Ikiwa ufaulu wa somo la Hisabati kwa watahiniwa wote nchini umeshuka na kupelekea 51% ya watahiniwa wote kupata daraja D, upande wa Shule ya Msingi Laalakir Wilayani Kiteto, wanafunzi 31 kati ya 45, ambao ni sawa na 69%, wamepata ufaulu wa daraja A katika somo hilo, 13 wamepata daraja B na mwanafunzi mmoja amepata ufaulu wa daraja C.
Mkurugenzi Mtendaji (W) Kiteto, CPA Hawa Abdul Hassan, pamoja na wakuu wa Idara na Vitengo, Novemba 27, 2023 wametembelea shule hiyo na kuwapongeza walimu kwa kazi nzuri waliyoifanya ambayo imeleta matokeo ya ufaulu huo mzuri ambao wanafunzi wote wamepata daraja A.
Akiongea wakati akimkaribisha Mkurugenzi Mtendaji (W) na timu ya wataalam aliyongozana nayo shuleni hapo, Afisa Elimu wa Wilaya Awali na Msingi Papakinyi Kaai, alisema kwamba, katika tathmini ya ufaulishaji katika Mkoa wa Manyara, Shule ya Msingi Laalakir imeshika nafasi ya pili kwa ufaulishaji kati ya shule za msingi 652 mkoani hapo zilizofanya Mtihani wa Taifa wa kuhitimu elimu ya Msingi 2023 huku nafasi ya kwanza ikishikwa na shule ya binafsi kutoka Wilayani Simanjiro.
Mkurugenzi Mtendaji amesema kwamba ameona ni vyema yeye pamoja na wataalam kutoka ofisini kwake kwenda shuleni hapo kuwapongeza na kuwatia moyo walimu hao kwa kazi nzuri waliyoifanya. “Tunatambua juhudi zenu katika kuwafundisha wanafunzi, juhudi hizo ndizo zilizopelekea shule hii kupata ufaulu mzuri, tunawaomba muendelee na moyo huo huo ili mpate kufanya vizuri zaidi” aliongeza Mkurugenzi Mtendaji (W) Ndugu Hawa Abdul Hassan.
Akiongea kwa niaba ya walimu wenzake, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Ndugu Emmanuel Sanka, alisema kwamba wamefarijika na ujio wa Mkurugenzi na ujumbe alioongozana nao. Mbali na hayo, Ndugu Sanka alisema kwamba shule yake imepata wastani wa 275 na kupata Daraja A bora na aliahidi kwamba mwakani watafanya vizuri zaidi.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa