Wilaya ya Kiteto imeanza rasmi maandalizi ya utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote kufuatia kikao maalum cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) ngazi ya Wilaya kilichofanyika Januari 06, 2026 Mjini Kibaya, kikilenga kutoa elimu ya awali na kujenga uelewa kwa wadau kuhusu mpango huo wa kitaifa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto na Mwenyekiti wa Kamati ya PHC, Mhe. Remidius Mwema, alisema kikao hicho ni mwanzo wa mchakato wa kuandaa jamii kabla ya kuanza kwa vikao maalum vya Tarafa zote saba kuanzia Januari 08, 2026, vitakavyofuatwa na mikutano ya wananchi katika ngazi ya vijiji.

Mhe. Mwema alisisitiza kuwa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya siku 100, wenye lengo la kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya bila vikwazo na kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kiteto, Ndg. Mufandii Msaghaa, alisema mpango huo ni dhamira ya dhati ya Serikali ya kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, huku akiahidi kuwa viongozi wa Wilaya watahakikisha wananchi wanapata elimu sahihi na ya kina.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Mhe. Athumani Kilimo, alibainisha kuwa uhamasishaji na uelewa wa wananchi ni nguzo muhimu ya mafanikio ya mpango huo, na kuwataka wajumbe wa Kamati hiyo wanafikisha elimu hiyo kwa wananchi kwa kuzingatia makundi na mazingira ya jamii husika.

Kikao hicho kilihusisha pia viongozi wa dini, vyama vya siasa, viongozi wa kimila pamoja na makundi maalum, hatua inayodhihirisha mshikamano wa kijamii na kisiasa katika kuhakikisha Bima ya Afya kwa Wote inakuwa agenda ya kila mwananchi Kiteto.

Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa