Katika kupambana na changamoto za Lishe, Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto imekua ikitekeleza shughuli mbalimbali na hivi karibuni imeanzisha shughuli ya ufugaji wa sungura kupitia wanafunzi wa klabu za lishe kutoka shule za msingi na sekondari.
Mbali na hilo Halmashauri pia inatekeleza mradi wa ufugaji wa samaki kwenye jamii kwa lengo kuu la kuboresha afya za wananchi ikiwepo kupambana na matatizo yatokanayo na lishe duni.
Hadi sasa mradi wa ufugaji wa sungura unatekelezwa kupitia klabu za lishe shuleni katika shule 10 na lengo la mradi ni kuzalisha sungura na kusambaza katika shule zote 128 (msingi na sekondari).
Utekelezaji wa mradi kupitia wanafunzi unalenga kuwapa wanafunzi ujuzi na usambazaji elimu ya lishe yenye kuelezea faida za nyama ya sungura na samaki kiafya ikiwa ni nyama nyeupe isiyo na mafuta mabaya hivyo kukabiliana na magonjwa yasiyo ambukizwa kama vile shinikizo la damu.
Aidha lengo la mradi wa samaki ni kuzalisha vifaranga aina ya sato na kupandikiza kwenye mabwawa sita ya asili ambayo ni Pori namba moja, Namelock, Orkitikit Asamatwa, Partimbo na Katikati ili kuongeza upatikanaji wa samaki kwa jamii.
Julai 13, 2025 katika mbio za Mwenge za Mwaka 2025 wilayani hapa , kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Ndg Ismail Ali Ussi, alitembelea banda la shughuli za mapambano dhidi ya changamoto za lishe.
Akiwa katika banda hilo Ndg. Ussi alisema kwamba wamefarijika kuona wanafunzi wadogo wakiendelea kujifunza mambo ya lishe.
" Ni imani yangu wanafunzi hawa watakua waadilifu na wataenda kuwafundisha wazazi na wenzao na wataenzi klabu hizo za lishe", alisema Kiongozi huyo.
Aidha Kiongozi huyo alisema kwamba kilimo sio lazma mtu aende shambani na anaamini kwa ufugaji wa samaki na sungura wanafunzi watakua mabalozi wazuri kwa Kiteto.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa