Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena, amekabidhi vifaa vya kazi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, CPA. Hawa Abdul Hassan, katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Kitaifa yaliyofanyika leo Septemba 29,2025.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na vishikwambi 32 kwa ajili ya wataalamu wa mifugo pamoja na dozi 15,000 za chanjo ya Kichaa cha Mbwa. Hatua hii inalenga kuongeza ufanisi wa utoaji huduma za mifugo kwa wananchi wa Kiteto na kuhakikisha chanjo za kichaa cha mbwa zinaendelea kutolewa ili kuilinda jamii na ugonjwa huu hatari.
Kupokelewa kwa vishikwambi hivyo kutarahisisha ukusanyaji na uhifadhi wa taarifa za mifugo, kufuatilia mwenendo wa utoaji chanjo, na kurahisisha mawasiliano kati ya wataalamu wa mifugo katika ngazi za kata, vijiji na wilaya.
Aidha, upatikanaji wa dozi 15,000 za chanjo ya kichaa cha mbwa utaiwezesha Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto kuendelea kutoa chanjo hizo bure kwa wananchi wote. Utoaji huu wa chanjo bila malipo ni msaada mkubwa kwa jamii na utachochea mwitikio wa wananchi kuwachanja wanyama wao ili kuzuia maambukizi.
Huduma ya chanjo hiyo ya Kichaa cha Mbwa itaendelea kutolewa bure na wataalamu wa mifugo kupitia ofisi za kata na vijiji wilayani hapa ikiwa ni sehemu ya juhudi endelevu za serikali kuhakikisha kila mnyama anapata kinga.
Maadhimisho haya ya kitaifa yalilenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa chanjo kama kinga bora dhidi ya Kichaa cha Mbwa na kuonesha dhamira ya Serikali katika kulinda afya za binadamu na wanyama.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa