Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto kupitia Idara ya Afya Kitengo cha Lishe imefanikiwa kufanya maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji (SALIKI) katika vijiji 10 kupitia ufadhili wa USAID Afya Yangu Mama na Mtoto.
Katika maadhimisho hayo ambayo yalianza Septemba 10, wataalam wa Lishe kutoka Ofisi ya Mkurugenzi (W) walitumia majukwaa ya SALIKI kuifundisha jamii kuhusu makundi sita ya chakula na kuhamasisha ulaji wa mlo kamili ili kujenga afya bora kwa Taifa bora.
Aidha wataalamu hao walitumia majukwaa hayo kuifundisha jamii kwa vitendo namna bora ya kupika chakula kwa kuzingatia makundi mbalimbali ya chakula na kwa kutumia mahitaji yanayopatikana kwenye jamii husika kama vile maziwa, viazi na na mbogamboga kama vile maboga.
Aidha katika majukwaa hayo ya SALIKI kumefanyika zoezi la tathmini ya hali ya lishe kwa watoto na vijana balehe pamoja na kutoa dawa za minyoo na chanjo kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.
Mkuu wa Kitengo na Lishe (W) Ndg. Beatrice Lutanjuka amesema kwamba maadhimisho haya yanapaswa kufanyika kwenye kila robo ya mwaka na katika kila kijiji, lengo likiwa ni kusogeza huduma za afya na lishe karibu na jamii ikiwemo kutoa elimu ya lishe na chanjo ili kuweza kupambana na utapia mlo kwa watu wa rika mbalimbali pamoja na kupambana na udumavu.
Aidha Ndg. Lutanjuka amewashukuru wadau ambao ni USAID Afya Yangu Mama na Mtoto kwa ufadhili wao ambao umewezesha kufanyika kwa maadhimisho hayo kwa vijiji kumi ambayo kilele kilifanyika Septemba 13,2024 katika Kijiji cha Mbeli ambapo Mgeni Rasmi alikua Katibu Tawala wa Wilaya Ndg. Mufandii Msaghaa.
Aidha, Ndg. Lutanjuka amewaomba wadau hao kuendelea kushirikiana na Halmashauri katika masuala ya Afya na Lishe ili kuisaidia Halmashauri kuendelea kutekeleza Mpango wa Pili Jumuishi wa Taifa wa Masuala ya Lishe (NMNAP II).
Tanzania Bara inatekeleza NMNAP II mpango ambao una lengo la kutoa mwongozo wa utekelezaji wa afua za lishe Tanzania Bara kwa kipindi cha Miaka mitano 2021/22 – 2025/26 ili kuweza kuimarisha mikakati ya kukabiliana na aina zote za utapia mlo kwa watu wa rika zote.
Matatizo ya utapia mlo yana athari kubwa kwa mtu mmoja-mmoja, kaya, jamii na Taifa kwa ujumla wake na hivyo kuchangia kupungua kwa kasi katika kufikia malengo ya maendeleo; kiafya, kiuchumi na kijamii.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa