Katika jitihada za kuinua uchumi wa wananchi na kuhakikisha usalama wa chakula, Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto imeamua kujenga ghala la kisasa la kuhifadhi mazao lililogharimu kiasi cha shilingi milioni 149,680,000 ikiwa chanzo cha fedha ni mapato ya ndani ya halmashauri.
Lengo kuu la mradi huu ni kutoa huduma za kiutawala kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala kwa kuwasaidia wakulima kuongeza thamani ya mazao yao na kuhakikisha mazao yanahifadhiwa kwa usalama kabla ya kuingia sokoni. Ghala hili litakuwa na uwezo wa kuhifadhi kati ya tani 437.5 hadi 600.
Kukamilika kwa ghala la kisasa kutakua na manufaa makubwa kwa wakulima na jamii kwa ujumla. Kwanza, litaongeza ubora na thamani ya mazao, jambo litakalowawezesha wakulima kupata bei bora na yenye tija. Pili, litakuwa kituo rasmi cha ukusanyaji wa mazao kwa taasisi kama NFRA pamoja na sekta binafsi.
Faida nyingine ni kuimarika kwa usalama wa chakula, kupunguza gharama za usafirishaji na kuongezeka kwa ajira hasa kwa kina mama na vijana. Vilevile, mradi unatarajiwa kuchangia kuongezeka kwa mapato ya halmashauri, hivyo kuongeza uwezo wake wa kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.
Kwa ujumla, ujenzi wa ghala la kisasa ambalo limejengwa katika kata ya Kibaya, ni hatua muhimu kuelekea maendeleo endelevu ya kilimo na ustawi wa jamii.
Jiwe la msingi la ujenzi wa ghala la kisasa liliwekwa Julai 13, 2025 na kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 Ndugu.Ismail Ali Ussi.
Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi, kiongozi huyo alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri pamoja na watendaji wengine kwa kuendelea kutii maagizo ya kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia mapato ya ndani.
"Mkurugenzi nakushukuru wewe pia ni miongoni mwa wakurugenzi pamoja na watendaji wenzako wote ambao mmeendelea kutii maelekezo na maagizo ya Dkt. Samia aliwaelekeza wakurugenzi wote nchini kuhakikisha mnatenga fedha za mapato ya ndani kujenga miradi mbalimbali ya kimaendeleo ambayo inawasaidia wananchi leo hii tumekuja kujionea ghala hili kwakweli ghala hili la kisasa ni ghala lenye ubora ambalo litaenda kuwasaidia wananchi wengi ambao watakuja kuhifadhi bidhaa zao hapa". Alisema Ndugu. Ussi.
Utekelezaji wa mradi wa ghala la kisasa umefikia asilimia 70.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa