Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Makame (WMA Makame), iliyopo Wilaya ya Kiteto, imeandika historia mpya katika sekta ya uhifadhi nchini baada ya kunyakua Tuzo ya Serengeti, tuzo inayotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa taasisi na wadau waliotoa mchango mkubwa katika kulinda rasilimali za wanyamapori, misitu na mazingira kwa ujumla.
Tuzo hiyo ilitolewa Januari 31, 2026, katika Hoteli ya Mount Meru, jijini Arusha, kwenye hafla maalum iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii. Mgeni Rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba.
Tuzo hiyo ilipokelewa na Katibu wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Makame, Ndg. Supuk Olekao, kwa niaba ya jumuiya hiyo huku tukio hilo likishuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto,Mhe.Remidius Mwema Emmanuel.

Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Makame iliibuka mshindi kati ya jumuiya sita (6) za hifadhi za wanyamapori zilizoshindanishwa katika kipengele hicho, huku Tanzania ikiwa na jumla ya jumuiya arobaini (40) za hifadhi za wanyamapori, hali inayoonesha ushindani mkubwa na thamani ya ushindi uliopatikana.
Sababu kuu iliyoifanya jumuiya hiyo kutwaa tuzo hiyo ni utekelezaji wake wa mfumo bora wa uhifadhi shirikishi, unaowashirikisha wananchi kikamilifu katika maamuzi ya uhifadhi na usimamizi wa rasilimali za asili. Kupitia mfumo huo, wananchi wameweza kutambua kuwa uhifadhi si kikwazo cha maendeleo bali ni fursa ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Aidha, Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Makame imetajwa kuwa mfano bora wa matumizi ya mfumo wa kisasa wa usimamizi wa taarifa, unaorahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wakati, kwa uwazi, na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi. Mfumo huo umeongeza ufanisi katika ulinzi wa rasilimali za asili na kuimarisha uwajibikaji kwa wadau wote.
Sifa nyingine iliyoipa jumuiya hiyo ushindi ni namna manufaa yatokanayo na shughuli za uhifadhi yanavyorejeshwa kwa jamii, kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Kupitia mkabala huo, wananchi wamekuwa tayari kutenga ardhi yao kwa ajili ya uhifadhi bila migogoro, jambo lililochangia mafanikio endelevu ya jumuiya hiyo.

Wataalamu wa uhifadhi wameielezea Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Makame kama eneo salama na la mfano wa kuigwa, hasa katika usimamizi wa uhifadhi unaoongozwa na jamii, utekelezaji wa sera ya uhifadhi shirikishi, na katika kuleta matokeo chanya yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Kupatikana kwa tuzo hiyo kunatarajiwa kuongeza hamasa kwa wadau wa maendeleo na sekta ya utalii kushirikiana na jumuiya hiyo, pamoja na kufungua fursa mpya za uwekezaji katika utalii wa ikolojia na utalii wa kitamaduni, ikiwemo utalii wa vyakula vya asili na mila za jamii zinazozunguka hifadhi hiyo.

Kwa ujumla, Tuzo ya Serengeti kwa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Makame imeonesha dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuthamini na kuhamasisha juhudi za wadau wanaolinda rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho, huku jumuiya hiyo ikiendelea kuwa kielelezo cha uhifadhi endelevu unaomshirikisha mwananchi.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa