Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mh Remidius Mwema Emmauel, amezindua Bodi ya Huduma ya Afya ya Wilaya ambayo moja ya majukumu yake ni kuhakikisha jamii inapata huduma bora za Afya inazozimudu na zinazoimarisha Afya zao.
Uzinduzi huo mbali na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali, pia ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kiteto Ndugu Abdala Bundala, Makamo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Ndugu Hassan Benzi, Mkurugenzi Mtendaji (W) CPA. Hawa Abdul Hassan pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya, Bi Mufandii Msaghaa, umefanyika Februari 7,2024 katika Ukumbi wa Maktaba ya Wilaya.
Akiongea katika uzinduzi huo, Mgeni Rasmi, Mh Mwema alisema kwamba serikali ina matumaini makubwa kutoka kwenye bodi hiyo na pia bodi hiyo inahesabu ya kutoa baada ya miaka mitatu .
“Kuna changamoto ya muingiliano wa majukumu hivyo ni vyema wajumbe hawa wa bodi wakapewa semina ili wafahamu vizuri majukumu yao” alisema Mh. Mwema.
Aidha Mh Mwema aliwasihi wajumbe hao wa bodi kufanya kazi kwa kushirikiana na kutimiza wajibu wao kwa uadilifu pasipo kutanguliza maslahi yao binafsi.
“Kazi ya Bodi ni kuangalia huduma ya afya inaendaje, ni vyema mkasome muongozo vizuri, tunaamini mtatuvusha. Matarajio yangu bodi hii iwe bodi ya mfano bora katika Mkoa”, aliongeza Mh. Mwema.
Nae Mwenyekiti wa Halmashauri Ndugu Abdala Bundala alisema bodi ina wajibu wa kusimamia utoaji wa huduma za afya wilayani hapo. “ Mnapaswa mjue kua mna jukumu la kufanya kwa kushirikiana na sisi” aliongeza Ndugu Bundala.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bi. Elizabeth Joseph Urio, alisema kwamba wapo tayari kufanya kazi kwa taratibu zilizowekwa na zaidi kwa kujitolea.
Nae Mganga Mkuu wa Wilaya, Dr. Vicent Gyunda ambaye pia ni Katibu wa Bodi hiyo alisema kwamba mipango ya semina imeshawekwa sawa na wajumbe watapewa semina ili kuepuka migongano ya kiutendaji. Aidha aliongeza kwa kusema uwajibikaji na kujituma ndio nguzo ya mafaniko kwa Bodi hiyo.
Jukumu jingine la bodi hiyo yenye wajumbe kumi, ni kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali na mgawanyo wake kwa kuzingatia mahitaji ya ngazi zote za huduma na matumizi bora.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa