Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Ndg. Tamim Kambona akizungumza wakati wa kikao cha baraza la Madiwani la halmashauri ya wilaya ya kiteto kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri, Oktoba 31,2018.
..... HABARI KAMILI.......
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto ndugu Tamim Kambona amewataka watendaji wote wilayani hapa kuhakikisha kwamba ujenzi wa madarasa unafanyika kwa ajili ya kidato cha kwanza mwaka 2019. Ndugu Kambona ametoa maelekezo hayo oktoba 31 ,2018 katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri .
Akizungumza wakati wa kikao hicho ndugu Kambona amesema “ Tunajua kwamba mwezi wa kwanza tutakuwa na mlundikano wa wanafunzi, asilimia 69.5 ya wanafunzi waliofaulu ni kubwa sana, kwa hiyo lazima kutahitajika vyumba vya madarasa, na madawati. Waheshimiwa madiwani wote,maafisa tarafa, watendaji wa kata na watendaji wa vijiji wote pamoja na waratibu elimu kata tushirikiane kwenye hili, ili tuhakikishe wanafunzi wetu wote waliofaulu wanapata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza kama ilivyokuwa kwa mwaka huu 2018.
Ndugu Kambona ameomba ushirikiano wa watu wote katika kuhakikisha kwamba wanafunzi wote waliofaulu wanaripoti katika shule walizopangiwa kwa wakati na wanaendelea na masomo yao.
Kadhalika ndugu Kambona amezungumzia suala la utoro wa wanafunzi mashuleni ambapo amewataka maafisa tarafa, maafisa watendaji wa kata na vijiji pamoja na waratibu wa elimu kata kwa kushirikiana na waheshimiwa madiwani kuhakikisha kwamba suala la utoro linaondoka, vile vile kuhakikisha kwamba wanafunzi hawapewi kazi ambazo sio za umri wao, kazi ambazo kwa namna moja ama nyingine zimekuwa zikichangia ongezeko la utoro wa wanafunzi mashuleni,pia kusababisha wanafunzi kutokuwa na muda wa kutosha kujisomea, watendaji hao pia wahakikishe kwamba watoto wote wanaojiunga na kidato cha kwanza wanamaliza kidato cha nne.
Aidha ndugu Kambona amezungumzia suala la uchangiaji wa chakula mashuleni, amesema kwamba wazazi wanatakiwa kuchangia vyakula mashuleni ili katika shule zote , za msingi na sekondari wanafunzi waweze kula chakula cha mchana , lakini wazazi wasilazimishwe kuchangia maharage , wakati uwezo wao ni kuchangia mbaazi ambazo bei yake ni nafuu zaidi kuliko bei ya maharage.Na kwamba mbaazi ni chakula halali kama vyakula vingine na kina protini kama ilivyo kwa maharage, hivyo wazazi wasikwazwe kwa kulazimishwa kuchangia maharage wakati wao wana magunia ya mbaazi ndani.
Katika hatua nyingine ndugu Kambona amewaagiza wakuu wote wa shule kununua vyakula vya shule kwa bei ya soko.Ameendelea kusema kwamba kadiri mahindi yanavyoshuka bei, na bei ambazo wakuu hao wa shule wananunua vyakula zinatakiwa ziwe zinashuka, ili fedha zinazobaki katika ununuzi wa vyakula zitumike katika kutekeleza miradi mingine ya maendeleo.
Ndugu Kambona pia aamezungumzia kuhusu fedha za mfuko wa pamoja ‘basket fund’ zilizopo katika vituo vya afya na zahanati , ambazo zilitolewa tangu mwaka jana kwa ajili ya ukarabati , amewaomba waheshimiwa madiwani kuhakikisha kwamba ukarabati unafanyika katika vituo vya afya na zahanati zote .
Wilaya ya Kiteto imekuwa ya mfano wa kuigwa kwa uibuaji na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.Miradi ambayo imekuwa ya manufaa makubwa kwa jamii yote.
...........MWISHO............
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa