Mwenyekiti wa Kikao cha DCC Mhe. Tumaini Magessa akiendesha kikao cha DCC kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto.
Mwenyekiti wa Kikao cha DCC Mhe. Tumaini Magessa (wa kwanza kushoto) ,Katibu wa kikao Ndg .Tamim Kambona (wa pili kutoka kushoto),katibu tawala (W) Kiteto Ndg. Stephano Ndaki(wa pili kulia) na katibu wa CCM (W) Kiteto Ndg. Shekue Pashua ( wa kwanza kulia) wakifuatilia kwa makini mwenendo wa kikao cha DCC kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto
Katibu wa Kikao cha DCC Ndg. Tamim Kambona akifunga kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto
Mwenyekiti wa Halmashauri (W) Kiteto Mhe. Lairumbe Mollel (wa kwanza kulia) ,Mwenyekiti wa CCM (W) Kiteto Ndg. Mohamed Kiondo ( wa katikati) na Makamu mwenyekiti wa halmashauri (W) Kiteto Mhe. Hassan Benzi ( wa kwanza kushoto) wakiwa kwenye kikao cha DCC kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto
Meneja wa TRA Wilaya ya Kiteto Akiwasilisha taarifa ya taasisi yake wakati wa kikao cha DCC kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri .
Meneja wa TFS Wilaya ya Kiteto Akiwasilisha taarifa ya taasisi yake wakati wa kikao cha DCC kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri .
Meneja wa TANESCO Wilaya ya Kiteto Akiwasilisha taarifa ya taasisi yake wakati wa kikao cha DCC kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri .
Wajumbe wa DCC wakiwa kwenye kikao cha DCC kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto.
Wajumbe wa DCC wakishauri kuhusiana na masuala mbalimbali ya maendeleo ya wilaya ya kiteto wakati wa kikao cha DCC kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri .
..................HABARI KAMILI..........................
DC Magessa Awataka Madiwani Kuwa Mfano Katika Uanzishaji wa Viwanda Wilayani Kiteto.
Mkuu wa wilaya ya Kiteto mheshimiwa Tumaini Magessa amewataka waheshimiwa madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto kuwa viongozi wa mfano kwa kutekeleza kauli mbiu ya Mhe Rais Magufuli ya Tanzania ya viwanda,kwa kuanzisha viwanda.Mheshimiwa Magessa ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha Kamati ya ushauri ya wilaya (DCC) kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto.
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Magessa amesema kwamba wilaya ya Kiteto inatakiwa kuanzisha viwanda vipya 15 ,lakini hadi sasa viwanda ambavyo vimekwisha kuanzishwa ni viwanda viwili tu . Mhe. Magessa amesema kwamba kuwa kiongozi ni kuonyesha mfano ,hivyo Wahe. Madiwani wanapaswa kuwa wa kwanza kuanzisha viwanda.Akisisitiza kuhusu kauli yake hiyo Mhe.Magessa anasema ‘‘Nilitegemea kusikia madiwani wameanza kukusanya fedha za kuanzisha viwanda.Sasa sisikii, sijui labda inabidi DC ndio nianzishe .Sijasikia diwani hata mmoja anasema mimi pale kwangu naanzisha cha kusaga mahindi.Naona kimya tu’’.Aidha Mhe. Magessa amewataka wajumbe wa DCC kama washauri katika masuala mbalimbali wilayani kuwahamasisha wananchi kuanzisha viwanda vidogo vidogo kwani anavyoiona wilaya ya Kiteto anaamini kwamba upo uwezekano wa kuwa na viwanda zaidi ya 20.
Kikao hicho cha DCC kilikuwa na agenda 11 ikiwemo taarifa ya mwenendo wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2017/2018.Mpango wa bajeti wa halmashauri kwa mwaka 2018/2019,ambapo bajeti iliwasilishwa ,wajumbe walitoa ushauri katika baadhi ya vipengele vya bajeti hiyo na hatimaye kuiridhia bajeti hiyo.
Ukusanyaji mapato na ulipaji kodi TRA ni ajenda nyingine muhimu ya kikao hicho, mwenyekiti aliwataka wajumbe wote kutoa ushauri utakaowezesha kuongezeka kwa ukusanywaji mapato ya halmashauri na kodi inayolipwa TRA.Wajumbe walibainisha vyanzo vingine vya mapato na kushauri ufuatiliaji ufanyike ili serikali kuu na halmashauri iweze kupata mapato kupitia vyanzo hivyo.
Migogoro ya ardhi iliyopo wilayani Kiteto na hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na uongozi wa wilaya , ni ajenda njingine ya kikao hicho ambapo mwenyekiti wa kikao aliwaeleza wajumbe wakikao hicho kuhusu mikakati mbalimbali ambayo uongozi wa wilaya umeiweka ili kumaliza migogoro wilayani Kiteto , vilevile wajumbe wa kikao walizungumzia kuhusiana na migogoro hiyo na kushauri juu ya nini kifanyike katika kutokomeza migogoro hiyo.
Agenda nyingine ni utunzaji wa mazingira na marufuku ya ukataji miti na uvunaji ovyo wa mazao ya misitu. Akiwasilisha ajenda hiyo Katibu Tawala wa wilaya ya Kiteto ndugu Stephano Ndaki amesema kwamba mipango ya matumizi bora ya ardhi ipo,hakuna mwananchi asiyejua kwamba katika kijiji chake eneo la malisho ni lipi,eneo la makazi ni lipi na eneo la kilimo ni lipi.Hivyo ni vema wananchi wakazingatia mipango ya matumizi bora ya ardhi iliyopo.Na iwapo kuna haja ya kufanya mapitio ili kufanya marekebisho katika mipango hiyo ,mapitio yatafanywa baada ya wao kuzingatia mipango iliyopo.Na kwamba kuheshimu matumizi bora ya ardhi yaliyopangwa ndio njia pekee ya kumaliza migogoro.
Katika hatua nyingine ndugu Ndaki amegongelea msumari agizo la RC wa Manyara la kuwekwa kwa adhabu kali kwa wafugaji watakaochungia katika mashamba ya wakulima,ambapo wafugaji hao watalazimika kulipa fidia itakayokuwa imetokana na tathmini ya uharibifu wa mazao .Pamoja na kulipa fidia ya uharibifu wa mazao, adhabu ya faini itatozwa kwa kila ng’ombe aliyeingia kwenye shamba na kufanya uharibifu huo.Kadhalika kwa wakulima watakao vamia na kulima maeneo ambayo sio kwa ajili ya matumizi ya mashamba watapewa adhabu ya kuotesha miti kulingana na idadi ya miti waliyokata katika mashamba hayo baada ya afisa misitu kufanya tathmini ya miti iliyokatwa.Pia ndugu Ndaki amepiga marufuku uanzishwaji wa vitongoji visivyo rasmi ,ambapo amesema kwamba vitongoji hivyo vinaanzishwa bila utaratibu, vinaanzishwa katika maeneo ambayo sio ya makazi , jambo ambalo linasababisha uharibifu wa mazingira na kuchochea migogoro ya ardhi.
Kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya hufanyika kila baada ya miezi mitatu .Dhima ya kikao hicho ni kushauri katika masuala mbalimbali yanayohusu wilaya ikiwemo upatikanaji wa mapato na matumizi ya halmashauri .
.........................MWISHO.................................
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa