.......HABARI KAMILI..........
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa amewataka wakuu wa idara za Halmashauri ya wilaya ya Kiteto zinazohusika na shughuli za lishe kuweka kipaumbele katika suala la lishe, ili kuiepusha jamii na na udumavu. Mhe. Magessa ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha mafunzo ya awali ya mipango na bajeti ya masuala ya lishe ngazi ya Halmashauri kilichofanyika katika ukumbi wa hospitali ya wilaya mwishoni mwa wiki iliyopita.
Akizungumza wakati akifungua kikao hicho Mheshimiwa Magessa amesema“ tatizo la lishe linasababisha udumavu wa mwili na akili,pia linasababisha kuongezeka kwa magonjwa yasioambukiza yanayotokana na ukosefu wa chakula bora pamoja na ulaji mbaya usiozingatia misingi ya afya bora.Katika tatizo la lishe duni,hali ni mbaya zaidi kwa watoto ,kina mama wajawazito na wanaonyonyesha.Watoto wadogo ndio waathirika zaidi wa matatizo yanayotokana na lishe duni’’.
Mhe . Magessa amesema kwamba suala la lishe,linatakiwa kupewa kipaumbele na watu wote,kwa sababu suala hilo bado ni tatizo katika jami,jamii bado inauelewa mdogo kuhusu mlo kamili.Hali ya kuwa Ustawi wa jamii unategemea hali nzuri ya lishe.Kama lishe ni duni jamii haiwezi kuwa na ustawi mzuri , kwa sababu hata uwezo wa kufikiri wa watu utakuwa mdogo.
Kadhalika Mheshimiwa Magessa ameeleza matarajio yake kwa wakuu hao wa idara baada ya mafunzo hayo ambapo amesema kwamba anatarajia kuwa kikao kazi hicho kitakuwa na tija , lakini ni lazima mipango yote waliyonayo kuhusu masuala ya lishe waiweke kwenye utekelezaji, na wahakikishe kuwa mipango hiyo inaigusa jamii. Amewataka kuweka kumbukumbu na takwimu kwa yale yote wanayotekeleza, kwani kwa kufanya hivyo, itawapa wepesi wa kufahamu ni yapi yametekelezwa, yametekelezwa kwa kiwango gani ,na yapi ambayo hayajatekelezwa.
Pia Mheshimiwa Magessa amesema kwamba vikao hivyo ni muhimu sana katika kujifunza ,kwa kuhudhuria katika vikao hivyo mtu anapata kitu ambacho kina mpa ari ya kutafiti zaidi.Anapokwenda kutafiti anajifunza vitu vingi zaidi.Vilevile Mhe. Magessa amesema kwamba wilaya imeazimia kufanya mapinduzi ya kilimo kwa lengo la kulima kilimo chenye tija kitakachoboresha kipato cha wananchi sambamba na kuboresha lishe,hivyo kikao hicho ni cha muhimu kwa sababu yale yatakayoazimiwa, yatakwenda kufanyiwa kazi.
Aidha Mhe. Magessa amesema kwamba ni muhimu kwa Mwenyekiti wa Halmashauri kuwashirikisha madiwani maazimio yote ya vikao hivyo kwani madiwani ndio kiungo muhumu cha kupeleka taarifa kwa wananchi kwenye kata zao.
Kikao kazi hicho cha siku moja kimehitimishwa kwa majadiliano ambapo kila mkuu wa idara alieleza ni kwa namna gani idara yake inatekeleza shughuli za lishe.
........MWISHO.............
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa