Mawaziri 7 pamoja na kamati ya ulinzi na usalama wakiwa kwenye ziara katika kijiji cha Kimotoroki wilayani Simanyiro. Lengo la ziara hiyo ni kukusanya taarifa kuhusu mgogoro kati ya kijiji cha Kimotoroki -wilaya ya Simanjiro na hifadhi ya Tarangire, na mgogoro kati ya kijiji cha Irikiushibor - wilaya ya Kiteto na Pori tengefu la Mkungunero.
Mawaziri wakisalimiana na kamati ya ulinzi na usalama ,mara baada ya kuwasili kijiji Simanjiro.
Mwenyekiti wa jopo hila mawaziri nane wanaotekeleza agizlo la Mhe. Rais la kukusanya taarifa kwa ajili ya kurasimisha vijiji na vitongoji vilivyoko katika maeneo ya hifadhi Mhe. William Lukuvi akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kimotoroki wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara.
Wananchi wakiwa wamekusanyika katika mkutano kuwasikiliza mawaziri pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti.
.....MWANZO WA MAKALA.........
Kwa muda mrefu hapa nchini Tanzania kumekuwepo na migogoro mingi inayotokana na baadhi ya vijiji na vitongoji kuwepo katika maeneo yanayodaiwa kuwa ni hifadhi.Migogoro hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa imesababisha wanachi wanaoishi katika maeneo hayo kuondolewa kwa nguvu, nyumba na mali zao kuchomwa moto, na wakati mwingine mifugo kukamatwa,mifugo kutaifishwa baada ya kesi, ambapo baadhi ya wananchi wanaoishi katika vijiji hivyo amekuwa wakishitakiwa kwa madai ya kuweka makazi ama kufanya shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya hifadhi na mapori tengefu, hali hiyo ikamsukuma Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. John P.J Magufuli Kutoa agizo la kusitishwa mara moja kwa zoezi la kuviondoa vijiji na vitongoji vinavyodaiwa kuwepo katika maeneo ya hifadhi.
Rais alitoa agizo hilo tarehe 15/01/2019 ikulu Dar es Salaam katika mkutano wake na Waziri wa maliasili na utalii,Daktari Hamisi Kigwangwala,Katibu mkuu kiongozi balozi John Kijazi ,Naibu waziri wa mifugo na uvuvi Abdalah Ulenga,Katibu mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga,na katibu Mkuu wa wizara ya ardhi Dorothy Mwanyika.
Sambamba na agizo, hilo Mhe Rais aliwataka mawaziri wote wa wizara husika kukutana ili kubainisha na kuanza mchakato wa kurasimisha maeneo ya vijiji na vitongoji hivyo.
Katika kutekeleza agizo hilo la Mhe Rais Mawaziri 8 wa wizara hizo husika ambao ni Mhe. Hamis Kigwangwala - waziri wa maliasili na utalii,Mhe. Wiliam Lukuvi - waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi,Mhe. Profesa Makame Mbarawa –waziri wa maji na umwagiliaji,Mhe. Luhaga Mpina - waziri wa mifugo na uvuvi,Mhe. Selemani Jaffo – Waziri wa Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Hussein Mwinyi – Waziri wa Ulinzi, Mhe. Omari Tebweta –Naibu Waziri,wizara ya Kilimo,chakula na ushirika na Mhe. Musa Sima – Naibu waziri, ofisi ya Rais Muungano na Mazingira wamekuwa katika ziara kutembelea vijiji vyenye migogoro kuwasikiliza wananchi ,pamoja na kuona hali ilivyo ili waweze kuandika taarifa na kumshauri Mhe. Rais kuhusu namna bora ya kumaliza migogoro hiyo.
Kiteto na Simanjiro ni wilaya ambazo ziko katika mkoa wa Manyara.Wakazi wake kwa asilimia 90 ni Wamasai ambao shughuli yao kuu ya kiuchumi ni ufugaji.Wilaya hizi ni miongoni mwa wilaya nyingi Tanzania ambazo vijiji vyake vimekuwa na migogoro ya mara kwa mara na hifadhi za taifa pamoja na mapori tengefu. Chanzo cha migogoro hiyo kwa wilaya ya Simanjiro na Kiteto ni mipaka kati ya pori la Tengefu la Mkungunero lililopo wilaya ya Kondoa na kijiji cha Irikiushibor wilaya ya Kiteto na Hifadhi ya Tarangire na Kijiji cha Kimotoroki wilaya ya Simanjiro.
Uongozi wa wilaya Kiteto ,Simanjiro na mkoa wa Manyara kwa ujumla wake umefanya jitihada mbalimbali ili kutatua migogoro hiyo,ili wananchi wa vijiji hivyo waishi na kufanya shughuli zao kwa amani.Moja wapo ya jitihada hizo ni kufuatilia kwa karibu kiini cha migogoro hiyo,kufanya vikao vya mara kwa mara na viongozi wa pori tengefu la Mkungunero na hifadhi ya taifa ya Tarangire .
Pamoja na jitihada hizo imekuwa vigumu sana kumaliza migogoro hiyo , kwani wananchi wanaona kwamba wanahaki ya kuwepo katika maeneo hayo, hali ya kuwa kwa upande wa uongozi wa Mkungunero na Tarangire hawataki uwepo wa wananchi wala shughuli yoyote ya kibinadamu katika maeneo hayo yanayodaiwa kuwa ni hifadhi.
Kutokana na migogoro hiyo ambayo utatuzi wake bado umebaki katika sintofahamu, jopo hilo la mawaziri husika waliopewa jukumu la kushughulikia mogogoro hiyo likiongozwa na mwenyekiti wake Mhe. William Lukuvi lilifika Mkoani Manyara wilaya ya Kiteto na Simanjiro kwa ajili ya kuona hali ilivyo na kuwasikiliza wananchi,ambapo wananchi walipewa nafasi ya kuzungumza wanayoyafahamu kususiana na migogoro hiyo,vile vile iliwapa nafasi ya kuzungumza viongozi wa hifadhi ya Tarangire,na pori tengefu la Mkungunero.
Baada ya kusikiliza pande zote, Mhe. Lukuvi alikuwa na haya ya kusema “Mara zote tumekuwa tukipata taarifa kutoka kwa uongozi wa mkoa na wilaya pamoja na taasisi za hifadhi kuhusiana na hii migogoro,lakini leo sisi tumekuja kuwasikiliza,mimi na wenzangu tunashukuru kwamba tumefika, tumezungumza nanyi.Sisi hatukuja kutoa uamuzi ,tumekuja kwa lengo la kuendelea kutekeleza agizo la Mhe. Rais. Tumeagizwa tufuatilie hizi taarifa zote,halafu tumshauri ,na safari hii sio kumshauri tu,lakini twende na waraka wa baraza la mawaziri, Mhe. Rais afanye maamuzi ya mwisho.Ili Rais atakaekuja baadae akute kuna uamuzi uliokwishafanyika.Ili mambo haya yasiwe tu kwa huruka ya mapenzi ya mtu bali yawe ya kisheria’’.
Aidha Mhe. Lukuvi alizitaka taasisi hizo zinazosimamia hifadhi kutowabugudhi wananchi mpaka pale uamuzi kuhusiana na migogoro hiyo utakapotoka.Mhe. Lukuvi amewaasa viongozi wa hifadhi hizo kutokufanya jambo lolote litakalowasumbua wananchi, kwani kwa kufanya hivyo wanamkasirisha Mhe Rais, kwa sababu hapendi kuona wala kusikia wananchi wanateseka.Kadhalika amewataka wananchi wanaoishi katika vijiji na vitongoji hivyo kuacha kuingia kwenye maeneo ya hifadhi kwa makusudi,badala yake pale mahali walipokuwa wakati Mhe. Rais anatoa agizo, wakae hapohapo wasiendelee kujitanua kwa kuingia hifadhini, wala kwenye pori la Mkungunero mpaka pale tangazo rasmi kuhusu uamuzi uliofikiwa litakapotoka.
Mhe Lukuvi pia amesema kwamba na wao ni wanasiasa hivyo wanamtazamo tofauti na watumishi wa serikali,kwani wao wanawaangalia wananchi kama wapiga kura wao.Kwa hiyo wananchi wawaamini kuwa baada ya kujionea hali halisi na kusikia kwa masikio yao kutoka kwa pande zote, wataandika taarifa nzuri kuhusu migogoro hiyo,taarifa ambayo wanaamini kwamba itamsaidia Mhe Rais katika kutoa uamuzi ambao utakuwa muafaka.
Mkuu wa mkoa wa manyara Mhe. Alexander Mnyeti kama alivyo Mhe Rais anapenda kuona kwamba wananchi wa mkoa wake wanaishi kwa amani ,na hawasumbuliwi, hilo linaonekana wazi katika kauli yake hii “Sisi Wanamanyara tunapenda wanyama pori,lakini pia pamoja na kuwepo kwa wanyama pori, maisha ya wananchi wanaoishi katika maeneo haya yanayodaiwa kuwa hifadhi,yanatakiwa yaendelee, wananchi wasisumbuliwe,wasinyanyaswe kwani wamekuwepo katika maeneo haya kwa miaka mingi,na wanyama pia wamekuwepo kwa miaka mingi,ni lazima haki ya wananchi ya kuishi na kufanya shughuli zao za kiuchumi ilindwe kwa kuweka utaratibu mzuri ambao utawafanya wanyama pori waendelee kuishi na wananchi pia waendelee kuishi kwenye maeneo yao”.
Naye waziri wa mifugo na uvuvi Mhe. Luhaga Mpina akiwa na nia hiyo hiyo ya kutaka wananchi waishi na kufanya shughuli zao vizuri ,amewahakikishia wafuguaji kuwa wizara yake itashughulikia changamoto zote zinazowakabili.Hapa Mhe. Mpina anasema “ Sisi tuko sawasawa,na changamoto za wafugaji zimefika mwisho.Tutaondoa changamoto moja baada ya nyingine,mpaka tuhakikishe kwamba wafugaji katika nchi hii wanaishi kwa haki usalama na kwa amani.Hatutashindwa’’.
Katika hatua nyingine mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papian ameshauri kuhusiana na namna bora ya kutatua mgogoro kati ya kijiji cha Irikiushibor na pori tengefu la Mkungunero ambapo amesema kwamba chanzo cha mgogoro huo ni mpaka kati ya Dodoma na Manyara ,na kwamba ili mgogoro huo uishe eneo lenye mgogoro ambalo ni takribani hekta 22,000 lirudishwe kwenye hifadhi ya jamii ya 'Wildlife Management Area' (WMA),hifadhi ambayo inaundwa na vijiji vya Makame,Ndedo,Katikati,Ngabolo na Irikiushbor ili iwe mali ya wananchi.Na kwamba eneo hilo likirudi kwa wananchi mgogoro utaisha,wanyama wataendelea kuwepo na wananchi wataendelea kuishi kwa usalama na amani.
Kadhalika mbunge wa jimbo la Simanjiro Mhe. James Ole Millya amewashukuru mawaziri kwa kufika mkoani Manyara,sambamba na shukrani hizo Millya amesema kwamba kwa mara ya kwanza jopo la mawaziri 7 limefika manyara,anaamini kwamba kufika kwa jopo hilo na kujionea hali halisi pamoja na kuwasikiliza wananchi ni hatua nzuri ya kuelekea kumaliza migogoro hiyo.Mhe Millya pia amesema kwamba wataalam (wahifadhi)ndio walioifikisha migogoro hiyo mahali ilipo kwa sababu ya kutokuwa na huruma kabisa na kutokuyachukulia mambo kwa uzito wake,kwani kutokana na ongezeko la idadi ya watu, kwa utashi wao tu wangeona sababu ya kusogeza mipaka ya hifadhi,jambo ambalo lingemaliza migogoro .Badala yake wamekuwa wakiwaondoa watu na kusogeza mipaka yao kwa kumega maeneo ambayo wananchi wanaishi.
Mhe.Millya ameendelea kusema kwamba wanachokifanya wataalam hao sio haki,wanapaswa kuwa na huruma.Wanapaswa pia kutambua kwamba jamii za kifugaji ambazo ndizo zinazoishi katika maeneo hayo ni wahifadhi .Kwa hiyo wanatakiwa wabadilishe historia kwa kukaa pamoja kama watu wanaoshirikiana katika kuhifadhi wanyama pori .Wakubaliane kwamba maeneo gani yawe mipaka, baada ya makubaliano waweke mikataba ya kudumu,kuliko kutumia nguvu kubwa kuwaondoa wananchi,ambapo wanapotumia nguvu hizo wanawaumiza.
Ziara hiyo ya mawaziri 7 mkoani manyara, imeleta matumaini mapya kwa jamii za kifugaji ambazo kwa asilimia kubwa ndizo zinazoathirika kutokana na migogoro hiyo.Ni dhahiri kwamba wananchi wanaoishi katika vijiji hivyo vyenye migogoro wanaiona kesho yao mpya, kesho ambayo wataishi bila ya kuwa na wasiwasi wa kufukuzwa , mifugo yao kukamatwa na nyumba zao kuchomwa moto.Matumaini hayo yanathibitishwa na wananchi waliohojiwa mara baada ya mkutano, ambapo walisema kwamba wanaamini kuwa migogoro hiyo mwisho wake umefika, kwa sababu kufika kwa mawaziri wengi namna hiyo katika vijiji vyao, ni dhahiri kuwa serikali imeona kwamba kuna tatizo kubwa na imejipanga vilivyo kulishughulikia.
.......MWISHO.......
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa