Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto leo Januari 31, 2026 imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi minne ya maendeleo yenye jumla ya thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.4, hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali katika kusimamia matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na rasilimali zao.
Akizungumza katika ziara hiyo kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Athumani Hamisi Kilimo, ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiamini Kiteto na kuelekezea fedha nyingi za maendeleo, akisema hatua hiyo ni ushahidi kuwa wa serikali inasikiliza na na kutenda.
Mhe. Kilimo amesema fedha hizo zimekuwa chachu ya kuimarisha huduma za afya na elimu, huku akisisitiza kuwa jukumu la viongozi wa ngazi ya Halmashauri ni kuhakikisha kila shilingi inatumika ipasavyo na kuleta tija kwa wananchi.
Aidha, Kamati hiyo ilitoa shukrani kwa Mbunge wa Jimbo la Kiteto, Mhe. Edward Ole Lekaita kwa juhudi zake za kisiasa na kiuwakilishi katika kufuatilia na kusimamia upatikanaji wa fedha za miradi ya maendeleo kutoka Serikali Kuu, akielezwa kuwa daraja muhimu kati ya wananchi na Serikali.
Wajumbe wa Kamati walieleza kuridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo, huku wakisisitiza umuhimu wa miradi kukamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora, ili thamani ya fedha ionekane na wananchi waanze kunufaika na huduma husika kwa mujibu wa malengo ya Serikali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto ambaye ndiye mtekelezaji wa shughuli za Halmashauri CPA, Hawa Abdul Hassan, ameahidi kuendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu wa miradi ya maendeleo kwa kushirikiana na Wataalamu ili kuhakikisha thamani ya fedha inayoletwa na serikali inaridhisha.
Miradi iliyokagukiwa na Kamati hiyo ni ujenzi wa jengo jipya la OPD katika Hospitali ya Wilaya iliyopo Kata ya Kibaya wenye thamani ya shilingi milioni 800. Pia ilikagua ujenzi wa jengo la OPD katika Kijiji cha Irkiushbor katika Kata ya Makame lenye thamani ya shilingi milioni 250.
Mbali na sekta ya afya, Kamati ilikagua pia miradi ya elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa matatu na matundu sita ya vyoo kwa elimu ya msingi, pamoja na madarasa mawili na matundu sita ya vyoo kwa elimu ya awali katika Shule ya Msingi Oloimugi (Oltaret) katika kata ya Namelock, mradi wenye thamani ya shilingi milioni 157.7. Aidha, ziara hiyo ilihitimishwa kwa ukaguzi wa ujenzi wa mabweni mawili katika Shule ya Sekondari Dosidosi yenye thamani ya shilingi milioni 260.

Ziara hiyo ni moja ya mkakati wa kiutawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto katika kusimamia maendeleo, kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa