hakuna kupe, hivyo kuona kwamba hawana sababu ya kuogesha mifugo wala kuipatia kinga katika kipindi hicho, jambo ambalo ndio kiini hasa cha mashambulizi ya ugonjwa wa kupe unaoua mifugo wakati huu .
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa