Mgeni rasmi ,ambaye pia ni mkuu wa wilaya Mhe. Tumaini Magessa akihutubia wafanyakazi katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani wilayani Kiteto . Maadhimisho hayo yamefanyika ndani ya uwanja wa halmashauri uliopo karibu na kituo kikuu cha mabasi - Kibaya .
Wafayakazi kutoka taasisi mbalimbali wilayani Kiteto wakiandamana kusheherekea maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ( Mei Mosi) .
Mgeni rasmi ambaye ni mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akipokea maandamano ya wafanyakazi katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ( Mei Mosi) .
Wafayakazi kutoka taasisi mbalimbali wilayani Kiteto pamoja na meza kuu wakiimba wimbo wa mshikamano katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ( Mei Mosi) .
Wafayakazi wakimsikilza mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa wakati akihutubia katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ( Mei Mosi) .
Mwl. Rehema Sudi akisoma risala ya wafanyakazi kwa mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ( Mei Mosi) . Aliyesimama pembeni yake ni Mama Lymo, mtumishi katika ofisi ya DC.
...................HABARI KAMILI....................
Mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ( Meimosi) wilayani Kiteto ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Kiteto, mheshimiwa Tumaini Magessa amewataka watumishi kujiwekea akiba ili waweze kujiendeleza kimaisha kabla ya kustaafu.Mhe. Magessa ameyasema hayo wakati akiwatubia wafanyakazi wa taasisi mbalimbali wilayani Kiteto katika maadhimisho hayo , ambapo kiwilaya yamefanyika katika uwanja wa halmashauri, uliopo jirani na kituo kikuu cha mabasi Kibaya .
Akizungumza na wafanyakazi wakati wa hotoba yake Mhe. Magessa amesema wafanyakazi waweke akiba wakati wakiwa kazini , kwani kutokuweka akiba , na kuwa na mawazo ya kutegemea pesa ya kiinua mgongo kuna madhara.Akisisitiza juu ya umuhimu wa wafanyakazi kuweka akiba Mhe. Magessa amesema “Tunategemea muweke akiba sasa, ukianza kuweka akiba sasa,kama una miaka 30 , baada ya miaka 20,utakuwa na miaka 50, akiba hiyo itakusaidia, utaweza kujenga kibanda chako.Lakini ukisema unasubiri kiinua mgongo ndipo ujenge nyumba, utakufa mwaka unaofuata, kwa sababu utakapojenga nyumba pesa yote itakwisha halafu baadae itakuwaje? Na wewe ulizoea kunywa chai asubuhi, kula chakula mchana na jioni. Sasa kwenye uzee utabadilisha maisha, utakuwa unakunywa chai,unakula mara moja usiku. Maana yake nini? Umekiita kifo mwenyewe. Pesa yote umeweka kwenye nyumba, na kifo kina kufuata sasa”.
Aidha Mhe Magessa amesema kwamba wafanyakazi waweke akiba katika umri walionao, kwani maandalizi ya kustaafu yanapaswa kuanzia katika maisha waliyonayo sasa.Ili wakati wa uzee usiwe ni wakati wa kujenga au kupanga kufanya miradi. Kwani kwa kufanya hivyo maisha ya uzee yatakuwa magumu sana, hali ya kuwa wametumia muda wao mwingi katika utumishi, wataona kama vile kiinua mgongo hakikuwasaidia chochote kutokana na kutokuweka mipango mapema ya namna ya kuishi baada ya kustaafu.
Maadhimisho hayo ya siku ya wafanyakazi duniani ( Meimosi) yalianza kwa maandamano ya wafanyakazi ambayo yalianzia katika ofisi za halmashauri ya wilaya ya Kiteto ( Bomani) na kupokelewa na mgeni rasmi ( Mhe. Tumaini Magessa) uwanjani.Kadhalika Sherehe hizo zilipambwa na burudani mbalimbali kama muziki, mashairi na tenzi pamoja na michezo kama vile sarakasi ,mashindano ya kukimbiza kuku ,mashindano ya kukimbia ndani ya magunia,kuvuta kamba na kukuna nazi.
.....................MWISHO......................
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa