Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mh. Remidius Mwema Emmanuel, amewahimiza wachimbaji wadogo katika eneo la machimbo ya dhahabu la Ilndorkon pamoja na muwekezaji wa eneo hilo kufuata kanuni za usalama katika shughuli zao.
Mh. Mwema ameyasema hayo Mei 6,2024 alipotembelea machimbo hayo ili kujionea shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo hilo pamoja na kuongea na muwekezaji AutoGerm Mining LTD (AGM LTD) pamoja na wachimbaji wadogo wa eneo hilo.
Akiongea mara baada ya kukagua eneo ambalo uchimbaji unafanyika, Mh. Mwema amesema kwamba amejionea baadhi ya maduara (mashimoi) ya machimbo hayajazingatia kanuni ya umbali kutoka shimo moja hadi jingine.
“Kuna mashimo yapo wazi hii ni hatari kwa usalama. Pia umbali kati ya shimo na shimo inapaswa kua ni mita 15 hii ni kwaajili ya usalama wa wachimbaji ila nimeona kuna baadhi ya mashimo hayajafuata utaratibu huu” alisema Mh. Mwema.
Kuhusiana na mashimo ambayo yapo wazi na ambayo yapo karibu karibu, Mh. Mwema amemuagiza Msimamizi wa Mgodi huo Ndg Majura Yohana kuhakikisha kua wanasimamia taratibu zote za kiusalama mgodini hapo ili kuhakikisha wachimbaji wanafanya kazi katika mazingira salama.
Akijibu hoja ya mashimo yaliyo wazi, msimamizi huyo amesema kwamba wameweka utaratibu mpya wa kuhakikisha kila siku asubuhi wanatumia muda wa saa moja (1) kufukia mashimo. Utaratibu huo umepangwa kuanza Mei 7,2024. Na kwa upande wa mashimo ambayo hayajafuata utaratibu wa umbali kutoka shimo hadi shimo, iliazimiwa mashimo hayo yafungwe miti (matimba).
Aidha Mh.Mwema amesema kwamba ni lazma wachimbaji waliopo eneo hilo kuweka utaratibu maalumu wa kumfahamu kila mmoja aliyepo eneo hilo. Vilevile aliwasisitiza wachimbaji hao kuzingatia maadili na matumizi bora ya fedha wanazozipata na kuwaasa kutozisahau familia zao walizoziacha mbali.
Upande wa afya na mazingira, Mh. Mwema aliagiza kuongezwa kwa matundu ya vyoo katika eneo hilo ili kukidhi mahitaji kwani matundu yaliyopo ni machache kuliko idadi ya watu.
“Mazingira ya usafi hayaridhishi, watu wote wanaouza chakula waweke eneo maalumu la kukusanyia taka. Wote mnapaswa kuzingatia kanunii za afya ili kujikinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko” aliongeza Mh. Mwema.
Machimbo ya Ilndorokon yalianza rasmi April 15,2024 na mpaka sasa eneo hilo lina watu wapatao 320.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa