Mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii (W) Ndg. Joseph Mwaleba akifungua kikao cha kamati ya lishe ya wilaya ya Kiteto kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji .Aliyekaa upande wake wa kushoto ni mganga mkuu wa wilaya ya Kiteto Dkt. Melkiadi Paschal Mbota.
Wajumbe wa kamati ya lishe ya wilaya ya Kiteto wakipitia kwa makini taarifa mbalimbali zilizomo kwenye mafaili,kabla ya kuanza kwa kikao.
Wajumbe wa kamati ya lishe ya wilaya ya Kiteto wakiendelea na kikao .Kikao cha kamati ya lishe kimefanyika katika ukumbi wa hospitali ya wilaya ya Kiteto mapema jana.
.......HABARI KAMILI...........
Kamati ya lishe ya wilaya ya Kiteto imezitaka idara ya kilimo, chakula na ushirika pamoja na idara ya mifugo na uvuvi kwa kushirikiana na idara ya afya kutoa tahadhari kuhusiana na sumukuvu.Azimio hilo limefikiwa katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hospitali ya wilaya ya Kiteto mapema jana.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wajumbe wa kamati hiyo ,wamesema kwamba jamii ya Kiteto bado haina uelewa wakutosha kuhusu sumukuvu ,jambo ambalo linasababisha kuendelea kuhifadhi nafaka katika hali ambayo ni hatarishi kwa walaji wa nafaka hizo.
Wajumbe hao wamesema kwamba kumekuwepo na matumizi ya viuatilifu vya kuhifadhia nafaka ambavyo ni sumu, na viautilifu vingine ambavyo viko katika hali ya kimiminika (maji), viuatilifu hivi ambavyo viko katika hali ya kimiminika vikiwekwa katika nafaka,na nafaka hizo zisipokaushwa vizuri,zinakuwa na unyevu unyevu ambao husababisha nafaka hizo kutengenzeza sumu ijulikanayo kama sumukuvu, vilevile wakulima wengi wamekuwa na mazoea ya kuweka nafaka chini kwenye udongo, au kwenye sakafu, nafaka zinapowekwa chini kwenye udongo au kwenye sakafu, huvuta unyevu kutoka ardhini, unyevu huo hutengeneza ukungu katika nafaka, hali hiyo husababisha nafaka hizo kuwa na sumukuvu .
Akizungumza wakati wa majadiliano ,mganga mkuu wa wilaya ya Kiteto Daktari Malkiadi Paschal Mbota amesema” Sumukuvu bado ni tatizo kubwa ,jamii bado haina uelewa wa kutosha katika kuhifadhi mazao yao,hususani nafaka kama mahindi, karanga na mtama ,ili mazao hayo yasiweze kupata sumukuvu,jambo ambalo ni hatari sana kwani madhara ya sumukuvu ni makubwa.Sumukuvu inapoingia mwilini kidogo kidogo,madhara yake hayawezi kuonekana kwa mara moja,lakini moja wapo ya madhara yanayoweza kuonekana baada ya muda mrefu ni saratani ya ini”.
Daktari Mbota pia amezungumzia kuhusu matumizi ya dawa zisizoruhusiwa kama DDT ambazo baadhi ya wakulima wamekuwa wakizitumia kuweka katika nafaka zao ili zisishambuliwe na wadudu.Amesema kwamba dawa hizo zinapotumika , ni sumu , hivyo zina madhara makubwa sana katika miili ya walaji wa nafaka hizo.Hivyo jitihada za ziada zinahitajika kuweza kuwajengea wakulima uelewa wa kutosha kuhusu madhara ya dawa hizo.
Kwa upande wake Mkuu wa idara ya Mifugo na uvuvi Daktari Wiliam Msuya amefafanua zaidi kuhusu sumukuvu , hapa daktari Msuya amesema “ Sumukuvu haiko kwenye nafaka peke yake,bali inaweza kuwepo hata kwenye nyama, pamoja na mazao ya mifugo kama vile maziwa, kutokana na mifugo kula vyakula ambavyo vina sumukuvu, hivyo jamii inapaswa pia kutahadharishwa kwamba mifugo inapokula mabua,au pumba ambazo zina sumukuvu, nyama pamoja na mazao yake yote ambayo hutumika kama chakula kwa binadamu vyote vinaweza kuwa na sumu hiyo”.
Naye mjumbe wa kamati ya lishe, mchungaji wa kanisa la kiinjili la Kirutheri Tanzania ( KKKT) usharika wa Kibaya ambaye amewakilisha viongozi wa madhehebu ya kikristo wilayani Kiteto, Mchungaji Wankembeta Marco Msingi amesema kwamba ni vema tahadhari ikatolewa mapema kuhusiana na sumukuvu,na namna ya kuiepuka, na kwamba wahusika wanaopaswa kutoa elimu pamoja na tahadhari hiyo watumie njia zozote zinazowezekana kwa haraka, ili kuepuka maangamizi yanayoweza kutokea kwa siku za usoni kutokana na ulaji wa vyakula ambavyo vina sumukuvu badala ya kukaa kusubiri bajeti.
Katika hatua nyingine mjumbe wa kamati ya lishe ambaye pia ni muwakilishi wa BAKWATA wilaya ya Kiteto,ndugu Ibrahim M. Bory ameitaka idara ya Kilimo,chakula na ushirika kwa kushirikiana na idara ya afya, kupita na kukagua bidhaa ya unga wa lishe unaotengenezwa na vikundi mbalimbali pamoja na watu binafsi,kuhakikisha kama bidhaa hiyo ni salama kwa matumizi ya binadamu, lengo likiwa ni kuepuka madhara yanayoweza kuwapata watumiaji ,ambao kwa asilimia kuwa ni watoto.
Kamati ya lishe wilaya ya Kiteto imekaa kikao chake cha robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2018/2019, ambapo taarifa za shughuli za lishe kutoka BAKWATA, idara na vitengo mbalimbali vya halmashauri kama vile idara ya kilimo,chakula na ushirika, idara ya mipango, idara ya elimu msingi, idara ya elimu sekondari, idara ya mifugo na uvuvi, idara ya afya na usafi wa mazingira, idara ya maendeleo ya jamii, kitengo cha Afya ya uzazi na mtoto, Kitengo cha dawa na vifaa tiba pamoja na Kitengo cha lishe zimewasilishwa.
.............MWISHO...............
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa