Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akitoa maelekezo ya serikali ,katika siku ya pili ya kikao cha baraza la madiwani Oktoba 31,2018, ndani ya ukumbi wa halmashauri .Waliokaa pembeni yake , upande wake wa kulia ni Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papian, na upande wake wa kushoto ni Makamu mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Hassan Benzi.
.......... HABARI KAMILI.......
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mheshimiwa Tumaini Magessa amewataka Waheshimiwa madiwani kuonyesha uwajibikaji kwa wananchi wao kwa kutembelea maeneo yao kukagua shughuli za maendeleo, kuhimiza maendeleo na kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi.Mheshimiwa Magessa ameyasema hayo Oktoba 31,2018 ,wakati akitoa maelekezo ya serikali katika kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Kiteto, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri .
Akizungumza wakati akitoa maelekezo hayo Mheshimiwa Magessa amesema ‘‘Madiwani wengi hamuendi kwenye maeneo yenu, madiwani mnatakiwa kwenda kwenye kata zenu ili muweze kufuatilia maendeleo ya wananchi , kama hamfanyi hivyo , uwajibikaji wenu unakuwa haupo, kwa sababu ninyi ni madiwani wa wananchi,maana yake mnatakiwa kujua matatizo ya wananchi,mnatakiwa kujua maendeleo ya wananchi , tembeleeni maeneo yenu , zungumzeni na wananchi, kafanyeni kazi ya kutatua matatizo ya wananchi”.
Mheshimiwa Magessa amesema kwamba wananchi wakiwaona madiwani wao mara kwa mara ,wanakuwa na uhakika kwamba mambo yatakwenda vizuri. Wasipofanya hivyo, wananchi wataondoa imani kwao na watawakataa. Akisisitiza kuhusu hilo Mheshimiwa Magessa amesema “ Isifike wakati wa uchaguzi ukasema kwamba DC ndiye ameliondoa jina langu, mimi huwa natembea sana, kwa hiyo kama diwani hafiki kwenye eneo lake, mimi najua kwamba hafiki, maana wananchi wananiambia huyu bwana hafiki, ndio leo umekuja nae.Tufike tuhimize elimu, tuzungumze na kukemea kuhusu tatizo la mimba za utotoni”.
Aidha mheshimiwa Magessa amewataka waheshimiwa madiwani kuwa na mienendo mizuri,ili kwamba wanapokemea vitendo viovu wao wawe wasafi. Amesema kwamba ili mtu aweze kuhimiza jamii kutenda matendo mema, ni lazima yeye mwenyewe mwema .Asiwaambie watu fuateni maneno yangu,msifuate matendo yangu,ni lazima huyo mtu awe na matendo mema, ili wale anaowaelekeza kutenda mema waige mfano kutoka kwake. Hivyo wao kama madiwani wasiwe kama sehemu ya kuweka miiba katika maeneo yao. Ili wawe viongozi wazuri lazima maneno yao yaendane na matendo yao.
Katika hatua nyingine mheshimiwa Magessa amewataka waheshimiwa madiwani kuhimiza kuhusu suala la elimu, kwamba asiwepo mtoto asiyekwenda shule kwa kisingizio chochote, wafuatilie kuhusu ufundishaji , kiwango cha ufaulu kiendelee kuongezeka.Kuwahimiza wazazi kuchangia chakula shuleni kwa ajili ya wanafunzi kupata chakula cha mchana , waweze kusoma vizuri, lakini pia amesisitiza kwamba waheshimiwa Madiwani wawaelimishe wazazi na walezi kuhusu chakula wanachopeleka shule, kwamba wapeleke chakula chenye ubora kinachofaa kwa matumizi ya binadamu. Kisiwe chakula ambacho kimewekwa dawa za kuua wadudu (viuatilifu) ndani ya muda mfupi ili kuepuka madhara yanayoweza kuwapata wanafunzi kutokana na kula vyakula vibovu ama vyenye kemikali za kuua wadudu.
Kuchangia chakula shuleni ni moja wapo ya mikakati ya wilaya ya Kiteto katika kuinua taaluma na kiwango cha ufaulu kiwilaya. Na kwa kiasi kikubwa wazazi wamehamasika, japo kuna changamoto za hapa na pale ambazo viongozi wa wilaya kwa kushirikiana na madiwani ambao ndio wawakilishi wa wananchi wamekuwa wakizitatua .
.........MWISHO............
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa