Watendaji wa Kata katika Halmashauri ya Wilaya Kiteto wameagizwa kuwashirikisha wazazi wa wanafunzi juu ya mavuno ya mazao yanayopatikana katika mashamba ya shule.
Hayo yamesemwa Januari 16, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mh Remidius Mwema Emmanuel, katika kikao cha tathmini ya mkataba wa lishe ngazi ya kata na vijiji robo ya pili ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Idadi ya shule zinazotoa chakula shuleni na idadi ya wanafunzi wanaokula angalau mlo mmoja shuleni, ni mojawapo ya viashiria vya utekelezaji wa mkataba huo wa lishe. Ili kuweza kutekeleza viashiria hivyo kwa 100%, ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kiteto ilitoa agizo kwamba katika msimu wa kilimo wa mwaka 2023/2024 kila shule wilayani hapo ilime angalu hekari tano za mahindi ili kuwapunguzia wazazi gharama ya kuchangia chakula shuleni.
Mh. Mwema alisema kwamba inawezekana mavuno yasitosheleze chakula kwa wanafunzi kwa mwaka mzima hivyo ni busara baada ya mavuno watendaji kufanya hesabu ya kujua mavuno hayo yatatosheleza chakula kwa muda gani na kisha kutoa taarifa hiyo kwa wazazi ili wazazi wafahamu kiasi gani kimepatikana na kiasi gani watapaswa kuchanga.
Aidha aliwapongeza watendaji ambao wamefamya vizuri katika kutekeleza mkatabata huo wa lishe kwenye kata zao. Kwa upande wa kata ambazo zilitekeleza chini ya lengo, Mh. Mwema amewaagiza watendaji wa kata hizo kuwashirikisha viongozi wa dini, mila na chama katika maeneo yao ili wawasaidie kuwahamasisha wananchi.
Nae Mkurugenzi Mtendaji (W), CPA. Hawa Abdual Hassan, aliwasisitiza watendaji hao kuendelea kusimamia vizuri suala la lishe shuleni kwani jambo hilo ni muhimu kwaajili ya wanafunzi na pia wilaya inapimwa kwenye utekelezaji wa mkataba huo wa lishe.
Kikao cha tathimini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe ngazi ya kata na vijiji kinafanyika kila robo ya mwaka kwa lengo la kujadili taarifa na viashiria vya lishe vilivyopo kwenye mkataba ambavyo vinatekelezwa kwenye ngazi ya kata na vijiji.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa