Katika kuhakikisha mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia kwa watoto wa shule za msingi nchini, Serikali kupitia Programu ya BOOST imetoa kiasi cha shilingi milioni 88.6 kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika Shule ya Msingi Wezamtima iliyopo kata ya Bwawani, wilayani Kiteto.
Akizungumza wakati wa kikao cha utambulisho wa mradi huo kwa serikali ya kijiji kilichofanyika katika shule hiyo Julai 22, 2025, Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi wilayani hapa, Mwl. Elizabeth Mlaponi alisema kuwa fedha hizo zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na matundu sita ya vyoo.
"Shule hii ilikuwa na uhitaji mkubwa wa miundombinu. Mradi huu utaleta mabadiliko makubwa katika mazingira ya kujifunzia na kufundishia," alieleza Mwl. Mlaponi.
Viongozi hao wa kijiji waliipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuona umuhimu wa kuboresha shule hiyo, wakisema kuwa hatua hiyo imeonesha namna serikali inavyowajali wananchi wake, hususan katika sekta ya elimu.
Mradi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa mara moja ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira salama na rafiki kwa ajili ya masomo yao.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa