Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Mhe. Lairumbe Mollel akiongoza kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto. Upande wake wa kulia ni makamu mwenyekiti wa halmashauri Mhe. Hassan Benzi na upande wake wa kushoto ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri Ndg. Tamim Kambona.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Mhe. Lairumbe Mollel , makamu mwenyekiti wa halmashauri Mhe. Hassan Benzi na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri Ndg. Tamim Kambona wakifuatilia kwa makini uwasilishwaji wa taarifa za maendeleo ya kata katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri.
Wahe. Madiwani wakiwa katika Kikao cha baraza la madiwani ndani ya ukumbi wa halmashauri.
Wahe. Madiwani wakiwasilisha taarifa za maendeleo ya kata zao katika kikao cha baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Kiteto kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri .
Wataalamu kutoka idara mbalimbali za halmashauri ya wilaya ya Kiteto wakiwa katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri
.......... HABARI KAMILI ..........
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto mheshimiwa Lairumbe Mollel amewataka Wahe. madiwani kuhakikisha wanajenga vituo vya afya katika kata zao, ili wilaya isiwe tegemezi katika huduma za afya.Mhe Mollel ameyasema hayo wakati akiongoza kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri mapema leo .
Mheshimiwa Mollel amesema kwamba yeye binafsi hajisikii vizuri kuona kwamba wananchi wa wilaya ya Kiteto wanakwenda kupata huduma za afya nje ya wilaya kwa sababu tu hakuna vituo vya afya katika maeneo yao hali ya kuwa uwezo wa kujenga vituo vya afya upo.
Akisisitiza kuhusu ujenzi wa vituo vya afya , Mhe. Mollel amesema ‘‘Tunataka wilaya yetu hii isiwe tegemezi,wananchi wetu wanakata CHF halafu wanakwenda kutibiwa nje ya wilaya.Huduma zinaigiliana ,lakini na sisi tujitahidi kwa nguvu zetu, ili watu waje kwetu badala ya sisi kwenda kwao kila wakati. Shida ni kuanzisha ujenzi wa kituo cha afya tu, tukishajenga serikali inaleta hela inamalizia ujenzi, wananchi wetu wanakuwa na huduma ndani ya maeneo yao’’.
Kadhalika Mhe. Mollel amewataka madiwani kujipanga kutekeleza miradi ya maendeleo katika kata zao kwa wakati uliopo. Akisisitiza kuhusu hilo Mhe. Mollel amesema ‘‘Jamani tuna muda mchache sana wa kufanya kazi za maendeleo katika kata zetu.Tunaelekea kwenye uchaguzi, tutachagua kamati ya siasa, tutaenda kuchagua wenyeviti wa vijiji, serikali za mitaa ,tutashindwa kufanya miradi mwakani, kwa hiyo niwaombe sana hilo muwe nalo.Tujipange kwa sasa .Vibali vinatolewa kwa DC kwa ajili ya michango,zile kamati za ukusanyaji tuziandae kuanzia sasa,ili hata mwezi wa 5 na wa 6 umeshapata kibali unaendelea kufanya kazi’’.
Kikao hicho cha baraza la madiwani kimekuwa na ajenda moja tu ambayo ni kuwasilisha taarifa za maendeleo ya kata ambapo waheshimiwa madiwani kutoka katika kata zote 23 wamewasilisha taarifa za maendeleo ya kata zao.