Mratibu wa Macho(W) Dkt. Enock Thomas Awary Akimfanyia uchunguzi wa macho mmoja wapo wa watu wenye matatizo ya macho wakati wa maadhimisho ya siku ya macho duniani.
Mganga mkuu (W) Dkt. Paschal Malkiadi Mbota akizungumza wakati wa maadhimisho hayo.
Mratibu wa Macho (W) Dkt. Enock Thomas Awary akizungumza wakati wa maadhimisho hayo.Mratibu wa Trakoma Mkoa mkoa wa manyara kutoka KCCO bi Agnes Lukumay akizungumza wakati wa maadhimisho hayo.Wataalamu wa macho kutoka hospitali ya wilaya ya Kiteto pamoja na Mratibu wa Trakoma Mkoa wa Manyara kutoka KCCO wakiendelea kutoa huduma wakati wa maadhimisho hayo.
Baadhi ya vitendea kazi vinavyotumika katika huduma za uchunguzi na matibabu ya macho kama vinavyoonekana katika picha.
Wagonjwa wa macho wakisubiri kuitwa majina kwa ajili ya kupatiwa huduma katika maadhimisho ya siku ya macho duniani.
Mmoja wa wagonjwa wa macho( Aliye simama mbele ya meza) akiandikisha jina kwa ajili ya kupatiwa huduma,huku wengine (waliokaa kwenye viti ) wakiendelea kupatiwa huduma,na wengine wakisubiri kupatiwa huduma.
Mratibu wa Macho(W) Dkt. Enock Thomas Awary Akiwafanyia uchunguzi wa macho wagonjwa mbalimbali waliofika katika maadhimisho ya siku ya macho duniani.
......HABARI KAMILI......
Wilaya ya Kiteto imeadhimisha siku ya macho duniani kwa kutoa huduma za macho bure.Maadhimisho hayo yamefanyika katika uwanja mkuu wa michezo uliopo katika mji mdogo wa Kibaya.
Katika kuazimisha siku hiyo wataalamu wa macho kutoka idara ya macho hospitali ya wilaya ya Kiteto kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la 'Kilimanjaro Center for Community Opthmology ( KCCO) kupitia mradi wa 'Trachoma Safe ’ wametoa huduma ya uchunguzi wa macho, ushauri, dawa sambamba na kuwapangia tarehe ya kurudi kwa ajili ya upasuaji wagojwa ambao baada ya uchunguzi wameonekana kuhitaji upasuaji.
Akizungumza katika mahojiano mafupi yaliyofanyika uwanjani hapo,Mganga Mkuu wa wilaya ya Kiteto daktari Malkiadi Paschal Mbota amesema kwamba katika wilaya ya Kiteto kuna matatizo mbalimbali ya macho kama Trakoma, mtoto wa jicho,presha ya macho na matatizo ya macho ambayo yanatokana na mionzi.Lakini ugonjwa ambao kitakwimu uko juu zaidi ni ugonjwa wa Trakoma, Trakoma bado ni tatizo kubwa, na kwamba idara ya Afya wilaya kwa kushirikiana na KCCO wamekuwa wakienda katika maeneo yote ya vijijini kutoa huduma za uchunguzi, ushauri, dawa,upasuaji na elimu juu ya umuhimu wa kusafisha uso kwa maji safi pamoja na usafi wa mazingira kwa ujumla kwa lengo la kutokomeza ugonjwa huo.
Kadhalika Daktari Mbota ametoa wito kwa jamii,hususani jamii ya kifugaji kujenga tabia ya kunawa uso kwa maji safi mara kwa mara ili kuepuka ugonjwa wa Trakoma.Sambamba na wito huo, ameeleza kuhusu mkakati wa wilaya katika kukabiliana na ugojwa wa Trakoma pamoja na magonjwa mengine ya macho, daktari Mbota amesema ''Kwa kushirikiana na KCCO tumekuwa tukifika kijiji hadi Kijiji kuwatambua wagonjwa,na tukishawatambua ,madaktari wetu na manesi wamejengewa uwezo wa kutosha kuwapatia huduma zote zinazotakiwa ikiwemo upasuaji,wanaweka mahema hukohuko vijijini wanawafanyia upasuaji ''.
Naye mratibu wa macho wilaya ya Kiteto Daktari Enock Thomas Awary amesema kwamba wamejipanga kuhudumia watu wote watakaofika uwanjani hapo kwa lengo la kupata huduma za macho,na kwamba wale ambao hawatakuwa wamehudumiwa kwa siku ya leo , huduma hiyo itaendelea hadi siku ya Jumamosi ,na watachukua namba za wagonjwa watakaotakiwa kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya kuwapangia tarehe za upasuaji na kuwafuatilia kuhakikisha wanafanyiwa upasuaji.
Daktari Awary ameendelea kusema kwamba huduma wanazotoa ni bure,hivyo watu wote wenye matatizo ya macho wasiache kufika ili wapate huduma.Daktari Awary pia amesema kwamba huduma hiyo itafika hadi vijijini, na kwamba wameshaweka utaratibu mzuri,wameandika barua kwa waganga wafawidhi wa vituo vya afya na zahanati zote ,kuhakikisha kwamba watu wote wanaohitaji huduma hata katika maeneo ya pembezoni wanafikiwa na huduma hiyo.
Katika hatua nyingine mratibu wa mradi wa Trakoma Mkoa wa Manyara kutoka KCCO Bi Agnes Lukumay amesema kwamba lengo la KCCO kufadhili utoaji wa huduma hizo za uchunguzi na matibabu ya macho katika maadhimisho ya siku ya macho duniani ni kuzuia upofu unaoweza kuzuilika.Lukumay pia amesema kwamba takwimu zinaonyesha kwamba kwa mkoa wa Manyara ugonjwa wa Trakoma uko juu zaidi katika wilaya za Kiteto na Simanjiro.
Aidha bi Lukumay amesema kwamba ni vema wananchi wakajitokeza kwa wingi ili kupata huduma hizo za uchunguzi na matibabu ya macho, kwa sababu zinatolewa bure, na ni kwa ajili ya wananchi wote,hivyo wasiache fursa hiyo iwapite.
Shirika la 'Kilimanjaro Center for Community Opthmology' limeanza kazi zake mwaka 2015, kwa mkataba wa miaka 5.Dhima ya shirika hilo ni kutokomeza ugonjwa wa Trakoma ifikapo 2020.Hadi sasa shirika limeshahudumia kwa kuwafanyia upasuaji wa macho wagonjwa wa Trakoma 600.
Katika maadhimisho hayo ,wagonjwa wa macho 379 wamefika uwanjani hapo kwa lengo la kupata huduma, ambapo wagonjwa 205 wamehudumiwa na wengine waliobaki wataendelea kuhudumiwa siku ya kesho Ijumaa na kesho kutwa Jumamosi . Kauli mbiu ya siku ya macho duniani kwa mwaka 2018 ni ’Afya ya macho kwa wote,huduma ya macho kila mahali’
....MWISHO......
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa