Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe Tumaini Magessa (aliyesimama) akizungumza wakati wa kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri 31-01-2019.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Lairumbe Mollel (aliyeshika kipaza sauti) akiongoza kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri.
Kaimu Mkurugezi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Ndg. Emmanuel Mwagala (aliyesimama) akijibu hoja mbalimbali za madiwani wakati wa kikao cha baraza .
Wahe. madiwani wakiwa katika kikao cha baraza .
Wahe. madiwani wakiwasilisha taarifa za maendeleo ya kata zao wakati wa kikao cha baraza la madiwani.
Wahe. madiwani wakichangia hoja mbalimbali wakati wa kikao cha baraza la madiwani.
..........HABARI KAMILI..........
Mkuu wa wilaya ya Kiteto mheshimiwa Tumaini Magessa amewataka waheshimiwa madiwani kusimamia urejeshaji wa mikopo inayotolewa kupitia vyama vya ushirika (SACCOS) vilivyopo kwenye maeneo yao ,ili viweze kukopesheka.Kwani kwa hali ilivyo sasa vyama vingi havikopesheki kwa sababu wanachama wake hawarejeshi mikopo.Mhe Magessa ameyasema hayo tarehe 31 Januari 2019 kwenye kikao cha baraza la madiwani kililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri.
Akizungumza wakati akitoa maelekezo ya serikali ,Mhe. Magessa amesema “Kazi kubwa madiwani mliyonayo,ni kusimamia maendeleo ya kata zenu, SACCOS ziliziko huko kwenye maeneo yenu, ni sehemu ya maendeleo ya kata zenu, hakikisheni kwamba mnasimamia watu wanalipa madeni.Kwenye mikutano yenu mlizungumzie hili la kutorejesha mikopo, na mpange mikakati itakayosaidia katika urejeshaji wa mikopo”.
Mhe Magessa ameeleza sababu kuu ya watu kushindwa kurejesha mikopo, amesema kwamba watu wengi huwa wanakimbilia kuchukua mikopo bila kuelewa kiwango cha riba,wala masharti ya urejeshaji wa mikopo hiyo.Na kwamba ili kuondoa tatizo hilo, watu wakitaka kuchukua mikopo kabla hawajafanya hivyo wamuone afisa ushirika na mwanasheria wa Halmashauri ili waelimishwe kuhusu utaratibu wote wa kukopa, riba na masharti mengine yote .Kwani kwa kufanya hivyo itawasaidia kuepuka kuchukua mikopo bila kuelewa vizuri kiwango cha riba inayotozwa,na masharti ya urejeshaji jambo ambalo limesababisha watu wengi kuingia kwenye madeni ambayo wanashindwa kuyalipa na hatimaye kusababisha migogoro , sambamba na kuua vyama vya ushirika.
Aidha Mheshimiwa Magessa amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika kutosimamia vizuri mali za vyama.Na kuzitumia kinyume na taratibu.Katika hili mh. Magessa ameahidi kufuatilia kuhakikisha kwamba nyumba ya MECCO SACCOSS - Matui ambayo iliwekwa rehani kwa shilingi 3,000,000 ,umiliki wake unarudi kwenye chama.
Mhe. Magessa pia amezungumzia kuhusu madini,Ambapo amewataka waheshimiwa madiwani, wakuu wa taasisi za serikali pamoja na wananchi kwa ujumla kutoa taarifa,pale ambapo wameona au kusikia kwamba kuna mahali madini yanachimbwa,ili mhandisi mkazi wa mkoa aje ayatambue hayo maeneo,utaratibu wa serikali ufuatwe.
Amesema kwamba hakuna uchimbaji wa madini unaoruhusiwa bila leseni, hivyo utoaji wa taarifa ni muhimu ili wataalamu waje waeleze nini kinatakiwa kifanyike.Ameongeza kwamba ni muhimu utaratibu ufuatwe, ili watu wafanye kazi kwa utaratibu,badala ya kufanya kazi kiholela kama ambavyo wanafanya sasa,ambapo wamekuwa wakichimba mashimo kila mahali, bila hata ya kuweka vizuizi,jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha ya watu wanaoishi karibu na maeneo hayo, hususani watoto wadogo.
Katika hatua nyingine Mhe. Magessa amezungumza kuhusu tamko la Mhe. Rais ,amesema kwamba wananchi wengi wamelielewa vibaya tamko la Rais ,alichozungumzia Rais ni kwamba kama kulikuwa na hoja yoyote ya kuwafukuza wananchi kwenye vijiji na vitongoji ambavyo vilikwisha kuwepo kwenye maeneo ya hifadhi, hiyo hoja isitishwe kwanza,wizara husika zikutane kubainisha na kurasimisha maeneo hayo, tamko hilo halimaanishi kwamba watu wavuruge mipango ya matumizi bora ya ardhi ambayo yalishawekwa kwenye vijiji kwa gharama kubwa au wavamie tu maeneo ya hifadhi na kufanya shughuli za kibinadamu.
Kikao hicho cha siku mbili, kimejadili ajenda mbalimbali, ajenda kuu zikiwa ni kupokea taarifa za kata kwa robo ya pili ya mwaka, kupokea majibu ya hoja za vyama vya siasa,ambapo majibu ya hoja hizo hutolewa na ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri na kupokea taarifa za kiutumishi ambazo hutolewa na afisa utumishi wilaya.
.........MWISHO..........
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa