Mkuu wa mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti akizungumza na watumishi wa serikali,wenyeviti wa vijiji na Wahe. madiwani katika kikao chake kilichofanyika ndani ya ukumbi wa kituo cha jamii ( Community Center) Kibaya - Kiteto
Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti Katika Kikao cha Mhe. Mkuu wa Mkoa na Watumishi wa Serikali,Wenyeviti wa Vijiji Pamoja na Wahe. Madiwani .
Watumishi wa Serikali,Wenyeviti wa Vijiji pamoja na Wahe. Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti ndani ya Ukumbi wa Kituo cha Jamii ( Community Center) Kibaya - Kiteto.
......... HABARI KAMILI...........
WATUMISHI WA SERIKALI KATAENI KUTUMIWA NA WANASIASA- RC MNYETI.
Mkuu wa mkoa wa Manyara mheshimiwa Alexander Mnyeti amewataka watumishi kukataa kutumiwa na wanasiasa kukwamisha shughuli za serikali na kuchochea migogoro.Mheshimiwa Mnyeti ameyasema hayo katika kikao chake na watumishi wa serikali,wenyeviti wa vijiji pamoja na waheshimiwa madiwani kilichofanyika ndani ya ukumbi wa Kituo cha jamii (Community Center ) kilichopo katika mji mdogo wa Kibaya wilayani Kiteto.
Akizungumza katika kikao hicho mheshimiwa Mnyeti amesema kwamba kuna wanasiasa ambao wanaikwamisha serikali kufanya shughuli zake , na wamekuwa wakiwatumia watumishi wa serikali katika kufanya hivyo kwa kuwatishia kuwafukuza kazi pale wanapokuwa hawakubaliani na matakwa yao . Aidha Mheshimiwa Mnyeti amesema kwamba watumishi wachape kazi , wafanye kazi kulingana na taaluma zao, wawe na misimamo katika yale wanayoamini kwamba ni sahihi , wasimame katika kutenda haki ,wasiyumbishwe wala kutikiswa na wanasiasa .Akisisitiza kuhusu kuwa na msimamo katika kufanya kazi, mheshimiwa Mnyeti anasema ‘‘ Watendaji wa vijiji,watendaji kata, wakuu wa idara ,kataeni kwa nguvu moja msiwe sehemu ya kutumika ,msitumiwe na wanasiasa kwa sababu zao binafsi,na kwa faida zao binafsi.Nitasikitika sana kuona mambo hayaendi ,eti kwa sababu kuna mwanasiasa anazuia. Kila mtu atimize wajibu wake. Mtendaji wa kata utakaekuja kuniambia kwamba umesimamishwa kazi kwa sababu umekataa maelekezo ya mbunge nitakuelewa na nitakutafutia cheo kingine’’.
Vilevile mheshimiwa Mnyeti amezungumzia suala la nidhamu kwa watumishi wa serikali ambapo amesema kwamba watumishi wengi wamesahau wajibu wao, wanajua muda wanaotakiwa kufika kazini na muda wa kutoka kazini, lakini wanaingia kazini kwa muda wanaotaka, na wanatoka kwa muda wanaotaka .Akisisitiza kuhusu kuwawajibisha watumishi wasiofuata maadili ya utumishi, mheshimiwa Mnyeti anasema ‘‘Tuna staili nyingi za kumfukuza mtu kazi ,na wala hatutishii, tukiona hii staili ya madiwani imeshindikana tuna staili nyingine.Ama tutakuwa tunawahamishia maeneo mengine ambayo wako tayari kuwajibisha watumishi wao’’. Kadhalika amewataka watumishi kuacha siasa maofisini , badala yake wafanye kazi zao.
Katika kikao hicho pia Mheshimiwa Mnyeti amezungumzia mambo mbalimbali ikiwemo makusanyo ya kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wilaya ya Kiteto ambapo amesema kwamba mapato yako chini ,hivyo amemuagiza Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto ndugu Tamim Kambona kwa kushirikiana na afisa biashara kumpa meneja wa TRA Wilaya ya Kiteto orodha ya wafanyabiashara wote ili aweze kuchambua wafanya biashara wanaopaswa kulipa kodi TRA , baada ya uchambuzi huo watendaji wa kata na vijiji wamsaidie kumuonyesha maeneo waliko wafanyabiashara hao.Kadhalika mkuu wa wilaya mheshimiwa Tumaini Magessa ambaye ndiye mshauri wa kodi wa wilaya ameagizwa kuitisha mikutano ya mara kwa mara ili kuhakikisha kwamba maelekezo aliyoyatoa mkuu wa mkoa yanafanyiwa kazi , lengo likiwa ni kuongeza mapato .Pia amezungumzia kuhusu viongozi na watumishi kufanya biashara na halmashauri ambapo amesisitiza kwamba hairuhusiwi kisheria, na ni marufuku kufanya hivyo.
Katika hatua nyingine mheshimiwa Mnyeti amezungumzia kuhusu ukataji miti, katika hilo ametoa utaratibu wa kukata miti ambapo ni mti mmoja kwa miti kumi , kwamba mtu haruhusiwi kukata mti hata mmoja isipokuwa amepanda miti kumi na imeshika vizuri ardhini .Pia ameelekeza utaratibu wa kufuata ili kupata kibali cha kukata miti baada ya kupanda miti hiyo kulingana na idadi ya miti mtu anayotaka kukata . Pia amezungumzia matumizi bora ya ardhi ambapo amemtaka mkuu wa wilaya kusimamia matumizi ya ardhi kulingana na sheria na taratibu ambazo zilikwisha kubalika. Sambamba na hayo, mheshimiwa Mnyeti amezungumzia suala la chakula cha mchana mashuleni ,ambapo ametoa agizo kwamba wanafunzi wapate chakula cha mchana , na wanaokwamisha utaratibu huo wachukuliwe hatua.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa