Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mhe. Remidius Mwema, ametoa wito kwa halmashauri ndani ya Kanda ya Kaskazini kuhakikisha kuwa yale yanayooneshwa katika mabanda yao kwenye maonesho ya Nanenane yanatekelezwa kwa vitendo na wakulima pamo na wafugaji katika maeneo yao.
Hayo ameyaongea Agosti 6,2025 akiwa kwenye ziara ya kutembelea baadhi ya mabanda akiwa Mgeni Rasmi wa siku.
Mhe. Mwema amesema kwamba haina maana endapo teknolojia na njia za kisasa za uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo ziwe zinaishia kwenye maonesho bali maafisa ugani wanajukumu la kuhakikisha kila mkulima na mfugaji ndani ya wilaya anazalisha kwa kutumia mbinu kama wanazozionesha au kuzifundisha kwenye maonesho ya Nanenane.
" Kinachooneshwa hapa ina maana ni taswira ya wilaya nzima, mtu anapokuja kwenye banda lako na kuona mazao bora ya kilimo au mifugo anajenga picha kwamba wakulima wote au wafugaji wote ndani ya wilaya husika wanazalisha kama unavyotuonesha kwenye maonesho haya" alisema Mhe. Mwema.
Akiwa katika ziara ya kutembelea mabanda mbalimbali, Mhe. Mwema alitoa maoni na mapendekezo kadhaa yenye lengo la kuboresha sekta ya kilimo na mifugo nchini. Katika banda la NMB, aliitaka benki hiyo kuongeza juhudi katika kutoa elimu zaidi kwa wananchi kuhusu huduma zao hususani kuweka wazi vigezo na masharti, hasa yale yanayohusiana na bima ya kilimo.
Katika banda la Mamlaka ya Uthibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Mkuu huyo wa wilaya aliishauri mamlaka hiyo kutumia maadhimisho ya siku ya mbolea kama jukwaa la kuwatunza na kuwatambua maafisa ugani wanaofanya kazi nzuri katika halmashauri zao. Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza morali kwa maafisa ugani na hivyo kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wakulima.
Vilevile, Mkuu huyo alipata nafasi ya kutembelea mabanda mawili ya ASAS Group ambapo akiwa banda lan AfriFarm alitoa rai kwa kampuni hiyo kuwafikia wakulima wengi zaidi katika maeneo ya vijijini ili kuhakikisha teknolojia na mbinu bora za ufugaji zinawafikia walengwa. Aidha akiwa kwenye banda la maziwa la ASAS, alitoa pongezi kwa kampuni hiyo kwa kuwa kiwanda cha kwanza nchini kuzalisha maziwa ya unga, na kusifu hatua yao ya kutoa mikopo kwa wakulima na wafugaji wanaoishi karibu na kiwanda chao, akisema kuwa ni mfano bora wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na wananchi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mwema alieleza kufurahishwa na ushiriki wa wanafunzi kwenye maonesho hayo, akisema kuwa ni jambo muhimu katika kuwaandaa vijana kuelewa kuwa kilimo sio adhabu, bali ni shughuli ya heshima na yenye manufaa makubwa kwa taifa.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa