Mbunge wa Kiteto Mhe. Emmanuel Papian akizungumza na wakazi wa kijiji cha Ngabolo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini Ngabolo mwishoni mwa wiki.
Mtendaji wa Kijiji cha Ngabolo akitambulisha uongozi wa serikali ya Kijiji chake katika Mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini Ngabolo mwishoni mwa wiki.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngabolo akifungua Mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho mwishoni mwa wiki.
Wakazi wa kijiji cha Ngabolo wakiwa wamekusanyika kumsikiliza Mbunge wao Mhe. Emanuel Papian katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijijini Ngabolo mwishoni mwa wiki.
Wakazi wa kijiji cha Ngabolo wakimuuliza maswali Mbunge wao Mhe. Emanuel Papian katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini Ngabolo mwishoni mwa wiki.
Mbunge wa Kiteto Mhe. Emmanuel Papia pamoja na ujumbe wake kutoka wilayani wakikagua madarasa yaliyojengwa kwa ajili ya shule ya msingi katika Kijiji cha Ngabolo ambayo ujenzi wake unaendelea . Madarasa hayo manne yamejengwa kwa nguvu za wananchi , na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Ndg Tamim Kambona ametoa mabati ambayo ndiyo yaliyopaulia madarasa hayo .
Msingi huu ni wa jengo la madarasa matatu ambayo yanajengwa kwa nguvu za wananchi ili kukamilisha madarasa saba kwa ajili ya shule ya msingi katika Kijiji cha Ngabolo .
Mbunge wa Kiteto Mhe. Emmanuel Papia pamoja na ujumbe wake kutoka wilayani wakikagua ujenzi wa nyumba ya mwalimu kwa ajili ya shule ya msingi katika Kijiji cha Ngabolo ambayo ujenzi wake unaendelea .
......HABARI KAMILI.......
Ziara ya Mbunge wa Kiteto Mhe. Emmanuel Papian imeleta matumaini mapya kwa wanakijiji wa Ngabolo,ambapo Mbunge huyo amewahakikishia kukamilika kwa usajili wa shule ya msingi na uletwaji wa walimu katika shule hiyo ambayo wameijenga kwa nguvu zao, sambamba na kutengeneza mashine iliyokuwa ikitumika kupandisha maji katika kijiji hicho,ambayo imeharibika.Mhe Papian ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini Ngabolo mwishoni mwa wiki.
Akizungumza katika mkutano huo Mheshimiwa Papian amesema” Nimeona mmejenga madarasa manne, na mengine matatu yako kwenye msingi, nimeona na tofali ambazo mmefyatua kwa ajili ya kupandisha yale madarasa matatu ambayo yako kwenye msingi. Diwani wenu amenihakikishia kwamba madarasa yale matatu ambayo yako kwenye msingi yatakamilika ndani ya muda mfupi.Suala hili naondoka nalo,nitalifuatilia kwa nguvu zangu zote mpaka shule ifunguliwe.Tumekubaliana, na mwenyekiti wa chama ,tumekubaliana na katibu, tumekubaliana na diwani wenu hapa ,tunakwenda kukutana na wahusika tujadiliane, tupange, tukubaliane, shule isajiliwe , ifunguliwe, Januari watoto waanze kusoma hapa . Hatutaki siasa tena,tunataka hii ifunguliwe.watoto wetu wasomee hapa, walioko Ndedo wasogee hapa, tupunguze msongamano kwenye shule ya Ndedo.
Kadhalika Mhe. Papian amezungumzia kuhusu maji,ambapo maji imekuwa ni tatizo kubwa sana kwa wakazi wa Ngabolo, hususani baada ya bwawa la kijiji hicho kupasuka na mashine ya maji kuharibika. Hapa Mhe Papian amesema “ Nimeuliza hapa kuhusu mashine ya maji,nimeambiwa mashine inasumbua.Ni lazima tupate mpango mahususi, ambao unaoeleweka,kuhakikisha kwamba huduma ya maji ya uhakika inapatikana hapa Ngabolo.Nitazungumza na mzabuni ambaye yupo tujue ni nini ambacho kinatakiwa kifanyike ili mashine iendelee kuzalisha maji kwa ajili ya binadamu na mifugo”
Aidha Mhe. Papian Amewapongeza wakazi wa Ngabolo kwa jitihada zao za kudumisha amani katika kijiji chao. Vilevile amekemea suala la uchungiaji mifugo kwenye mashamba ambapo amesema kwamba suala hilo linawatia umaskini wakulima ,hivyo wanaofanya vitendo hivyo waache mara moja ili kutokusababisha uvunjifu wa amani .
Mhe. Papian ametembelea kijiji cha Ngabolo,ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku saba katika vijiji mbalimbali vya jimbo lake kukagua shughuli za maendeleo sambamba na kuzungumza na wakazi wa vijiji husika. Akiwa katika kijiji cha Ngabolo Mhe. Papian amekagua ujenzi wa madarasa kwa ajili ya uanzishaji shule ya Msingi katika kijiji hicho ambacho kwa sasa watoto wanalazimika kwenda shule katika kijiji cha Ndedo ambacho kiko umbali mrefu kutoka kijijiNgabolo. Pia amekagua bwawa ambalo la kijiji hicho ambalo limepasuka baada ya mvua nyingi zilizonyesha mwaka huu .
.............MWISHO...........
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa