Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kiteto, Ndg. Ally Kichuri, amewataka Makarani Waongozaji Wapiga Kura kuhakikisha wanajiepusha kuwa chanzo cha malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na badala yake kushirikiana kwa karibu na mawakala wa vyama hivyo katika vituo vya kupigia kura.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa makarani waongozaji wapiga kura, wasimamizi wa vituo na wasaidizi wao, yaliyofanyika Oktoba 25, 2025, Ndg. Kichuri alisema ni muhimu watendaji hao wa muda wa uchaguzi wakatenda haki na kuzingatia maadili ili kulinda taswira ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

“Ni wajibu wenu kuhakikisha mnafanya kazi kwa weledi, uadilifu na ushirikiano mzuri na mawakala wa vyama vya siasa. Msigeuke kuwa chanzo cha malalamiko au migogoro katika vituo vya kupigia kura,” alisema Kichuri.
Aidha, aliwahimiza makarani hao kusoma kwa umakini Katiba, Sheria, Miongozo na Maelekezo yatakayotolewa na Tume, ili wawe na uelewa mpana wa majukumu yao.

Ndg. Kichuri pia aliwataka makarani hao kufanya kazi kwa ushirikiano, kuhakiki vifaa vya uchaguzi watakavyokabidhiwa na kuhakikisha wanawahi kwenye vituo vyao siku ya uchaguzi.
Mafunzo hayo ya siku tatu yameanza kwa kundi la makarani Oktoba 25, 2025, na yataendelea kwa wasimamizi wa vituo na wasaidizi wao kuanzia Oktoba 26 hadi 27, 2025.
Kabla ya mafunzo hayo kuanza, makarani hao walikula kiapo cha kutunza siri na kiapo cha kujitoa uanachama kwenye vyama vya siasa.

Mafunzo hayo ambayo yamejumuisha makarani 598, yamefanyika katika vituo vinne tofauti ambavyo ni Maktaba Kibaya, Kiteto Sekondari, Engusero na Lesoit, ambapo washiriki wamepatiwa mafunzo ya vitendo na maelekezo ya msingi ya jinsi ya kusimamia zoezi la upigaji kura kwa amani na utulivu.

Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa