Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akitoa maelekezo kuhusu uvunaji wa mazao ya misitu katika kikao cha baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya ya kiteto
............HABARI KAMILI............
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mheshimiwa Tumaini Magessa amewataka wakazi wa wilaya hiyo pamoja na wageni wote wanaoingia wilayani humo kwa lengo la uvunaji wa mazao ya misitu kufuata utaratibu katika uvunaji huo ili kuwezesha utunzaji mazingira endelevu .Mhe. Magessa ameyasema hayo wakati akizungumza katika baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Kiteto mwishoni mwa mwezi juni 2018.
Akielekeza kuhusu utaratibu wa uvunaji mazao ya misitu Mhe. Magessa amesema” mtu yeyote atavuna mazao ya misitu baada ya kupata kibali na leseni kutoka kwa kamati ya uvunaji.Kamati ya uvunaji iko wazi kupokea maombi ya uvunaji .Baada ya kupokea maombi ,kamati itakaa, baada ya kikao tutaidhinisha nani wamepewa vibali vya uvunaji, na afisa misitu wa wilaya anazo leseni za kuwapatia watu hao”.
Mhe. Magessa amesema kwamba waraka wa mkuu wa mkoa wa Manyara unaelekeza kwamba ili mtu aweze kuvuna mti mmoja anatakiwa awe amepanda miti kumi na imeota,lakini vijiji havionyeshi mahali pa kupanda miti ,isipokuwa vinaonyesha mahali pa kuvuna tu.
Aidha Mhe. Magessa amesema kwamba wananchi wana haki ya kuvuna mazao ya misitu, lakini wanatakiwa kufuata utaratibu na mwongozo wa serikali. Akisisitiza kuhusu kauli yake hiyo Mhe. Magessa amesema” Kuna watu wanatembea na bendera huko mitaani wanasema tumezuia uvunaji wa mkaa,hatujazuia uvunaji,tunataka watu wafuate utaratibu”.
Mhe. Magessa pia ameeleza kuhusu madhara ya kutokuwa na utunzaji wa mazingira endelevu, Mhe. Magessa amesema“Tusipoheshimu mazingira leo,tukaanza kuweka mikakati ya kuyafanya mazingira yetu yaendelee kuwa endelevu, tutaadhibiwa kesho.Watu walime,watu wafuge, lakini mazingira yetu yaendelee kuwa salama.Tukifika hapo tunaweza kufanikiwa bila wasi wasi”.
Wilaya ya Kiteto imekuwa katika tishio la kuwa jangwa baada ya uvunaji miti holela ambao umekuwa ukifanywa na watu kwa malengo mbalimbali.Hata hivyo mwanzoni mwa mwaka huu 2018 Mkuu wa mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti alitoa waraka unaoelekeza utaratibu utakaotumika katika uvunaji wa mazao ya misitu.
............MWISHO..............
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa