Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Januari 27, 2026, limepitisha bajeti ya Shilingi bilioni 41.9 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, hatua inayolenga kuimarisha utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa wilaya hapa.

Akizungumza wakati wa kikao cha Baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Mhe. Athumani Hamisi Kilimo, alisema kuwa halmashauri inatarajia kukusanya, kupokea na kutumia jumla ya Shilingi 41,907,909,000, ambapo Shilingi 5,148,249,000 ni mapato ya ndani ya halmashauri.
Mhe. Kilimo alieleza kuwa halmashauri imetenga asilimia 40 ya mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa mwelekeo wa bajeti hiyo unalenga kuongeza ustawi wa jamii na kuimarisha miundombinu katika sekta mbalimbali.
“Halmashauri imetenga asilimia 40 ya mapato ya ndani, ambapo fedha hizo zitaelekezwa katika utoaji wa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya kilimo, mifugo na maeneo mengine muhimu yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, ikiwemo sekta za elimu na afya,” aliongeza Mhe. Kilimo.
Katika hatua nyingine, Baraza hilo pia lilipitisha mipango na bajeti za taasisi nyingine za serikali zinazotoa huduma ndani ya Wilaya ya Kiteto, zikiwemo Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), pamoja na Mamlaka ya Maji Mji wa Kibaya (KIUWASA).
Upitishwaji wa mipango na bajeti hizo ni ishara ya dhamira ya uongozi wa Wilaya ya Kiteto katika kusukuma mbele maendeleo, kuimarisha uwajibikaji wa kisiasa na kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kuboresha huduma za kijamii na kukuza fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Kwa upande wao, Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto wameeleza imani yao kuwa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 itatekelezwa ipasavyo ili kukidhi mahitaji ya wananchi na kuboresha utoaji wa huduma bora.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa