Katibu Tawala wa Wilaya ya Kiteto Ndugu. Mufandii Msaghaa amewasihi wananchi kujenga tabia ya kuwekeza katika mifuko na maeneo mbalimbali ya kifedha ili kujiwekea akiba na maandalizi ya maisha ya baadaye.
Ameyasema hayo Septemba 10, 2025 wakati akifunga Semina iliyojikita kutoa Utaratibu wa Uwekezaji katika Dhamana za Serikali iliyoendeshwa wilayani Kiteto na Maafisa kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
“Uwekezaji ni njia salama na yenye manufaa kwa wananchi wote wakiwemo wafanyabiashara, watumishi na hata wastaafu kwani hutoa dira ya hapo baadae”. alisema Msaghaa
Semina hiyo ilihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo watumishi, wastaafu na wafanyabiashara.
Katika Semina hiyo, washiriki walipata elimu ya kina juu ya utaratibu wa uwekezaji katika dhamana za serikali, aina za dhamana za serikali, jinsi ya kushiriki kwenye manunuzi ya dhamana hizo, pamoja na faida zinazotokana na uwekezaji huo. Sambamba na hayo washiriki walifundishwa namna uwekezaji kupitia dhamana za serikali unavyoweza kumsaidia mtu mmoja mmoja kujiandaa kwa ajili ya maisha ya baadaye na kwa serikali kuongeza mapato ya ndani na kuweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Maafisa wa BOT waliondesha semina hiyo walitokea ofisi ya BOT Kanda ya Kaskazini – Arusha, wakiongozwa na Ndugu.Simon Kessy ambaye ni Meneja Msaidizi wa Idara ya Fedha na Utawala.
Hata hivyo Ndugu. Msaghaa aliwaomba maafisa hao kujipanga na kurudi tena Kiteto kutoa elimu zaidi ya uwekezaji, akibainisha kuwa wananchi wengi bado wanahitaji maarifa ya kifedha ili kuimarisha ustawi wao kiuchumi.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa