Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mhe. Remidius Mwema, leo Oktoba 27, 2025 ameongoza Matembezi ya Amani yaliyolenga kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
Akizungumza baada ya matembezi hayo, Mhe. Mwema alisema matembezi hayo yalilenga kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia kwa kufuata misingi ya kikatiba.
“Huu ni uchaguzi wa wote, na kupiga kura ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania mwenye sifa. Ni wajibu wetu kujitokeza kwa amani na utulivu kuchagua viongozi wetu,” alisema Mhe. Mwema.
Aidha aliwapongeza wananchi kwa mwitikio mkubwa, akibainisha kuwa mwamko huo unaonesha uzalendo na umoja wa wana Kiteto. Pia aliwataka viongozi wa dini, taasisi na jamii kuendelea kuhamasisha wananchi wengine hadi siku ya uchaguzi.

Aidha, aliwakumbusha wananchi kuzingatia taratibu za uchaguzi ikiwemo kukaa umbali wa mita 500 kutoka kituo cha kupigia kura baada ya kupiga kura, na kusisitiza kuwa usalama uko imara katika Wilaya nzima ya Kiteto.
“Hakuna sababu ya kuwa na hofu. Vyombo vya ulinzi vipo tayari kuhakikisha kila mwananchi anapiga kura kwa amani na utulivu. Kiteto ni salama,” alisisitiza.

Mhe. Mwema alitoa wito kwa wananchi kuepuka matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi wanapobaini dalili za uvunjifu wa amani.
Matembezi hayo yalihudhuriwa na viongozi wa dini, watumishi wa umma na sekta binafsi na makundi mbalimbali ya kijamii, yalianzia Shule ya Msingi Boma Sidan na kuhitimishwa katika Uwanja wa Michezo Kibaya kwa mazoezi ya viungo na michezo mbalimbali.
"KURA YAKO HAKI YAKO, JITOKEZE KUPIGA KURA"
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa