Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, CPA. Hawa Abdul Hassan, ameipongeza Timu ya Wataalamu wa Halmashauri (CMT) na watumishi wa Halmashauri kwa kuendeleza ufanisi na weledi katika kipindi chote ambacho baraza la madiwani lilikuwa limevunjwa.
Akizungumza wakati wa Mkutano wa Kwanza wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto uliofanyika Desemba 02, 2025, CPA. Hawa alisema wataalamu waliendeleza utekelezaji wa majukumu ya Halmashauri bila kuyumba, ikiwemo kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani na miradi ya maendeleo.

Katika taarifa aliyoiwasilisha, alisema kuwa kati ya mwezi Julai hadi Oktoba 2025, Halmashauri imekusanya Tsh. 2,321,489,279, sawa na asilimia 46.40 ya lengo la mwaka, ikiwa juu ya lengo la kipindi husika la asilimia 33.3.
Aidha, Halmashauri imeendelea kutoa mikopo ya makundi maalumu ambapo Tsh. 155,569,108.36 zimetolewa kwa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, huku uhakiki wa vikundi ukiendelea ili kuhakikisha walengwa wanafikiwa kwa usahihi. Kwa upande wa marejesho, kati ya Tsh. 133,352,100 zilizotarajiwa kurejeshwa katika kipindi cha Julai–Novemba, kiasi cha Tsh. 128,626,100 kimerejeshwa sawa na asilimia 96.46.

“Nitoe pongezi za dhati kwa Menejimenti na watumishi wote wa Halmashauri kwa weledi, ushirikiano na ufanisi wa kazi kwa kipindi chote ambacho Waheshimiwa Madiwani hawakuwepo,” alisema CPA. Hawa.
Katika kikao hicho, alitoa pia pongezi kwa Mhe. Athumani Hamisi Kilimo kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri na kumuahidi ushirikiano katika utekelezaji wa shughuli za Halmashauri. Vilevile, aliwapongeza Madiwani kwa kuaminiwa na wananchi.

CPA. Hawa pia alimshukuru Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Mhe. Abdala Bundala, kwa uongozi wenye hekima na mchango wake katika kipindi cha miaka mitano.

Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa