Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papian akizungumza na wakazi wa kijiji cha Kijungu katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa ofisi ya kata ya kijungu.
Wakazi wa kijiji cha Kijungu wakiwa wamekusanyika kumsikiliza mbunge wao sambamba na kuwasilisha kero zao .
...........HABARI KAMILI...............
Mbunge wa jimbo la Kiteto Mheshimiwa Emmanuel Papian amewataka wakazi wa kijiji cha Kijungu kufuata mpango wa matumizi bora ya ardhi waliojiwekea ili kuepuka migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara.Mhe. Papian ameyasema hayo wakati akizungumza na wakazi hao katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa ofisi ya kata ya Kijungu,wilayani Kiteto.
Akizungumza katika mkutano huo Mhe. Papian amesema “Wananchi wa kijungu tuna tatizo la migogoro ya ardhi,tulizungumza hapa kama mnakumbuka ,wananchi mnatakiwa kuhakikisha kwamba mnafuata mpango wa matumizi bora ya ardhi, mnapokwenda kupata mwenyekiti,mnapokwenda kupata serikali ya kijiji, hakikisheni mnafuata mpango wa matumizi bora ya ardhi, na muache udalali wa kuuza maeneo, ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima. Udalali wa maeneo umesababisha vijana ambao ni wazawa wa hapa kukosa maeneo ya kulima,kukosa maeneo ya kujenga”.
Aidha Mhe. Papian ameahidi kushughulikia matatizo mbalimbali yanayowakabili wakazi wa kijiji hicho, Akisisitiza kuhusu kuhusu hilo Mhe. Papian amesema “Hapa kuna matatizo mawili matatu,tatizo la kwanza ni chanzo cha maji, hakuna maji,na yaliyopo yako mbali.Hili tunalo ,tumekwenda nalo kwa Mkurugenzi,tunafanya jitihada kuhakikisha kwamba kwa pesa mliyonayo ya mfuko wa maji, na tutaangalia ni namna gani kwa kutumia mapato ya halmashauri ,tunaweza kufunga bomba kule, tusogeze bomba huku tuweke walau kichoteo kimoja,wananchi wapate maji”.
Kadhalika Mhe. Papian amezungumzia kuhusu suala la upungufu wa Mkunga,katika zahanati ya Kijungu, Mhe Papian amesema “ kuna upungufu wa muuguzi mkunga,katika ajira za serikali kwa mwaka 2018/2019 tutapata mtumishi mwingine hapa ili aweze kusaidiana na watumishi wengine walioko hapa, huduma ziendelee kwa salama”.
Mhe. Papian pia ameahidi kushughulikia suala la chumba cha kujifungulia na kitanda cha kujifungulia, ambapo amesema kwamba anafahamu kwamba eneo la wakina mama kujifungulia haliko sawasawa,ni dogo ,na kitanda cha kujifungulia hakiko vizuri , na kwamba jambo hilo wameshalifikisha kwa Mkurugenzi, watalifanyia kazi, eneo hilo litarekebishwa, na kitanda hicho kitapatikana.
Katika mkutano huo wakazi wa kata ya kijungu waliwasilisha kero zao, kero kubwa ikiwa ni ukosefu wa maeneo ya kujenga na maeneo ya kulima, ambapo Mhe. Papian amewataka wanachi hao kuwa watulivu wakati yeye pamoja na serikali ya wilaya wakiendelea kuangalia ni namna gani tatizo hilo linaweza kushughulikiwa,na wananchi hao kupata maeneo kwa ajili ya makazi na ya shughuli za kilimo.
Mhe. Papian amefanya ziara katika kijiji cha Kijungu ,ikiwa ni sehemu ya ziara zake katika jimbo lake kukagua shughuli za maendeleo na kusikiliza kero za wananchi .
..........MWISHO............
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa