Halmashauri ya Wilaya Kiteto pamoja na Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Makame (WMA Makame) wamesaini mkataba wa miaka 40 ya uvunaji wa hewa ukaa na Kampuni ya Carbon Tanzania (CT ltd) kutoka katika hifadhi hizo.
Halfa ya utiaji wa saini wa Mkataba huo ambayo Mgeni Rasmi alikua Mwenyekiti wa HW Kiteto Mhe. Abdala Bundala, imefanyika katika viwanja vya WMA Makame Agosti 22, 2024, huku ikishuhudiwa na Mkurugenzi Mtendaji (W) CPA. Hawa Abdul Hassan, wajumbe wa bodi pamoja na wanajumuiya wa WMA Makame.
Akiongea katika halfa hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Ndg. Lendukushi Keiya, ameiomba kampuni hiyo kuhakikisha wanarudisha kwa wakati sehemu ya faida ya biashara hiyo kwa Jumuiya na Halmashauri kwani ucheleweshaji wa fedha hizo unakwamisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika taasisi hizo.
Mgeni Rasmi Mhe.Bundala amesema kwamba halmashauri inafurahi kumpata muwekezaji huyo kwani pesa inayopatikana katika biashara hii inasaidia kueleta maendeleo katika wilaya. Aidha alitoa wito wa wanajumuiya na wananchi kwa ujumla kutunza mazingira kwani biashara ya hewa ukaa haiwezi kufanyika endapo mazingira yataharibiwa.
Nae Mkurugenzi Mtendaji CPA. Hawa Abdul Hassan, aliwashukuru CT Ltd. na kusema kwamba kupitia biashara hiyo wameweza kunufanika na vyumba vya madarasa, barabara, ofisi za vijiji na visima mbali na fedha zinazolipwa moja kwa moja kwa HW kama mapato ya ndani.
“Turithishe jamii kutunza mazingira na waone faida tulizopata kupitia kutunza mazingira”, ameongeza CPA. Hawa.
Mkurugenzi wa Fedha wa CT ltd, Ndg. Alphael Jackson, alishukuru kwa ushirikiano wanaopata kutoka kwa HW, bodi na vijiji na kusihi kuendelea kutunza misitu ili kuendelea kupata fedha kupitia misitu hiyo.
Tangu kuanza kwa biashara hii, Jumuiya imeshapokea zaidi ya 3.7 bilioni ambapo 40% imeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo, 10% imepokelewa na HW Kiteto kama mapato ya ndani. Pia 15% ya pesa iliyopokelewa imetumika kwaajili ya ufadhili wa elimu kwa wanafunzi wa vijiji wanachama, 20% imetumika kwaajili utawala na 15% kwaajili ya doria.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa